Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu wanne waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya G4S Security kwa tuhuma za wizi wa Sh.1.280,000,000, Dola za Marekani 402,000 na Euro 27,700 huku pia likiwashikilia askari wa polisi tisa kwa tuhuma za kuchukua sehemu ya fedha hizo kutoka kwa mmoja ya watuhumiwa. 

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam , Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amewataja watu wanaoshikiliwa kwa wizi huo ni Chistopher Rugemalila(34)ambaye ni dereva wa G4S mkazi wa Chanika, Mohamedi Ramadhani (40) mlinzi G4S anayeishi Mtoni Kijichi, Ibrahim Maunga Mlinzi G4S na mkazi wa kiluvya pamoja na Salim Shamte(45) Mkazi wa Mbagala kizuiani.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa Februari 7 mwaka huu watuhumiwa watatu ambao ni Christopher Rugemalila, Mohamed Athuman na Ibrahim Maunga wakiwa na gari namba T 728 BAN, Nissan Hard Body mali ya kampuni ya G4S,linalotumika kusindikiza fedha walikabidhiwa fedha kutoka tawi la benki ya NBC Kariakoo na NBC samora ili wazipeleke makao makuu ya benki ya NBC yaliyopo Posta ya Zamani katika Mtaa wa Sokoine Drive lakini hawakufanya hivyo, matokeo yake walipanga njama na kuelekea maeneo ya Temeke Maduka mawili karibu na kituo cha mafuta cha CAMEL.

"Baada ya hapo wakachukua fedha zote na kupakia kwenye gari ndogo T134 DHY Toyota IST ikiendeshwa na Salim Shamte. Watuhumiwa hao baada ya kufanikisha uhalifu huo walitelekeza gari la Kampuni ya G4S, silaha mbili mali ya G4S, moja aina ya pump action, na bastola moja, mashine ya kuhesabia fedha na muhuri wa Benki ya CBA kisha kuondoka kusikojulikana. 

"Jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hizo liliunda kikosi kazi na kuanza ufuatiliaji mara moja, ambapo Februari 17, 2020 mchana huko Mongo la ndege mtuhumiwa wa kwanza aitwaye Christopher Rugemalila alikamatwa na alipopekuliwa alikutwa na Sh. 110,000,000, Dola za Marekani USD 19,000 zikiwa ndani ya gari lake T 691 BMW DSU,"amesema Kamanda Mambosasa.

Ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuhojiwa amekiri kununua magari matano yenye namba za usajili T691DSU BMW yenye thamani ya Sh.15,000,000, gari namba T909DSU Toyota Runx yenye thamani Tsh 13,000,000, gari namba T627DSU Toyota IST yenye thamani ya Tsh 11,000,000, gari namba T653DSU Toyota IST yenye thamani ya Sh.11,000,000 na gari namba T857DSU Toyota IST yenye thamani ya Sh. 11,000,000.

Amesema kuwa mtuhumiwa baada ya kuendelea kuhojiwa alikiri tayari ameshanunua nyumba mbili na kiwanja kimoja vyenye thamani ya Sh.107,000,000, samani za ndani vyenye thamani ya Sh. 5,000,000, na kufanya jumla ya mali na fedha taslimu Sh.297,110,000, dola za Marekani 21,000.

Mambosasa amesema kuwa Febrauri 21 mwaka huu Jeshi la Polisi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Mohamed Ramadhan na Salim Shamte huko maeneo ya Mbagala na walipopekuliwa walikutwa na Sh. 332,000,000, Dola za Marekani 50,000, EURO 5010 na gari moja aina ya IST namba T134 DHY ambayo ndio iliyotumika kubebea fedha baada ya kuiba na kutelekeza gari la kampuni ya G4S. 

Amesema watuhumiwa wote wawili baada ya mahojiano wamekiri kununua viwanja viwanja viwili maeneo ya Kisemvule na Kivule vyenye thamani ya Sh. 25,000,000. Jumla kuu ya mali na fedha taslimu ni walizokutwa nazo watuhumiwa hao wawili ni Sh.357,000,000, dola za Marekani 50,000 na EURO 50,10 3.

" Aidha upelelezi uliendelea na Februari 24, 2020 mtuhumiwa Ibrahim Maunga alikamatwa na baada ya kupekuliwa alikutwa na Sh. 195,213,450,dola za Marekani 70,600, nyumba aliyonunua Kibaha yenye thamani ya Sh.milioni 30 pamoja na samani za ndani zenye thamani ya Sh.milioni 10 na kufanya jumla Jumla kuu ya mali na fedha ni Sh. 253,000,000.Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kukamata watuhumiwa wote watatu pamoja na mtuhumiwa aliyewasaidia kukamilisha wizi huo,"amesema Mambosasa na kuongeza pia wanawashikilia askari Polisi tisa kwa kukiuka maadili ya kazi wakati wa ufutiliaji na upekuzi wa tukio hilo.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...