Charles James, Michuzi TV
MIRADI minne mikubwa ya kimkakati jijini Dodoma ya Stendi ya Mabasi, Soko kubwa la kisasa, Stendi ya Malori na eneo la mapumziko la Chinangali inatarajia kukamilika kabla ya April 26 mwaka huu.

Wananchi mbalimbali wametakiwa kujitokeza kuchukua fomu za kuomba kuwekeza kwenye maeneo hayo kuanzia April 7 mwaka huu katika Ofisi za zamani za iliyokua mamlaka ya ustawishaji wa Dodoma (CDA).

akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi amesema miradi hiyo itakua ya mfano siyo tu hapa nchini bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Kunambi amesema katika kutimiza hayo yote kwa uadilifu wameanzisha Kampuni ya Jiji la Dodoma ambayo itakua na kazi ya kusimamia, kuendesha na kuwekeza miradi hiyo ili kuleta faida kubwa na kuongezea serikali mapato.

" Tumeunda Kampuni hii ambayo ndio watakua wasimamizi wakubwa wa miradi hii, hawa ndio watakua na jukumu la kuwapangishia watu kwa sababu huwezi kumtoa Afisa biashara wa jiji hapa eti akasimamie soko la Job Ndugai hapa tutakua tunajidanganya," Amesema Kunambi.

Akizungumzia masharti ya uwekezaji kwenye maeneo hayo amesema ni lazima mfanyabiashara yoyote alipe kodi ya miezi mitatu ya kwanza lakini pia endapo atashindwa kulipa kodi kwa miezi miwili atakua amevunja masharti ya mkataba na hivyo atasitishiwa kwa kupewa notisi ya mwezi mmoja.

Amewataka wananchi wa Dodoma na sehemu nyingine kujitokeza kuwahi fursa za uwekezaji kwenye maeneo hayo huku akitanabaisha kuwa wamezingatia suala la unafuu wa kodi.

" Ziko fursa nyingi sana kwenye miradi yetu hii minne ambayo kwa hakika tuna kila sababu ya kumshukuru sana Rais Dk John Magufuli kwa kuamua kuileta miradi hii ndani ya Jiji letu la Dodoma.

Wananchi wajitokeze kuwekeza hii miradi ni yao na Jiji la Dodoma linathamini wawekezaji na tumeeka mazingira mazuri sana kwao lengo letu ni kuhakikisha kwamba hakuna mwekezaji ambaye atashindwa kufanya biashara zake Dodoma kwa sababu ya mazingira, " Amesema Kunambi.

Amezitaja fursa za biashara zilizopo kwenye miradi hiyo kuwa ni pamoja na eneo la kukata tiketi kwenye stendi, vibanda vya machinga, maduka makubwa kama ilivyo Mlimani City jijini Dar es Salaam, eneo la vifaa vya nyumbani, biashara ya chakula, bidhaa za mifugo na Kilimo, bidhaa za kielektroniki na huduma za kifedha, huku pia wakianza maandalizi ya kujenga maeneo ya mama lishe.

Kuhusu eneo la mapumziko la Chinangali, Kunambi amesema kutakua na viwanja vya michezo mbalimbali kama Tenisi, mpira wa wavu, eneo la kuogelea, mpira wa kikapu pamoja na michezo ya watoto.

" Miradi hii inakamilika baada ya kuchukua miezi 15 na imegharimu Sh Bilioni 89 na fedha zingine zilipelekwa kwenye miradi ya miundombinu ambapo tumetengeneza taa za barabarani kwenye barabara za km 27 ambazo zimetumiwa takribani Sh Bilioni 19.

Mradi wa stendi ya Mabas umetumia Sh bilioni 24, mradi wa soko la Job Ndugai umetumia Sh bilioni 14 na eneo la mapumziko limetumia bilioni 1.9," Amesema Kunambi.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake leo jijini Dodoma kuhusiana na tarehe ya kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya Jiji hilo na jinsi wawekezaji wataweza kupata fursa ya kuwekeza kwenye miradi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...