Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Februari 21, 2020 ilipitia taarifa mbalimbali za mechi ya Ligi Kuu Vodacom (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) zinazoendelea hivi sasa.
LIGI KUU

Mechi namba 218- Azam FC 1 vs Coastal Union FC 2. 

Klabu ya Azam FC imetozwa faini ya Tsh 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la timu hiyo kuchelewa kutoka uwanjani hata Kamishna alipowaita walikaidi amri ya kutoka vyumbani na golikipa wa timu hiyo kuchelewa zaidi na alipofika uwanjani kushindwa kuwapa mikono timu pinzani (Coastal Union) kwenye mchezo uliofanyika February 15, 2020 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(43) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 220- Yanga SC 0 vs Tanzania Prisons 0

Timu ya Yanga SC imetozwa
faini ya Tsh 500,000 (laki tano) kwa kosa la timu hiyo kushindwa kuwasilisha fomu ya
wachezaji wao kwenye Pre match meeting ya mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mchezaji wa Yanga SC Bernard Morrison amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons FC Jeremia Juma wakati mpira ukiwa umesimama kwenye mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 74B Stand United FC 1 vs Gwambina FC 1 

Klabu ya Stand United FC imetozwa faini ya Tsh 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake kufanya vurugu kubwa kwa kurusha mawe kwenye benchi la ufundi la timu Pinzani na kuwapiga waamuzi waliosimamia mchezo huo uliofanyika Februai 1, 2020 uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.
Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 43(1) kuhusu Udhibiti wa klabu.

Endapo vitendo hivyo vitajirudia tena katika mchezo mwingine watakaocheza, Kamati haitasita kuchukua maamuzi makubwa zaidi ikiwemo kuwabadilishia uwanja wa nyumbani klabu ya Stand United (home ground) na kupangiwa uwanja mwingine.
Mechi namba 85 – Iringa United FC 3 vs Mlale FC 0

Timu ya Mlale FC imepewa Onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalam cha maandalizi ya mchezo bila kutoa sababu kwa msimamizi wa mchezo (Kamisaa) kwenye mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Mkwawa mkoani Iringa.
Mechi namba 87- Gwambina FC 1 vs Geita FC 0

Timu ya Geita Gold FC imetozwa faini ya Tsh 200,000 (laki mbili) kutokana na timu hiyo kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa ukaguzi na wakati wa mapumziko kwenye mchezo uliofanyika February 15, 2020 katika uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 34 ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
 Timu ya Geita Gold FC imetozwa faini ya Tsh 200,000 (laki mbili) kutokana na timu hiyo kutotumia mlango uliokuwa umeandaliwa kwa timu wakati wa kuingia uwanjani na badala yake wakatumia mlango wa jukwaa kuu, kwenye mchezo uliofanyika February 15, 2020 katika uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(14) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Klabu ya Gwambina FC imetozwa faini ya Tsh 500,000/ (laki tano) kwa kosa la mashabiki wa timu hiyo kufanya matukio ya kuwashambulia na kuwapiga mashabiki wa Geita FC mara kadhaa katika mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
LIGI DARAJA LA PILI

Mechi namba 31A – Eagle FC 2 vs Rufiji FC 0

Kocha wa makipa wa timu ya Eagle FC Greyson Mwanjombewa ametozwa faini ya Tsh 200,000 na kufungiwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kwa kosa la kumtukana mwamuzi wa akiba katika mchezo uliofanyika Februari 03, 2020 uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(2) kuhusu Udhibiti wa Viongozi.
Mechi namba 30A – Mkamba Rangers FC 1 vs Rufiji FC 3

Klabu ya Mkamba Rangers imetozwa faini ya Tsh 50,000 (elfu hamsini) kwa kosa la kutofika katika kikao cha maandalizi ya mchezo (Pre match meeting) katika mchezo uliofanyika Februari 10, 2020 uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14 (2) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 37A – Mpwapwa FC 1 vs Rufiji FC 0

Timu zote mbili (Mpwapwa FC na Rufiji FC) zimepewa Onyo kali kwa kitendo cha kutomaliza mchezo huo tajwa na kusababisha mchezo kumalizika siku inayofuata kwa kisingizio cha mvua kuwa kubwa na vurugu za washabiki kwenye mchezo huo uliofanyika Februari 15, 2020 na kulazimika kumaliziwa Februari 16, 2020 uwanja wa Mgambo mkoani Dodoma.
Timu ya Mpwapwa FC imepewa Onyo kwa kosa la mashabiki wake kumtolea matusi mwamuzi kwa kutaka mchezo uendelee hata kama uwanja haukidhi vigezo kwa wakati huo kwenye mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 na kulazimika kumaliziwa Februari 16, 2020 uwanja wa Mgambo mkoani Dodoma.
Kiongozi wa timu ya Mpwapwa FC Omary Mustafa anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa kosa la kuanzisha fujo kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kutoa lugha za matusi na kejeli kwa waamuzi katika mchezo uliofanyika Februari 15, 2020 uwanja wa Mgambo Dodoma.
Mechi– Milambo FC 2 vs Mgambo FC 1

Klabu ya Mgambo Shooting FC imetozwa faini ya Tsh 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake kumvamia na kuanza kumpiga ngumi mwamuzi wa mchezo Abdu Kalenzo baada ya mchezo huo kumalizika. Mchezo ulifanyika Februari 17, 2020 uwanja wa St. Vicent mkoani Tabora.
Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 43 (1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa klabu.
Klabu ya Mgambo FC imepewa Onyo Kali kwa kitendo cha viongozi wao kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (Pre match meeting) katika mchezo uliofanyika Februari 17, 2020 uwanja wa St. Vicent mkoani Tabora.
Adhabu imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14 ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Almasi Jumapili Kasongo,Ofisa Mtendaji Mkuu,Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...