Na Catherine Magige

MWANZONI mwa mwaka huu, yaani Januari mwaka 2020, niliandika makala kuhusu Rais Magufuli na Tanzania ya kesho. 

Katika makala yangu hiyo niliangalia mipango ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Tano toka imeingia madarakani hadi kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano kitapomalizika. 

Niliangalia Tanzania ijayo chini ya Rais Magufuli na ndio sababu nikaipa makala yangu jina la Rais Magufuli na Tanzania ya kesho. Kwa kutilia maanani kuwa watanzania wako katika mchakato wa kuamua Serikali ya awamu ya sita iwe na muonekano upi, ni haki nikamwangalia Rais Magufuli na Tanzania ya leo.

Ukisikiliza hotuba ya Rais Magufuli wakati wa ufunguzi wa Bunge, tarehe 20 Novemba, 2015; na kisha ukasiliza hotuba ya Rais Magufuli wakati wa kufunga Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jun 16, 2020 utakubaliana na mimi kuwa ile Tanzania ya kesho niliyoizumngumzia Januari 2020 inaweza kuangaliwa kwa mtazamo wa Tanzania ya leo.

Novemba 2015 Rais Magufuli alitoa matazamio yake ya Tanzania inayokuja kulingana na maagano yake kwa Tanzania wakati wa kuomba ridhaa yao kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Juni 2020 Rais Magufuli alitoa mrejesho kwa watanzania kama alivyowaahidi wakati wa kuomba ridhaa yao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Magufuli alitoa mrejesho wa orodha ya yaliyofanyika (Checklist) kufuatana na ahadi zake kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Checklist ya Tanzania ya leo ya Rais Magufuli ni hii hapa:
Madini – Rais Magufuli aliahidi kuwa atahakikisha madini yetu yanawanufaisha watanzania ambao ndio wamiliki wa raslimali hii. Pamoja na kuunda wizara mahsusi inayoshughulikia madini tu, tumeona madini yetu yakiuzwa katika masoko ya ndani ambayo yameanzishwa katika kila mkoa huku wachimbaji wadogo wazalendo wakinufaika moja kwa moja na mageuzi haya. Hakuna uongo tena wa makinikia kuwa hayana thamani au hasara za makampuni ya madini huku yakilipa gawio huko nje ya nchi. 

Heshima ya tanzanite imerudi kwa watanzania na kufuta tusi la “wajinga ndio waliwao” maana sasa dunia inatambua kuwa tanzanite ni yetu watanzania hata kwa takwimu za mauzo katika soko la dunia. 

Aliyekejeli ujenzi wa ukuta wa Mererani wa kilometa 25 anaweza kumuuliza Bilionea Laizer au ukoo wa mvumbuzi wa tanzanite, Mzee Ngoma. Rais Magufuli amesimamia upitishwaji wa sheria zinazowapa haki watanzania kumiliki madini yao kisheria ambapo Kampuni ya Twiga Minerals Company inayomilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick. 

Dola za Marekani milioni 100 kati ya Dola za Marekani 300 zimelipwa kwa watanzania na Kampuni ya Barick kama fidia ya udanganyifu waliokuwa wakitufanyia kutokana na usingizi wa pono tuliokuwa tumelala.

Mafanikio katika sekta ya madini sio porojo bali hesabu zake pia zinadhibitisha hilo ambapo shilingi bilioni 58 zilitarajiwa kukusanywa mwezi Aprili 2020 ukilinganisha na shilingi bilioni 43 kama kiwango cha juu kwa mwezi kwa muda uliopita. 

Miundombinu – Hili ni eneo la kujidai la Rais Magufuli. Tunakumbuka jinsi alivyoitendea haki sekta hii toka akiwa waziri mwenye dhamana. Hatukumwamini na tulidhihaki pia kuwa hizi ni “stori”za kisiasa aliposema atafufua ATCL, atajenga reli ya kisasa, atarudisha usafiri wa reli Moshi na Arusha, ataboresha usafiri wa majini na ataboresha na kujenga barabara za mijini na za kitaifa.

Tanzania ya leo ya Rais Magufuli imedhirisha umakini wa Rais Magufuli katika kusimamia utekelezaji wa hayo anayoyaamini. Pamoja na maamuzi ambayo wengi tuliyatilia shaka kwa kuangalia historia ya nyuma, kuna swala kuu moja ambalo linatanabaisha Rais Magufuli kama mtu wa pekee katika utekelezaji wa maamuzi yake. 

Suala hili ni jinsi alivyosimamia mapato ya taifa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.Tuliaminishwa na tukaamini kuwa bila mikopo kutoka nje ya nchi hatuna uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ambayo kiuhalisia ndio chachu ya maendeleo ya nchi yetu.
 
 Rais Magufuli hakukubaliana na hilo na akaamua kutekeleza miradi hiyo ya kimkakati kwa kutumia mapato yetu ya ndani. Alijua fedha ipo ila inatumika isivyopaswa na akaamua kuiwekea mikakati ya upatikanaji wake. Alisema na kuamini kuwa Tanzania ni tajiri na ina uwezo kifedha, tukamdhihaki! 

Amethibitisha maneno yake kwa vitendo kwa kununua ndege 11 ili kuifufua ATCL ambapo mtanzania ameweza kutoka sehemu mpoja ya nchi hadi nyingine chini ya masaa matano. Ameiunganisha Tanzania na mataifa ya nje kwa usafiri wa anga. Alizungumzia kukuza utalii na kuhakikisha bidhaa zetu zinapata masoko nje ya nchi akijua fika bila usafiri wa anga wa kuaminika ndoto hii inabaki kuwa ndoto. 

Ametumia pesa ya ndani kuanza kujenga reli ya kisasa ili kuendana na kiu yake ya kutaka kuona Tanzania inaingia katika uchumi wa kati. Anajua vizuri kuwa ukosefu wa usafiri imara, nafuu na madhubuti, kama wa reli, ulivyochangia kudumaza uchumi wetu.

Alishuhudia uwezo mdogo na gharama kubwa ya usafirishaji kwa kutumia barabara akiwa waziri. Hakutaka kosa hili lijirudie tena wakati wa uongozi wake na ndio maana amehakikisha usafiri wa reli kwenda Moshi na Arusha unarudishwa baada ya kufutika na kusahaulika kabisa. 

Kwa upande wa usafiri wa majini, tumeona jinsi uwezo wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga ulivyoongezeka huku usafiri katika maziwa yetu makuu yakiwamo Victoria, Nyasa na Tanganyika na hata vivuko katika mito ulivyoboreshwa.

Barabara zetu za kitaifa na mijini ni ushaidi mwingine wa mafanikio ya Tanzania ya leo ya Rais Magufuli. Sio rahisi kuanza kuzitaja moja baada ya moja. Kwa kifupi ametekeleza kwa vitendo maono yake ya kuwa na Tanzania ya leo yenye miundombinu ya usafirishaji ya kisasa na bora. 

Swala la nishati ya umeme lilikuwa kama laana kwa watanzania. Tunakumbuka kashfa za ufisaidi zilizoambatana na swala hili. Mgao wa umeme na kukatika mara kwa mara kwa umeme ilikuwa ni “kauli mbiu” ya TANESCO!.

Katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli, mgao na kukatika kwa umeme ni hadithi. Uwezo wa nchi katika uzalishaji wa umeme unaongezeka kila kukicha. Huku tukisubiri kukamilika kwa Mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere kwenye Bonde la Mto Rufiji utakaotupa umeme wa Megawati 2115, vijijini umeme wa REA unawaka!. 

Mradi wa Bwawa la Nyerere umepigwa vita sana na hata watanzania wenzetu bila kufahamu wakaanza kucheza ngoma wasiyoijua. 
 
Hawakukumbuka maslahi ya taifa yalivyowekwa mbele katika utekelezaji wa miradi ya nishati huko Uganda na Ethiopia.Hawana habari na maslahi mapana ya taifa yalivyotangulizwa na Norway, Japan na Iceland katika kuridhia uhifadhi wa nyagumi! Mifano iko mingi sana, muhimu Tanzania kwanza. 

Kama nilivyoainisha hapo juu, swala la kujiuliza kuhusu Tanzania ya leo ya Rais Magufuli ni jinsi alivyoweza kuibadili Tanzania kwa kutumia fedha za ndani ambazo kwa miaka mingi zilionekana hazipo au hazitoshi. Amekuwa mzalendo wa kweli kwa nchi yake.

Amekitumia cheo chake kwa faida ya nchi yake tofauti na hadithi tulizozoea za watawala wa Afrika, yeye kwanza nchi baadae! Sekta za afya na elimu ni uthibitisho mwingine katika hoja hii. Miaka mitano inakwisha akiwa ana vituo vipya vya kutolea huduma za afya 1,769 ambamo kuna zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda 3. 

Hizi ni fedha zilizokuwazikitumika kufanya safari za nje ya nchi na makongamano hapa nchi yasiyo na tija kwa nchi bali wahusika binafsi. Ni kodi zetu zilzokuwa zikiingia mifukoni mwa wafanyakazi wasiowaaminifu au zikibakia kwa wafanyabiashara wakwepaji wa kodi. Ni fedha zilizokuwa zikilipwa kwa wafanyakazi na wanafunzi hewa!. 

Ni fedha hizo ambazo sasa zinawezesha elimu kwa shule za msingi na sekondari kutolewa bila malipo wakati miundombinu yake ikiendelea kuboreshwa na kuongezwa kila siku. Hatusikii tena kilio cha madawati wala migomo kutokana na kuchelewa kwa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya juu. 

Sitaacha kurudia kuulezea uadilifu wa Rais Magufuli katika kuhakikisha raslimali za watanzania zinatumika kuwaletea maendeleo yao. Hata kama angekuwa na mipango mizuri kiasi gani, bila kuwa na raslimali zitakazowezesha utekelezaji wa mipango hiyo bado ingebakia katika makablasha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
 
 Ameyaishi maneno ya Baba wa Taifa kuwa taifa lisilokusanya kodi haliwezi kujikwamua kiuchumi. Alieleza nia yake ya kuhakikisha kodi zinalipwa kama inavyotakiwa toka mwanzo wa utawala wake. Pamoja na kutilia mkazo swala la ulipaji kodi alipitia kodi zilizokuwapo na kuzitoa kodi sumbufu na hata kupunguza wigo wake ili kuwafanya wananchi walipe kodi bila matatizo.

Matokeo yake ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa mwezi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 1.3 kwa sasa. Usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuhakikisha yanakusanywa kwa nidhamu, kumesababisha kuongezeka kwa mapato ya ndani kwa shilingi trilioni 7.

Kwa kutanguliza maslahi ya Taifa letu mbele, Serikali ya Rais Magufuli imeweza kutupa raslimali kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imekuwa katika maandishi miaka nenda rudi.
Nimalize kwa kusema kuwa Tanzania ya leo ya Rais Magufuli inaonekana. 
 
Pamoja na checklist niliyotoa hapo juu bado yako mengi tu ambayo yamefanyika katika miaka hii mitano. Kuna mafanikio ya soko la utali ambapo pamoja na kuhakiksisha wanyama wetu wanaongezeka na ujangili unakwisha, idadi ya watalii na mapato yameongezeka sana.

Tanzania inarudia nafasi yake ya kuwa kitovu cha utalii katika bara la Afrika hasa kwa fukwe zake na mbuga za wanyama zilizotapakaa kote nchini. Tanzania ya leo ya Rais Magufuli inafungua Tanzania ya kesho ya Rais Magufuli kwa miaka mingine mitano ijayo. Mwenye macho haambiwi tazama. 

Mwandishi wa Makala haya ni Catherine Magige

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...