Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette N. Dissing-Spandet akizungumza na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye ofisi za THBUB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.
Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette N. Dissing-Spandet (kulia) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu katika Maktaba ya THBUB alipokuwa akioneshwa mazingira ya ofisi hizo ambazo zilijengwa kwa msaada wa Denmark.
Afisa wa THBUB, Omary Limu (kushoto) akimuonesha Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette N. Dissing-Spandet baadhi ya tuzo katika maktaba hiyo ambazo tume ilizipata kufuatia ushiriki wake katika matukio mbalimbali nchini na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akimuonesha Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette N. Dissing-Spandet maeneo mbalimbali ya ofisi za THBUB zilizopo jijini Dar es Salaam.



Na Mbaraka Kambona,

Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette N. Dissing-Spandet, ameieleza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuwa wataendelea kufanyakazi kwa karibu na tume kufuatia mahusiano mazuri ya muda mrefu yaliyojengeka baina ya Denmark na Tanzania.

Dissing-Spandet alitoa ahadi hiyo katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye ofisi za THBUB jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma baina yake na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.

Alisema kuwa Denmark itaendelea kufanya kazi na THBUB na itaendelea kuisaidia kutekeleza majukumu yake ya kuhamasisha, kutetea na kulinda haki za binadamu nchini.

“Denmark imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na THBUB kwa muda mrefu sasa, na tupo tayari kuendeleza ushirikiano wetu, tumeweza kufanya kazi kwa karibu kutokana na mahusiano mazuri ya muda mrefu baina ya nchi zetu mbili”, alisema Dissing-Spandet

Kwa mujibu wa Balozi huyo, alisema kuwa ni muhimu katika nchi yoyote kuwa na taasisi kama THBUB kwa kuwa zinasaidia nchi katika kuhamasisha uzingatiwaji wa masuala ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Mwenyekiti wa THBUB, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alionesha kuridhishwa kwake na ushirikiano ulipo baina ya tume na Denmark na kusema kuwa ushirikiano huo umesaidia sana tume kuweza kutimiza majukumu yake kwa kiasi kikubwa.

“Tunashukuru kwa jitihada zenu za dhati za kutuunga mkono, Denmark mmekuwa washirika wa mwanzo kabisa kuisaidia tume, na kupitia msaada wenu tume iliweza kujenga jengo hili la Haki House ambalo ndio tumekuwa tukilitumia kama ofisi zetu...Ahsante sana”, Jaji Mwaimu alimshukuru Balozi huyo

Kamishna wa THBUB, Nyanda Shuli alisema katika kikao hicho kuwa moja ya mipango ya THBUB mwaka huu ni kufanya ufuatiliaji wa uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu, na kwamba mpaka sasa wameshaanza kufuatilia mchakato wa daftari la mpiga kura.

“Miongoni mwa mipango yetu mwaka huu wa uchaguzi ni kuwa na mikutano ya majadiliano na wadau mahususi ikiwemo Jeshi la Polisi, Vyama vya Siasa na Tume ya Uchaguzi ili kukumbushana umuhimu wa kuwa na uchaguzi wa amani nchini”, alieleza Shuli

Ziara ya Balozi huyo kwa tume ni ya kwanza ambayo ililenga katika kufahamiana na kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya THBUB na Denmark katika kuimarisha uzingatiwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...