Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea taarifa ya mradi ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma, kutoka kwa  Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Rashid Mchata, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali inatoa fedha kuigharamia, alipokuwa ziarani mkoani humo.
Fundi Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhandisi Solomon Tile, akitoa maelezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (katikati), wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Bw. Kanali Michael Ngayalina. 

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kukagua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, alipotembelea na kukagua ujenzi wa  Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akifafanua jambo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipotembelea na kukagua ujenzi wa  Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mkoa wa Kigoma.
Meneja Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Bw. Masawika Kachenje, akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) na wapili kushoto ni  Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina, alipotembelea ujenzi wa mradi wa ofisi hiyo. Mkoani Kigoma.Picha na Josephine Majura – KIGOMA)
……………………………………………………………………………………


Na: Josephine Majura na Peter Haule KIGOMA

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango (Mb), ameupongeza uongozi wa mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Buhigwe kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe inayojengwa katika eneo la Bwega, Tarafa ya Manyovu, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma na kuagiza Jengo hilo likamilike kabla ya mwezi wa kumi ili wananchi wa wilaya hiyo waanze kupata huduma kwenye jengo hilo jipya.

Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo jipya la Ofisi ya MKuu wa Wilaya mpya ya Buhigwe ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi bilioni 1.1

“Nakupongeza Mkuu wa Wilaya na timu yako yote kwa usimamizi mzuri wa Fedha za Serikali, lazima tujenge Makao Makuu ya Wilaya ambayo yataishi kwa miaka mingi, kwa hiyo nimefurahi jengo ninavyoliona hata kama sio Mhandisi lakini ninaona lina ubora”. alisisitiza Dkt. Mpango.

Alimtaka Mkuu wa Wilaya kuendelea kusimamia rasilimali fedha zinazotolewa na Serikali kama alivyofanya kwenye mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili thamani ya fedha za miradi inayotekelezwa ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa.

Kwa upande wake, Meneja mradi huo Masawika Kachenje, akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe amesema kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni mia tano (500,000,000) ambazo Serikali zilitoa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo kimetumika kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi.

Aliongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni (550,000,000), kimebaki ili kukamilisha kiasi cha sh. Bilioni 1.1 ikiwa ni gharama ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi jengo zima, ambapo mipango ya Wilaya ilikuwa kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Julai tarehe 15 mwaka 2020.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali, Michaeli Ngayalina, amemshukuru Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, kwa kutembelea na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa Fedha za Serikali na kuahidi kuzisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na Serikali kukamilisha miradi ya maendeleo.

Kanali Ngayalina, amemuomba Dkt. Mpango kusaidia upatikanaji wa Fedha zilizobaki ili waweze kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo kama ilivyopangwa kwenye ratiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...