Na Said Mwishehe,Michuzi TV

KWA mashabiki wa soka katika mataifa mbalimbali duniani wakiwemo wa Taifa la Tanzania wanafahamu uwezo wa Mshambuliaji nyota wa Kikosi cha Barcelona Lionel Mess pamoja na uwezo alionao mshambuliaji wa timu ya Juventus Christiano Ronaldo.

Umahiri wa wachezaji hao katika mchezo wa mpira wa miguu a.k.a Soka umewafanya kuwa gumzo kila siku iendayo kwa Mungu.Sababu ni moja tu washambuliaji hao ambao mpaka sasa mashabiki wa soka wanashikwa kigugumizi kutambua nani zaidi ya mwingine.

Swali la nani zaidi kati ya Christiano Ronaldo na Lionel Mess limekuwa gumu kujibika.Hivyo jibu rahisi wote bora wawapo kwenye timu zao.Kila mmoja kwa nafasi yake wanatambua majukumu waliyonayo kwenye timu zao, wanajua namna ambavyo mashabiki wanawategemea na hasa linapokuja suala la ushindi. Wakiwa kwenye timu zao za taifa wachezaji hao wanabeba dhamana ya kuhakikisha wanawakilisha vema nchi zao.

Kwa kifupi Christiano Ronaldo na Lionel Mess wanajua nini ambacho mashabiki wa soka waliopo kwenye vilabu vyao, waliopo kwenye timu za taifa na walioko ulimwenguni kote wanataka kutoka kwao.

Nimeanza na kuwazungumzia Mess na Ronaldo nikiwa na maana ya kutoa mfano rahisi wa kuzungumzia utendaji kazi wa Rais Dk.John Magufuli. Rais Magufuli namna anavyosimamia vema majukumu yake ingekuwa tunazungumzia katika ulimwengu wa soka basi uwezo ni zaidi ya Ronaldo na Mess.Ndio na Watanzania wanafahamu uwezo mkubwa wa utendaji kazi wake.

Uwezo wa Rais Magufuli umeifanya Tanzania kwenda kasi katika kuleta maendeleo.Miradi ya maendeleo mbalimbali imetekelezwa na mingine iko katika hatua za umaliziwaji.Macho ya Watanzania yanashuhudia ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea.

Kasi ya ujenzi wa reli hiyo unaridhisha.Chini ya usimamizi wake na maelekezo yake kuhusu reli hiyo hatimaye tunashuhudia reli zikiendelea kutandikwa na baadhi ya vipande inapitika kwa majaribio.

Huko tulikotokea treni za kisasa za mwendo kasi tena zinazotumia umeme tulikuwa tunaona kwenye televisheni lakini chini ya uongozi wa Rais Magufuli na kwetu mambo yamekuwa bam bam.

Yaani reli hiyo kwa waliokuwa jijini Dar es Salaam eti inapita  Kariakoo, Buguruni, Vingunguti, Kipawa, majumbasita, Ukonga ,Pugu na kisha inaelekea mkoani Pwani,Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma. Inajengwa kwa fedha zetu wenyewe.Piga kelele kwa Magufuli akeeeeeee!

Achilia mbali kwenye ujenzi wa reli ya kisasa, nenda katika nishati ya umeme nako maajabu yanaendelea. Umeme unaendelea kusambazwa vijijini.Wizara ya Nishati kupitia Tanesco umeme unaendelea kusambaa.Hata kijijini kwako umeshafika.Yote hiyo ni kazi ya Rais Magufuli.Kama hiyo haitoshi ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere kazi inaendelea tena kwa kasi.

Wakati akiomba kura katika uchaguzi mkuu ,Dk.Magufuli moja ya mambo aliyoyazungumza na kuahidi kutafuta ufumbuzi wake na eneo la nishati ya umeme. Alisema lazima tuwe na umeme wa kutosha na usio katika.Ndani ya miaka mitano ya uongozi wake hilo limefanikiwa.

Kwa spidi hii ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ingekuwa tunazungumzia kwenye soka basi ingekuwa ni kasi kama ya Mess au Ronaldo pindi wanapokuwa wakitafuta ushindi na hatimaye kuwa na alama tatu muhimu.

Hakika Rais Magufuli spidi yake ya kuleta maendeleo ni kubwa mnoo. Ni spidi haswaaa.Ukitaka kujiridhisha na spidi yake kaangalie katika sekta ya Vituo vya afya, Zahanati na hospitali zimejengwa kila wilaya.Rais ameifanya Tanzania kuwa ya kuogopwa katika suala la maendeleo.

Tanzania ya sasa sio ile ya zamani.Ndio kwani wote si tunaona jamani ambayo yamefanyika, Kila Mkoa ukienda hata muda huu utakuta kuna mradi mkubwa wa maendeleo unatekelezwa.Nenda Sumbawanga leo hii utadhani uko Ulaya.Chezea Magufuli wewe.Swali la nani kama Magufuli? Jibu tegemea tu hakunaa.Magufuli atabaki kuwa Magufuli.

Ukitaka kujua yaliyomo kwenye nchi yetu kama unashindwa kuyaona kwa macho basi tega sikio uhadithiwe.Yanayofanyika nchini kwetu kwenye upande wa maendeleo yanazungunzwa kila mahali.Ukishindwa kabisa kusikiliza yanayosemwa kuhusu maendeleo makubwa ya nchi yetu nikuombe tu msikilize msanii wa Bongo Fleva kutoka lebo ya WCB ,anaitwa  Zuchu.

Mwanadada huyo kuna wimbo wake ambao amefafanua vizuri tu kuhusu maendeleo yaliyofanywa na Rais Magufuli. Katika wimbo huo pamoja na mistari yote kwangu napenda pale anaposema Tanzania ya sasa ...owiiii mama...Tanzania ya Magufuli. Kazi kubwa na nzuri inaonekana tena kwa macho.

Kinachofurahisha zaidi kuna miradi mingi mikubwa imefanyika ndani ya miaka mitano tu yaani kuanzia mwaka 2015 hadi 2020.Tunafahamu katika mchezo wa soka dakika 90 ndio hutumika uwanjani kwa mujibu wa kanuni na sheria zinazotumika kuuchezesha.

Lakini sheria hiyo ya soka inataka katika hizo dakika 90 kuwe na mapumziko ya dakika 45 kwa kila kipindi.Hivyo kipindi cha kwanza cha mchezo dakika 45 na kipindi cha pili cha mchezo nacho dakika 45.Ni kama vile tu tunavyoangalia akina Mess na Ronaldo wawapo kwenye 'game' .

Kwa Rais Magufuli kwa sasa amemaliza kipindi chake cha kwanza cha kuiongoza Tanzania.Ingekuwa kwenye soka tunasema amemaliza dakika 45 za kwanza na anajiandaa kurejea kumalizia dakika 45 za pili.

Kwa jinsi ambavyo ameonesha umahiri mkubwa wa kulitumikia Taifa la Watanzania,ni jukumu letu sote kuhakikisha anarudi kumalizia kipindi chake cha pili cha miaka mitano.

 Najua Rais Magufuli kwa aliyoyafanya katika nchi yetu imemfanya awe kwenye mioyo yetu. Tunampenda kama ambavyo yeye amekuwa akitupenda kwa dhati.Nakumbuka wakati ule anaomba kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ,alikuwa akisisitiza umoja na mshikamano miongoni mwetu.Hakika amesimamia hilo kwa zaidi ya asilimia 100.

Chini ya Rais Magufuli wananchi wanyonge sasa kauli zao zinasikika. Kwa Rais Magufuli anaposikia wanyonge wananyanyasika anaumizwa sana na hataki kuona hilo linatokea.

Ni jambo la kawaida kwa Rais Magufuli anaposikia au kuona kuna mnyonge ameonewa mahali akahakikisha haki ya mnyonge huyo inapatikana.Kupitia Rais Magufuli wanyonge wengi wamepata haki.

Utawala wa Rais Magufuli ambao ameuonesha kwa miaka mitano ya awamu ya kwanza ya uongozi wake kumbe Watanzania tunaweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo bila kutegemea fedha za wafadhili ambazo zimejaa masharti lukuki.

Nakumbuka Rais Magufuli huko nyuma wakati anahutubia Taifa katika moja ya hotuba zake amewahi kusema kwa utajiri ulioko Tanzania nchi yetu huenda nayo imekuwa ikisaidia nchi nyingine bila sisi wewe kujua.Kwa utajiri wa rasilimali za kila aina ambazo nchi yetu imejaaliwa ,kwa Rais Magufuli hizo hizo zinamtosha katika kuiendeleza nchi yetu.

Miradi mingi inatekelezwa kwa fedha zetu. Ni Rais Magufuli huyu huyu aliyeamua kusimamia vema sekta ya madini.Wazungu waliokuwa wanatuchukulia madini yetu wanamjua vizuri Rais Magufuli.Walifunga safari mpaka Jiji la Dar es Salaam kuja kujisalimisha.Leo wote tunanufaika na madini yetu.Katika hifadhi na mbuga za wanyama nako kulikuwa na ujanja ujanja mwingi Rais ameukomesha.

Kwani umesahau stori za Twiga kupandishwa ndege kwenda uzunguni? Umesahau habari za ujangiri kushamiri nchini kwetu? Tembo walikuwa wakiuliwa kwa wingi sana na majangiri.Utawala wa Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli hakuna cha Twiga kupanda ndege wala Tembo kuuliwa na majangiri.Faida inayotokana na uwepo wa hifadhi hizo sasa zinawafikia Watanzania wote.

Wakati ule wa mwaka 2015 Rais alipokuwa anaomba kura alisema amekuwa Serikalini kwa muda mrefu,hivyo anajua fedha zinapovujia, na akatuhakikishia atakwenda kuzifunga kwa Makufuli kama jina lake la Magufuli lilivyo.

 Katika hilo la udhibiti wa fedha wala sio la kujadili , sote ni mashahidi,fedha za umma zinaheshimiwa.Hakuna ufujaji kama huko nyuma.Mwenyewe amekuwa akiwaambia watumishi wa umma wasicheze na fedha za umma maana hawatabaki salama.

Tunajua huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, ni mwaka ambao Watanzania wanakwenda kuchagua madiwani, wabunge na Rais.Ni wazi kwa kazi ambayo Rais Magufuli ameifanya hana mpinzani.Watanzania wanataka kuona kazi ya kuleta maendeleo ambayo Rais ameifanya kwa uzalendo mkubwa inaendelea tena kwa miaka mingine mitano.

Oktoba 25 mwaka huu tutakuwa kwenye misururu ya kupiga kura.Tunafahamu kura ni siri ya mpiga kura lakini kwa kazi ambayo Rais ameifanya katika miaka mitano ya kwanza uchaguzi wa mwaka huu kura ya urais haitakuwa siri tena.

Kura zote ni kwa Rais Magufuli.Ukibisha ujue unabishana na ukweli.Nani aliyeko upinzani unaona anatosha kupambana na Dk.Magufuli? Acha kukunja sura nijibu tu.Nani? Mbona kimya? hakuna ,uchaguzi mkuu mwaka huu ni Magufuli tu.Serikali ya Awamu ya Tano tumeanza na Magufuli na tutamaliza na Magufuli.

Hata hivyo nihitimishe kwa kuomba radhi kwa kutumia mfano wa Ronaldo na Mess katika kuelezea utendaji kazi wa Rais Magufuli.Najua Rais wetu ni mwanamichezo mzuri sana, uwanja wa Taifa amekwenda karibu mara mbili kwenye ile  mechi ya Simba na Kagera na katika mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga.

Yaliyotokea uwanjani kwa mechi zote hizo sio muhimu kujua.Nachotaka kusisitiza Rais wetu anawajua Ronaldo na Mess maana ni mfuatiliaji mzuri wa michezo.Chini ya uongozi wake timu ya Taifa ya Tanzania tumefanikiwa kucheza michuano ya Afcon .

Watanzania narudia tena kuwakumbusha tu usisahau tulianza awamu ya Tano na Magufuli na tutamaliza na Magufuli.Mengi kuhusu yeye rejea hotuba yake wakati anafunga Bunge.Alitumia dakika 122 kuelezea yaliyofanywa na Serikali yake,tena sio yote ni baadhi tu.

Hata hivyo mwisho tena kwa umuhimu wake, zingatia hili la umuhimu wake ni kufahamu chini ya Rais Magufuli Benki ya Dunia imeitangaza Tanzania kuwa katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.

Lengo la Tanzania lilikuwa ni kufikia uchumi wa   kipato cha kati mwaka 2025 lakini chini ya uongozi mahiri wa Dk.Magufuli tumeingia kwenye hatua hiyo mwaka huu wa 2020.Tunataka nini kwa Mungu? Jibu ni moja tu atulindie Rais wetu awe mwenye afya njema na maisha marefu.


Mawasiliano yangu bado
ni yale yale tu 0713833822

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...