CHAMA cha Wafanyakazi kwenye vyombo vya Habari (JOWUTA) kimekubaliwa kuwa mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la vyama vya waandishi wa Habari (IFJ).

Maombi ya JOWUTA yalikubaliwa na IFJ katika kikao chake cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Julai 9, 2020, Brussels, Ubelgiji. 

IFJ inawakilisha waandishi wa Habari wapatao 600,000 katika nchi 140 duniani. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa JOWUTA Claud Gwandu, chama hicho kiliwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na IFJ mwishoni mwa Juni, 2020.

JOWUTA inaamini katika mshikamano wa pamoja baina ya mwandishi wa Habari mmoja, vyama vya waandishi wa Habari na hata kampuni za Habari kwa kuwa ndiyo njia sahihi ya kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari nchini na duniani kote.

 Gwandu ameeleza kuwepo kwa faida kubwa kwa JOWUTA kujiunga IFJ kama taasisi na kwa mwanachama mmoja mmoja hasa kipindi hiki ambacho sekta ya habari duniani inakabiliwa na matatizo ambayo baadhi yake yanazuia waandishi wa habari kutimiza majukumu yao.

Baadhi ya faida za JOWUTA kuwa mwanachama wa IFJ ni pamoja na wanachama wake kupata fursa za kushiriki katika mafunzo, semina na mikutano mbalimbali inayoandaliwa na shirikisho hilo moja kwa moja au kupitia ofisi yake ya Afrika yenye makao yake makuu Dakar, Senegal.

“Katika kipindi hiki tunahitaji sana kuwajengea uwezo waandishi wanachama wetu na waandishi wa habari kwa ujumla katika maeneo mbalimbali, kama kuandika habari za uchaguzi kwa ufasaha, habari za maendeleo, sayansi na teknolojia na kama inavyofahamika kuwa elimu ni ghali, hivyo nafasi hii itasaidia kuongeza kasi ya kuwajengea uwezo wanachama wetu,” alisema Gwandu.

Katika barua yake, Katibu Mkuu wa IFJ Anthony Bellanger amesema shirikisho hilo linafurahi kuona JOWUTA inajiunga katika umoja wa vyama vya wafanyakazi vya waandishi wa habari na vyama vya habari duniani.

JOWUTA ilisajiliwa rasmi Julai 26, 2018, ambapo Novemba 30, 2019 ilifanikiwa kupata viongozi katika mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika jijini Dodoma. Uchaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2006.

Kwa sasa JOWUTA ina wanachama zaidi ya 300 waliopo katika mikoa mbalimbali nchini, lakini pia tangu kusajiliwa kwake imefanikiwa kuendesha mafunzo ya Usalama na Usawa wa Kijinsia kwa waandishi wa habari wanawake 204 katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Iringa, Arusha, Mwanza, Tabora na Tanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...