MKUU wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga amepokea vifaa kinga vya magonjwa ya mlipuko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Dodoma kutoka kwa Jumuiya ya Watanzania waishio Marekani (ATC) vyenye thamani ya Sh Milioni Saba.

Jumuiya hiyo pia imekabidhi pia na vifaa kinga vya kupambana na ugonjwa wa Covid19 ambavyo ni Glovu za Upasuaji boksi 30, Vitakasa Mikono Lita Tano, Sabuni ya Mikono chupa 160 za Lita tano ambapo vifaa vyote hivyo vimenunuliwa nchini.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga amewashukuru watanzania hao kwa moyo wa kizalendo waliouonesha huku akimpongeza Diwani wa Kata ya Buigiri wilayani humo, Kenneth Yindi kwa kusaidia kupatikana kwa msaada huo.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli itaendelea kuhudumia watanzania kwa nguvu zote kwa kujali pia Afya zao na ndio maana idadi kubwa ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati zimejengwa kwenye awamu hii ya tano lengo likiwa ni kuhudumia wananchi.

" Niwapongeze sana kwa moyo wenu wa kizalendo pamoja na kwamba mpo nje ya Nchi lakini mmeguswa mkaona mlete msaada wenu hapa, tunawahakikishia utawafikia walengwa wote ambao ni wananchi na watanzania wenzenu," Amesema DC Vumilia.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi ambaye amechangia kupatikana kwa vifaa hivyo ameishukuru Jumuiya hiyo kwa kuwezesha kupatikana kwa vifaa hivyo ambavyo vitasaidia watanzania wanyonge katika mapambano dhidi ya Corona.

Amesema msaada huo walioutoa unaonesha ni jinsi gani watanzania wote walivyo kitu kimoja na namna gani wameguswa na namna ambavyo Rais Magufuli amewaongoza watanzania katika kujikinga na maambukizi ya Corona.

" Hakika huu ni uzalendo mkubwa, licha ya kwamba mko mbali lakini mmeguswa kumuunga mkono Rais wetu na watanzania kwa ujumla, tunaomba msichoke kutoa na siyo tu Chamwino sehemu yoyote ya Nchi yetu kwa sababu watanzania sisi ni wamoja," Amesema Yindi.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya ATC, Kepteni Amos Lwiza amesema Jumuiya hiyo iliyochangia inaundwa na watanzania wanaoishi Majimbo ya Washington DC, Maryland na Virginia na sababu kubwa iliyofanya wachangie ni kutokana na juhudi kubwa zinazooneshwa na serikali katika kuwatumikia watanzania.

" Pamoja na kwamba sisi tuko mbali, changamoto zilizopo Tanzania zinatugusa moja kwa moja kwa sababu wazazi wetu, watoto na ndugu zetu wako hapa, tuliposikia Covid19 imeingia tukaona na sisi tuna wajibu wa kuchangia kwa hali na mali," Amesema Kepteni Lwiza kwa niaba ya ATC.
 Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Dodoma, Vumilia Nyamoga akipokea msaada wa vifaa vya kujikinga na magonjwa mlipuko kutoka kwa Jumuiya ya Watanzania waishio Marekani.
 Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga akizungumza baada ya kupokea vifaa vya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kutoka kwa Jumuiya ya Watanzania waishio Marekani. Kulia ni Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi.
 Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi ambaye amesaidia kupatikana kwa vifaa vya kujikinga na magonjwa mlipuko kwenye Wilaya ya Chamwino akizungumza mbele ya DC Vumilia Nyamoga.
 Mwakilishi wa Jumuiya ya Watanzania waishio Marekani, Kepteni Amos Lwiza akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya kujikinga na magonjwa mlipuko vilivyotolewa na Jumuiya hiyo kwa Wilaya ya Chamwino.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...