WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania washirikiane katika kuulinda na kuutetea Muungano wa Tanzania pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kamwe wasiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kuwagawa.

Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika mikutano iliyofanyika wilaya ya Kati na wilaya ya Kusini alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Kusini Unguja.

“Watanzania tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu, hivyo ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu tusiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani watu hao hawana tija.”

Waziri Mkuu ambaye awali alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari ya Bwejuu, mradi wa kilimo cha kisasa Jozani na kuzindua jengo la mama na mtoto Bambi. Amesema hayo yote ni matunda ya muungano hivyo, hawana budi kuendelea kuudumisha.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari ya Bwejuu, Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa mkandarasi anayejenga maabara hiyo awe amekamilisha kazi hiyo.

Pia, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub Mohammed Mahmoud ahakikishe watumishi wanatenga muda wa siku nne kwa wiki kwa ajili ya kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao hususan ya vijiji. 

Vilevile, Waziri Mkuu aliagiza Maafisa kilimo wahamishiwe vijijini ili waweze kuwasimamia vizuri wakulima ikiwa ni pamoja na kuwashauri namna bora ya kulima kwa kufuata kanuni na matumizi mazuri ya pembejeo.

Kadhalika, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wananchi wote bila ya kujali dini, kabila, rangi wala itikadi za chama kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wananufaika na kuhudumiwa bila ya kubaguliwa kwa namna yoyote.

Awali, viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwemo wa vyama vya CUF, NRA, UPDP, NSSR-MAGEUZI waliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuimarisha huduma za kijamii.

Viongozi hao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais Dkt. Ali Mohammed Shein kwa sababu viongozi hao wanafanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahudumia wananchi.

“Maendeleo hayana chama naunga mkono jitihada zinazofanywa na SMT na SMZ na nimefurahia ziara ya Waziri Mkuu hapa kisiwani Unguja na ninamuunga mkono Rais Dkt. Magufuli tumepata maendeleo ambayo hatukuyatarajia,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa NRA Bw. Khamis Faki katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shehia ya Bambi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...