Mkuu wa Kitengo cha Mfumo wa Taarifa za Kijiografia wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Benedict Mugambi akimueleza Mtakwimu Mkuu wa Serikali namna kazi ya utengaji maeneo kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi inavyoendelea wilayani Chemba. Kulia ni Mrasimu Ramani Martha Macha na Mtakwimu Mkuu Seif Kuchengo. 
 Mkuu wa Wilaya ya Chemba Simon Odunga akizungumza na ujumbe kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliyoongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa wakati ulipokuwa wilayani humo kukagua maandalizi ya Sensa ya Watu na Mkazi ya Mwaka 2022.
 Mkuu wa Wilaya ya Chemba Simon Odunga akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Timu ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliyoongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa wakati alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo kukagua utengaji wa maeneo ya kuhesabia kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akizungumza katika Ofisi ya Kijiji cha Chemba wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua ubora wa kazi za maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kushoto ni Mtendaji wa Kijiji cha Chemba Bibi Sauda Said Majala na kuli ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Shule Bw. Omar Ramadhani Rashid.
 Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa (nyuma mwenye kilemba) akiwa ameongozana wa viongozi wa Kijiji cha Chemba pamoja na wataalamu wa kutenga maeneo ya kuhesabia watu wakati wa ziara yale ya kukagua kazi ya utengaji maeneo katika wilaya ya Chemba Ijumaa tarehe 22 Mei, 2020. 
Mrasimu Ramani Martha Macha akimuonesha kitu Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa wakati wa kuhakiki kazi ya utengaji wa maeneo ya kuhesabia watu ikiwa ni maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 huko wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
MKUU wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma Simon Odunga amepongeza kazi nzuri ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu inayofanywa na wataalamu wa Mifumo ya Taarifa ya Kijiografia (GIS) kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS).
Mkuu wa Wilaya huyo alitoa pongezi hizo ofisini kwake hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na wataalamu hao wakiongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa ambao walimtembelea.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali alikuwa katika ziara ya siku moja wilayani Chemba kukagua ubora wa kazi ya utengaji maeneo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanya mwaka 2022.
Bwana Odunga amesema kwa kuwa tekinolojia inayotumiwa sasa katika kutenga maeneo inawezesha kuchukua taarifa nyingi ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za afya, maji, elimu na ofisi mbali mbali za serikali tangu ngazi ya kijiji hadi wilaya, taarifa hizo zitaisaidia sana wilaya katika kupanga mipango ya maendeleo katika ngazi mbalimbali.
“Nimefurahishwa na kazi yenu ambayo mbali ya kutenga maeneo lakini taarifa mnazokusanya zitausaidia uongozi wa wilaya yetu kuielewa vyema wilaya hivyo zitatusaidia kujipanga vyema na kwa weledi katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na masuala mengine ya kimaendeleo” alisema Bwana Odunga.
Alisifu utendaji bora wa timu hiyo na namna ilivyoweza kuyafikia hadi sasa maeneo mengi katika wilaya hiyo pamoja na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo wilayani humo huku nchi ikiwa katika kipindi cha mapambano dhidi ya mlipuko wa virusi hatari vya Corona.
“Wilaya yetu bado ni mpya; tuna changamoto nyingi hasa upande wa miundombinu ya barabara lakini mnafanya kazi kwa umahiri mkubwa na kuweza kufika kila kitongoji, kijiji, kata na tarafa” alibainisha na kuongeza kuwa wilaya hiyo ina vijiji 114, kata 26, tarafa 4 na vitongoji 498.
Bwana Odunga alisisitiza umuhimu wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa kubainisha kuwa takwimu zitakazokusanywa katika Sensa hiyo zitaiwezesha Serikali kufanya mapitio ya Dira ya Maenddeleo 2025 ambapo lengo lake ni kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kipato cha na pia msisitizo wa utekelezaji wa mpango wa taifawa kujenga uchumi wa viwanda.
Kwa upande wa wilayani kwake alieleza kuwa wakati wote wanawasisitizia viongozi katika ngazi zote umuhimu wa matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi yanayohusu maendeleao ya wananchi.
“Kiongoni mathalan wa kijiji ambaye haelewi mipaka ya kijiji anachokiongoza kiutawala, haelewi kuna kaya ngapi, hajui idadi ya wanawake na wanaume, hajui idadi ya vijana itakuwa vigumu uongozi wake kutoa matokeo bora” Alisisitiza.
Wakati huo huo Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa alimueleza Mkuu wa Wilaya huyo kuwa ziara yake Wilayani humo ni kukagua ubora wa kazi inayofanyika ya kutenga maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
Alieleza kuwa sehemu kubwa ya kazi hiyo katika wilaya ya Chemba imekamilika isipokuwa sehemu ndogo tu ambayo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
“Leo tutapitia baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa kazi katika kijiji cha Chemba hapa kitongoji cha Shuleni ili kuyahakiki na tutakapokamilisha kazi hivi karibuni tutakukabidhi taarifa ili viongozi wa wilaya nanyi mjiandae tayari kwa Sensa” alieleza.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali alieleza kuwa kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu itafanyika hatua kwa hatua katika wilaya zote 139 na halmashauri zote 185 nchini ili kuhakikisha Sensa inafanyika katika kiwango cha ubora unaokubalika.
Alibainisha kuwa lengo kuu ni kuhakikisha watu wote wanahesabiwa na kunakuwepo na takwimu tangu ngazi ya kaya hadi ngazi za juu ambazo zitasaidia Serikali na wananchi kwa pamoja kupanga mpango ya Maendeleo.
Naye mkuu wa kitengo cha Mfumo wa Taarifa za Kijiografia Benedict Mugambi alieleza kuwa kazi ya kutenga maeneo katika mkoa wa Dodoma imekamilika katika Wilaya za Chamwino, Bahi na Kondoa ambapo watakapokamilisha sehemu ndogo ya kazi iliyobaki wilaya ya Chemba wataalamu hao watakwenda wilaya nyingine zilizobaki mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...