Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) akijibu maswali ya Wabunge wakati wa Bunge la Kumi na Nane Jijini Dodoma hii leo tarehe 7 Februari, 2020.



Serikali imetenga takribani ekari laki mbili katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwa ni mikakati wa kukuza na kuendeleza shughuli za maendeleo ya vijana.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb) Februari 7, 2020 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Grace Tendega aliyetaka kufahamu juu ya utekelezaji wa Serikali katika kuendeleza shughuli za vijana.

Naibu Waziri Mavunde alieleza kuwa Serikali imetenga maeneo ya shughuli za uzalishaji mali kwa lengo la kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo na itakayo wanufaisha kiuchumi.

“Serikali itaendelea kuzihamasisha Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za Vijana ikiwemo kilimo, viwanda na ufugaji ili kuwapa vijana fursa ya kuyatumia maeneo hayo katika shughuli zitakazowaletea maendeleo,” alisema Mavunde.

Wakati huo huo, Mhe. Mavunde alitoa ufafanuzi kwa Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Simon Msigwa (Mb) ambaye aliuliza kuhusu Mpango wa Serikali katika kutoa mafunzo kwa vijana ambao wamehitimu ili waweze kukidhi soko la ajira?

Alieleza kuwa Serikali Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi inapata ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.

Akifafanua baadhi ya Programu ambazo zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na Mafunzo ya Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo usio rasmi, Mafunzo ya Uanagenzi ambayo yanatolewa kwa njia ya ufundi wa fani mbalimbali na Mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa Teknolojia ya Kitalu Nyumba “Greenhouse”, Mafunzo ya Vitendo Mahali pa Kazi kwa wahitimu n.k.

Aidha alielezea suala la ukosefu wa ajira kwa vijana waliohitimu katika elimu ya juu kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu, “Jitihada za Serikali imekuwa ikiwapeleka vijana hao katika makampuni na viwanda mbalimbali ambapo wanapata mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi 6 hadi 12 na baada ya hapo wanapatiwa cheti cha Utambuzi “Certificate of Recognition”, cheti hiko kinawasaidia vijana hao kuwa wanauzoefu wa kazi Fulani,” alisema Mavunde.

Aliongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwafadhili vijana kwa kuwapatia mafunzo ya Ufundi stadi katika Vyuo vya Veta, Don Bosco na Vyuo shirikishi ili kuwawezesha vijana wanapata ujuzi unaostahili katika soko la ajira.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...