WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili kuwahudumia watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na amesema ameridhishwa na maandalizi.

Aliyasema hayo jana (Jumamosi, Machi 28, 2020) wakati akizungumza na wananchi wilayani Kibaha, Pwani baada ya kukagua hospitali ya wilaya ya Kibaha ambayo imetengwa kwa ajili ya kuwahudumia watu watakaogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabilia na COVID-19, ambapo kwa sasa watu wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandari lazima wapimwe na wakigundulika wanamaambukizi wanawekwa kwenye maeneo maalumu kwa muda wa siku 14.

“Tunazingatia sana wale wanaotoka kwenye nchi ambazo zimeathirika sana wakiingia hapa Tanzania tunawazuia kwanza, tunawapima na tunafuatilia historia yake anatoka wapi na tunaangalia katika siku 14 amepita kwenye nchi zipi.”

Waziri Mkuu alisema wawaweka kwenye maeneo maalumu ili kuweza kuwapima kila siku na kujirishika kama hawana maambukizi kwani mtu anaweza kupimwa leo akaonekana yuko vizuri lakini ana maambukizi ambayo bado hayaonekani kwenye vipimo. Kama katika kipindi cha siku 14 mtu atabainika hana maambukizi anaruhusiwa kwenda kujiunga na familia.

Pia, alisisitiza wananchi waendelee kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko na kwa wale wanaosafiri kwenye usafiri wa umma wasibanane kila mtu akae kwenye kiti.

Waziri Mkuu alisema wananchi wanapokwenda kufuata huduma kwenye masoko wahakikishe wanapeana nafasi baina ya mtu mmoja na mwingine na kabla hawajaingia katika maduka wanawe mikono kwa sabuni na maji tiririka ili kujikinga na maambukizi ya corona.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kuwachukulia hatua watu wote wanaopotosha kuhusu taarifa za ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19). “Aliyetangaza kuwa shule zinafunguliwa tumeshamkamata na atachukuliwa hatua.”

Hivyo aliwataka wananchi wajihadhari na taarifa zinazotolewa na watu ambao si wasemaji rasmi. Alisema taarifa kuhusu virusi vya corona itatolewa na Waziri Mkuu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Msemaji wa Serikali.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua wodi za hospitali ya wilaya ya Kibaha  iliyopo eneo la Lulanzi  ambayo imetengwa  kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Corona Mchi 28, 2020. Kushto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilio. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu )

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...