Na Karama Kenyunko, Michuzi Globu ya jamii

MFANYABIASHARA James Rugemalira ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amemuandikia barua Gavana wa Benki Kuu ya Tanzani(BoT), akimuomba amuorodheshee majina ya watu wote waliopokea fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ili ajisafishe kwani yeye hakupokea hata senti moja.

Hata hivyo Gavana alimjibu atatoa orodha hiyo pale atakapopata amri halali ya Mahakama ya kumtaka kufanya hivyo. Pia Rugemalira amedai ameandika notisi kwa taasisi tisa za serikali ikiwemo ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga akiomba Mahakama hiyo imuondoe katika kesi ya hiyo ya uhujumu uchumi inayomkabili endapo DPP hataiondoa.

Rugemalira amedai hayo yote leo Februari 13, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.

Amezitaja taasisi zingine kuwa ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Diwan Athuman, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa BOT, Kamishna wa TRA Kamishna wa Magereza, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Clement Mashamba na Msajili wa Mahakama ambapo alidai taasisi zote zimepokea taarifa hiyo.

Rugemalira alinyoosho mkono Mahakamani hapo na kudai kuwa aliandika barua kwenda BOT huku akieleza kwamba yeye hajapatiwa hata senti moja kutoka kwenye akaunti ya Escrow na fedha alizopewa yeye ni zile zilizotolewa kwa amri ya Mahakama kwa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP).

Awali, Rugemalira alidai mahakamani hapo kuwa aliandika barua kwenda kwa Kamishna wa TRA akieleza namna Benki ya Standard Chartered ya Hong kong walivyokua wakikwepa kodi na ushuru wa forodha wa Sh.bilioni 1.5.

Alidai ameandika barua ya nyongeza na kuikabidhi Takukuru ili watakapotoa majibu watoe kwa usahihi.Pia mshtakiwa huyo aliomba kukutana na Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon kabla ya kwenda mahabusu kwa ajili ya kumpa ufafanuzi kuhusu kesi hiyo na kama hawatamtoa katika kesi hiyo ataleta maombi maalum ya kutaka kuondolewa kwenye kesi hiyo.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Mbali na Rugemalira, washitakiwa wengine ni mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power (IPTL) na Mwanasheria wa IPTL Joseph Makandege.

Makandege anadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuongoza genge la uhalifu, katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali akishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.

Pia washitakiwa Seth na Rugemalira kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh.309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19,mwaka 2017.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...