WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ni vema viongozi wa vyama vya siasa nchini wakaonesha mfano wa kuendesha siasa za kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha watanzania na siyo kuwatenganisha.

“Hivyo basi, tudumishe utulivu, amani, mshikamano pamoja na ustaarabu wetu wa Kitanzania katika kipindi chote cha kampeni na Uchaguzi Mkuu ili kulifanya Taifa letu kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma.

Pia, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania washiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Nchi. “Hakuna kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha mifarakano.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili linatarajiwa kuanza Aprili 5, 2020 na kukamilika Juni 26 2020. “Zoezi hili litaenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wapiga kura katika daftari hilo. Natoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili waweze kutumia haki yao ya Kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka.”

Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2020 nchini.

Amesema pamoja na mambo mengine, maandalizi hayo yanahusisha Zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika nchi nzima. Awamu ya kwanzailizinduliwa tarehe 18 Julai, 2019 Mkoani Kilimanjaro na kukamilika tarehe 23 Februari, 2020 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

“Uboreshaji wa daftari hili ulihusisha uandikishaji wa wapiga kura wapya ambao wametimiza umri wa miaka 18 au watatimiza umri huo ifikapo siku ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; urekebishaji wa taarifa za wapiga kura walioandikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ufutaji wa taarifa za Wapiga Kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”

Amesema katika zoezi hilo, jumla ya wapiga kura 10,285,732 wameandikishwa na kati yao, wapiga kura wapya ni 7,043,247, walioboreshewa taarifa zao ni 3,225,778 na wapiga kura waliofutwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutokana na kupoteza sifa ni 16,707.

Wakati huo huo, Wazirti Mkuuamesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba liidhinishe jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...