Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KUFUATIA mlipuko wa virusi vya Corona (Covid_19) ulioathiri nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, asasi ya kiraia ya Karibu Tanzania Organization (KTO) imetoa mafunzo maalumu kwa njia ya masafa kwa walimu na wakufunzi kutoka vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ikiwa ni njia mbadala na endelevu ya wanafunzi kupata masomo na kujifunza wawapo nyumbani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya wiki mbili kwa walimu hao Kaimu Mkurugenzi idara ya Mafunzo kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Margreth Mussa amesema kuwa wazo hilo la KTO limekuja wakati muafaka na wametumia fursa hiyo kupitia changamoto ya janga la Corona na maarifa yaliyotolewa kwa walimu hao yatasaidia vyuo vingi zaidi ambavyo hadi sasa kuna changamoto ya walimu.

"Sote tunafahamu madhara na changamoto zilizotokana na mlipuko wa virusi vya Corona katika sekta nyingi ikiwemo sekta ya elimu ikiwemo vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo pia vililazimika kufungwa hivyo mafunzo haya yatakuwa amali kubwa kwa sasa na kwa siku za baadaye" ameeleza Margreth.

Amesema kuwa KTO imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha vyuo vya maendeleo ya wananchi vinatoa elimu bora kwa vijana wa kike waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali.

"Ni mara nyingi KTO imekuwa ikiwakutanisha walimu kutoka vyuo vya maendeleo ya wananchi na kutoa mafunzo mbalimbali na warsha na tunaamini mafunzo haya ambayo pia wameyafanya kwa vitendo ikiwemo kurekodi vipindi mbalimbali kwa masafa ikiwemo Redio, Televisheni na hata kutumia mitandao ya kijamiii itawafikia walengwa wengi zaidi hata wale ambao hawana walimu na wazazi pia wanaweza kusikiliza na kuwashauri vijana wao zaidi" ameeleza.

Pia amewashauri walimu na wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi kote nchini kushirikiana ili kufikia malengo hasa kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa kwa njia za mtandao na kuwasaidia wasichana vijana waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kwa kuwa kuzaa ni zaidi ya elimu ambayo haina mwisho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa KTO Maggid Mjengwa wamekuwa wakiwezesha vyuo 41 kati ya 54 vilivyopo nchi nzima na kuzuka kwa janga la Corona lililopelekea shule na vyuo kufungwa hivyo kama taasisi wakalazimika kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha vijana kusoma bila changamoto yoyote na tayari ndani ya siku 14 za mafunzo tayari vipindi vya masomo mbalimbali vimerekodiwa.

Mjengwa amesema kuwa, mafunzo hayo ni endelevu na yatatolewa kwa wakufunzi wa vyuo mbalimbali na kusambazwa katika vyuo vyote nchini huku akieleza kuwa janga la Corona limetoa funzo hasa kwa kuwa tayari zaidi na hadi kufikia sasa vipindi vya masomo mbalimbali yanarekodiwa katika studio ya taasisi hiyo na wanufaika watafaidika kwa kusoma wakiwa mahali popote.

Mmoja wa washiriki kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga, Miriam Juma amesema kuwa wanaamini wanajamii wengi watanufaika kupitia mafunzo hayo hata wale wasiokuwepo darasani.

Amesema kuwa kupitia rekodi walizozifanya kupitia mafunzo hayo wanaamini mabinti wengi watasaidika zaidi kwa kuwa elimu haina mwisho.
Mwalimu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msinga, Miriam Juma akiongea na wanahabari wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo na kueleza kuwa kupitia mafunzo hayo wanaamini mabinti wengi zaidi watasaidika, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Karibu Tanzania Organization (KTO) Maggid Mjengwa akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo na kueleza kuwa mafunzo hayo ni endelevu na vipindi vya masomo mbalimbali vilivyorekodiwa na walimu kupitia mafunzo hayo vitafika katika vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi.
Kaimu Mkurugenzi idara ya Mafunzo kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Margreth Mussa akizungumza na wanahabari mara baada ya kufunga mafunzo hayo na kueleza kuwa KTO imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na Wizara ya Elimu kwa kuhakikisha mabinti vijana wanapata elimu waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, na ameishukuru KTO kwa kushirikiana kwa ukaribu zaidi na na vyuo 41 kati 54 vilivyopo nchini, leo jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa mawasiliano na msimamizi wa programu hiyo Symphrose Makungu akizungumza na wanahabari kuhusiana na mradi huo ambapo ameeleza kuwa walimu wamepata nafasi ya kujifunza kwa nadharia na vitendo na wanategemea baada ya mafunzo hayo walimu wataweza kuwafikia walengwa wengi zaidi hata wale wasioweza kuvifikia vyuo hivyo, Leo jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...