Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akiangalia moja ya tuzo ya Filamu (Bongo Movie), kutoka kwa Gabo Zigamba alipotembelea banda hilo katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl.Julius Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.Picha na Idara ya Habari-MAELEZO

**********************************

Na Mwandishi wetu-MAELEZO


Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema hivi karibuni itaanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ili kuwasaidia wasanii kujiendeleza kiuchumi kupitia masuala mbalimbali nje ya sanaa.

Akizungumza katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbasi aliwapongeza wasanii wote kwa kuja na mawazo ya kutangaza bidhaa zao mbalimbali za ujasiriamali katika maonesho hayo na kusema Serikali iko tayari kuanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ili kuinua uchumi wao.

“Nimetembelea banda la wasanii kwa kuwa Sanaa ni kitu muhimu sana kwa nchi yetu, nimeona kazi zao nzuri nje ya Sanaa, kwa hiyo Serikali iko pamoja na ninyi na tunatarajia mwezi Agosti mwaka huu tutaanzisha mfuko wa Sanaa na Utamaduni ambao utawawezesha wasanii kueleza mawazo yao na kupata fedha ya kuendeleza mawazo hayo”, Dkt.Abbasi.

Alibainisha kuwa kupitia mfuko huo msanii yeyote mwenye wazo lolote kama vile wazo la siasa, biashara au la sanaa yenyewe ataweza kuwasilisha wazo hilo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili liweze fanyiwa mchakato na kuwezeshwa kupata msaada wa fedha kutoka mfuko huo.

Dkt.Abbasi aliongeza kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuihamishia Taasisi inayoshughulika na hakimiliki ya kazi za wasanii (COSOTA) katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili wasanii waweze kupata haki za kazi zao haraka.

Aidha, Dkt.Abbasi alitembelea banda la timu ya soka ya Yanga na kujionea bidhaa za timu hiyo zikiwemo jezi na vikombe vya ushindi na ametoa wito kwa timu kubwa kushiriki maonesho ya Sabasaba kwani inachangia kutangaza soka la Tanzania.

“Nawapongeza timu ya Yanga kwa kushiriki maonesho haya ambayo ni fursa kwa timu zetu kubwa zinazopendwa na wananchi kuja kutangaza bidhaa zao kwani itasaidia pia kukuza soka hapa nchini”, Alisema Dkt.Abbasi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...