Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Fomu zake alizopata wadhamini mara baada ya kuzikabidhi kwa Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally Kakurwa katika Ukumbi wa NEC makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ndani ya ukumbi wa NEC wa Chama cha Mapinduzi mara baada ya kurudisha Fomu zake.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wanachama mbalimbali wa CCM waliokusanyika nje ya Ofisi za Makao Makuu ya CCM White House jijini Dodoma mara baada ya kurudisha Fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi CCM.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Sekretariet ya Chama cha Mapinduzi mara baada ya kuzungumza katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na wanachama wa CCM mara baada ya kuzungumza nao katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama White House jijini Dodoma. PICHA NA IKULU.


NDG. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, MWENYEKITI WA CCM NA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AREJESHA FOMU ZA KUOMBA KUTEULIWA KUGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO KWA TIKETI YA CCM
_______________

Makao Makuu ya CCM, Dodoma
30 Juni 2020

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku ya leo amerejesha fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kugombea dhamana ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba, Mwaka 2020.

Ndg. Magufuli amerejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM katika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 1977, Toleo la 2017. Sambamba na fomu hizo, Ndg. Magufuli amepokea fomu za wadhamini ambazo zimewasilishwa kwake na Wenyeviti wa CCM kutoka mikoa yote 32 ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na yeye kuzikabidhi kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Bashiru Ally Kakurwa.

Katika tukio hilo la kurejesha fomu, Mamia ya wana CCM wakiwemo, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Wenyeviti wa Mikoa wa CCM, Wajumbe wa Kamati Kuu, Viongozi watendaji wa CCM Taifa, Wabunge na Madiwani wa CCM, wamejitokeza katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma na wameongozwa na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Mzee Philip Japhet Mangula.

Akizungumza na umma wa wanachama wa CCM waliojitokeza katika Makao Makuu ya CCM, Ndg. John Pombe Magufuli amewashukuru wana CCM na Watanzania kwa kuwa pamoja naye katika safari ya miaka mitano na kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ambayo tumeyapata kama Taifa katika kipindi hiki cha Miaka Mitano.
Ndg. Magufuli amesisitiza Tanzania ni nchi tajiri na kwa pamoja tunaweza ikiwemo kama tulivyoishinda korona kwasababu Mungu wetu ni mwaminifu na anatupenda na kuipenda nchi yetu ya Tanzania.

Wakati uo huo Ndg. Magufuli ametangaza kuwa tarehe 1 Julai 2020 wana CCM wote waanze kupita katika maeneo yao na Ofisi za Chama ili kujitambulisha na kuomba kupata utaratibu wa mchakato wa Uchaguzi na ametoa angalizo kuwa wote watakaoshiriki katika uchaguzi wafanye kampeni za kistaarabu, walinde maslahi ya Chama cha Mapinduzi na wasitumie muda huu kuchafuana kitu ambacho kitabomoa na kukidhoofisha chama chetu.

Ndg. Magufuli amesisitiza kuwa wagombea wa Urais Zanzibar wasiumizane, kamwe wasivunje umoja, wavumiliane, wapendane na waheshimiane pia. Halkadharika Ndg. Magufuli ametoa rai kwa vyama vingine vya siasa wasiwasahau wanawake na vijana katika kuwapa nafasi za uongozi katika uchaguzi huu.

Kwa umahususi Ndg. Magufuli ameelezea Mipango ambayo tayari iko katika utekelezaji ikiwemo umaliziaji wa barabara ya Tabora – Mpanda mpaka Wilaya ya Tanganyika kwenye bandari ya Kalema ambapo Serikali ya CCM inapanga kununua meli kubwa ambayo itafanya safari zake kati ya bandari ya Kalema na Kalemii katika Nchi ya Kidemokrasi ya Kongo ambapo ni ukanda wenye idadi kubwa ya watu na biashara kubwa ikiwamo madini ya dhahabu ambayo yatachochea ukuaji wa uchumi katika nchi yetu tofauti na sasa ambapo malori ya mizigo yanalazimika kwenye mwendo mrefu kupitia nchi jirani za Zambia.

Ndg. Magufuli ameelezea kazi inayoendelea ya kulijenga Jiji la Dodoma ambapo takribani Bilioni 660 ziko tayari kwa ujenzi wa barabara kubwa za lami kuuzunguka Mji wa Dodoma na saizi mchakato wa tenda unaendelea.

Akifafanua kuhusu maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja Mkubwa wa Kimataifa wa Msalato Dodoma, Ndg. Magufuli amesema tayari shilingi Bilioni 500 zimeshatengwa na kinachosubiriwa ni ujenzi kuanza hivi karibuni.

Aidha Ndg. Magufuli ameelezea mafanikio katika sekta ya nishati ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka mitano ambayo ni kuongezeka kwa idadi ya vijiji vyenye umeme kutoka 2018 hadi vijiji 9,112 na kwamba ifikapo mapema mwaka kesho vijiji vyote 12000 vitakuwa na umeme. Usambazaji wa umeme unakwenda sambasamba na ujenzi wa Bwawa la Mwl. Julius Nyerere la kufua umeme kwa maporomoko ya maji na litakalozalisha zaidi ya Megawati 2115. Ujenzi wa Bwawa la Mwl. Julius Nyerere limepelekea fursa ya kuanzisha Mbuga kubwa kabisa ya wanyama ya Mwl. Nyerere (Mwalimu Nyerere National Park).

Ndg. Magufuli ameelezea kazi kubwa ambayo imefanyika katika kuhakikisha upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya kilimo kwa wakulima na mifugo kwa wafugaji kwa kupunguza maeneo ya hifadhi na kuongeza maeneo ya vijijini kote nchini.

Ndg. Magufuli ameelezea kazi nzuri ambayo imefanyika ya kufanyia maboresho makubwa reli ya Kati ikiwemo kuhakikisha usafiri ya treni unarejeshwa katika tawi la Kaskazini kwa Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Tulisema hapana kwa kero zilizokuwa zikiwakabili mama lishe na wamachinga na zimefanyiwa kazi, kutatuliwa na kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao kwa uhuru na bila kubughudhiwa amesisitiza Ndg. Magufuli

Ndg. Magufuli ameelezea ongezeko kubwa la Mikopo ya Elimu ya Juu ambao mpaka sasa zaidi ya Bilioni 467 zimetengwa na wanafunzi wanaipata mikopo hiyo kwa wakati. Mikopo ya Elimu ya Juu imekwenda sambasamba na utolewaji wa elimu bila malipo kutoka Shule za Msingi, Mpaka Sekondari ambayo imegharimu Taifa zaidi ya shilingi Trilioni Moja.

Katika sekta ya madini Ndg. Magufuli ameelezea mafanikio makubwa ikiwamo madini ya vito, Tanzanite ambapo uchimbaji umeongezeka maradufu mpaka kupatikana kwa Mawe makubwa mawili ya Tanzanite kuwahi kupatikana katika historia ya uchimbaji madini hayo ikiwa ni baada ya kujenga uzio kuzunguka eneo la machimbo.

Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania ametumia muda wake leo pia kuelezea mageuzi makubwa ambayo yamefanyika katika sekta ya usafiri wa anga ikiwamo kununua mitambo ya kisasa ya kuongozea ndege (rada), ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege sambamba na ununuzi wa ndege 11 kubwa za masafa ya kimataifa, za masafa ya kati na ndege za masafa ya ndani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ndg. Magufuli ameeleza Tanzania imeendelea kufanya vizuri kiuchumi ambapo katika Bara la Afrika Tanzania ni miongoni wa nchi tano zenye uchumi imara na ni miongoni wa nchi 10 ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Mipango yote hii imetekelezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na inaendeleza maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni kwa msingi nimeona na kwa unyenyekevu niombe tena dhamana kwa chama changu cha Mapinduzi (CCM) ili kazi hii nzuri tushirikiane kuikamilisha na kuiongeza maradufu. Tunataka kila mtanzania afaidike na matunda ya nchi yetu Amesema Ndg. Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...