Mkuu wa Usalama Barabarani Nchini, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania (SAPC) Fortunatus Musilim (kushoto) akiwa katika eneo lilotokea ajali ya basi la Prezdar na kuua watu 10 kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi akiambatana na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa, Yusuph Kamota.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa, Yusuph Kamota akizungumza na wanahabari katika eneo lilotokea ajali ya basi la Prezdar juni 27 mwaka huu katika mlima Kitonga.
………………………………………………………………………….


NA DENIS MLOWE,IRINGA 

JESHI la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani Tanzania limebainisha chanzo cha ajali iliyoua watu 10 iliyohusisha kampuni ya Mabasi ya Prezdar inayofanya safari zake kati ya mkoa wa Iringa na Dar es salaam iliyotokea June 27 mwaka huu katika Mlima Kitonga Mkoani Iringa. 

Akizungumza na Waandishi wa habari katika eneo la Tukio Mkuu wa Usalama Barabarani Nchini, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania (SAPC) Fortunatus Musilim alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa aliamua kurudi katika eneo la ajali kwa mara ya pili kujiridhisha kutokana na yale ambayo aliweza kuyapata kutoka kwa baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo na kubaini mambo mbalimbali kuhusu ajali hiyo. 

Alisema kuwa hakuna ubishi kwamba basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi kutokana na mazingira ambayo yanaonyesha ikiwemo kukata miti iliyokuwa kama kinga kwa basi hilo na mawe na madhara yaliyotokana na ajali hiyo . 

Alisema kuwa zaidi ya hapo wa wamebaini kwamba licha ya mwendo kasi na kuweza kupita kona zaidi ya 37 za mlima Kitonga, wamebaini kuwa gari hilo lilikuwa bovu kabla halijaanza safari kutokana na mifumo yake kutokuwa salama baada ya kuchukuliwa Yadi baada ya kuonekana siku ya tukio kulikuwa na abiria wengi. 

Alisema kuwa chanzo kingine walilochobaini katika ajali hiyo ni Dereva aliyesababisha ajali hiyo hakuwa mzoefu na njia hiyo huku ikisemekana alikuwa anaendesha njia nyingine ya Iringa Dodoma kupitia Mtera hivyo kwa dereva ambaye sio mzoefu wa barabara ya Iringa Dar es Salaam Kupitia Morogoro ni tatizo kwake na hii ni kutokana na Dereva wa basi hilo kukataa kuendesha basi hilo lililokuwa bovu na kutoa taarifa kwa mmiliki wake. 

“Na hili wamelisema wale majeruhi kwani ilifikia mahala walimwambia dereva punguza spidi na hata wakati mwingine walikuwa wanasaidiana kuingiza gia kwenye lile gari kwamba isiwe nzito isiweze kutembea kutokana na dereva kutokuwa mzoefu wa kuendesha gari hilo na hitilafu zilizokuwepo kwenye gari hilo” alisema .

Aliongeza kuwa kabla ya ajali hiyo Wakala wa Kampuni hiyo alimpigia simu Mmiliki wa Gari hilo na kumwambia kuna abiria wengi katika stend ya mabasi ya igumbilo hivyo kwa tamaa ya kutaka faida bila kufanya ukaguzi wa gari hilo, waliamua kupakilia nje ya stendi hali iliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo. 

Aidha SAPC Musilim alisema kuwa licha ya mmiliki huyo kupigiwa simu na mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Iringa kutoa ushirikiano lakini hataki kutoa ushirikiano hivyo kumtaka Mmiliki wa gari hilo aliyejulikana kwa jina la Nedji Msuya Mkazi wa Dar es salaam kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kufanikisha kumpata dereva aliyesababisha ajali hiyo na yeye mwenyewe kufika katika kituo chochote cha polisi au kufika ofisi za Trafiki makao makuu. 

Kamishna Muslim amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya usalama wa barabarani sura ya 168 kifungu cha 36 kidogo cha tano, imesema kuwa ajali inapotokea na kubaini chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa gari, basi mmiliki wa gari atashitakiwa sambamba na Dereva wa Gari. 

Aliongeza kuwa Dereva wa Gari hilo Said Abas Said anatakiwa kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi ili waweze kuchukua maelezo kuhusu ajali hiyo na kushtakiwa kuendesha gari bovu barabarani. 

Alisema kuwa kutokana na ajali hiyo moja kwa moja jeshi la Polisi limeisimamisha leseni ya dereva huyo kwa muda wa miezi sita na kuongeza kuwa baada ya dereva huyo kumaliza adhabu yake watampa mtihani wa masuala ya udereva wa kujihami, sheria na usalama barabarani kabla ya kumpa leseni mpya. 

Aidha amewataka madereva kafuata sheria za usalama barabarani huku jeshi hilo likiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wote watakaovunja sheria za na kuongeza kuwa wamiliki wa magari ya abiria wanatakiwa kuacha kupeleka magari ambayo ni mabovu ili kuepukana na ajali za barabarani. 

Naye Mkuu wa Kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Iringa Yusuph Kamota amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani hasa wanapokuwa katika katika mkoa wa Iringa kwani kuna milima ambayo ni hatarishi ikiwemo Mlima Kitonga na Mlima Nyang’oro ambayo bila kuwa na uzoefu husababisha ajali. 

Kamota aliongeza wamiliki wa Magari waache utaratibu wa kuwapatia madereva wasiokuwa wazoefu wa kutumia barabara hizo na ikiwezekana waombe msaada kwa jeshi hilo hasa wanaokuwa barabarani kujua ni namna gani ya kuweza kupita katika milima hiyo. 

Hata hivyo alitoa onyo kali kwa madereva mkoani hapa wasiotaka kufuata sheria za usalama barabarani ni bora wakafanya shughuli nyingine ikiwemo kilimo kwani kwa mkoa huu hawatakuwa salama pindi wakivunja sheria za usalama barabarani. 

Katika ajali hiyo ambayo ilitokea june 27 mwaka huu katika Mlima Kitonga imeua watu 10 na kati ya hao Miili ya marehemu watano imechukuliwa na ndugu zao huku majeruhi wa ajali hiyo wakiendelea vizuri na wengine wakiruhusiwa baada ya hali zao za kiafya kuimarika

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...