Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi),  Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi Mkataba na Michoro ya Majengo ya kituo cha kukuzia viumbe maji kwa Meneja wa Kampuni ya Corporation Sol, Simeo Machibya Julai 8, 2020 katika kijiji cha Rubambangwe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi),  Dkt. Rashid Tamatamah amesema serikali inatarajia kujenga Kituo kikubwa cha ukuzaji wa viumbe maji Wilayani Chato, Mkoani Geita, huku akisema kuwa kituo hicho kitakuwa  kinatoa zaidi ya tani 10 za samaki kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi eneo la ujenzi wa kituo hicho  kwa kampuni ya ukandarasi ya serikali, Corporation Sol Julai 8, 2020 katika kijiji cha Rubambangwe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, Dkt. Tamatamah amesema kuwa mradi huo mpaka kukamilika utagharimu kiasi cha Sh Bilioni 3.8 na tayari Wizara imeshalipa fidia ya shilingi milioni 42 kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linaukubwa wa ekari 28.

“Mradi huu utakuwa mkubwa kuliko yote nchini na utakuwa na mabwawa ya kufugia samaki, vitotoleshi vya samaki , kiwanda kidogo cha kuchakatia samaki, jengo la kutengeneza chakula cha samaki, shamba darasa, hosteli na ofisi za kituo hicho”, Amesema Dkt. Tamatamah.

Ameongeza kuwa mradi huo ambao unategemea ujenzi wake kuchukua miezi mitatu na kukamilika Oktoba, 2020 utakuwa jengo la vitotoleshi vya samaki ambalo litakuwa na uwezo wa kutoa vifaranga zaidi ya milioni mbili kwa mwaka.

Aidha, Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Viumbe Maji, Dkt. Nazaeli Madala ameongeza kwa kusema kuwa  kituo hicho kitakuwa ni ufumbuzi wa changamoto ya uhaba wa samaki ulioanza kujitokeza kwenye vyanzo vya asili.

“Kituo hiki kitahudumia mikoa yote inayozunguka kanda ya ziwa na maeneo ya jirani na ukanda huu, na tutawafundisha wafugaji samaki, maafisa ugani wa fani ya ufugaji wa samaki, pia kitatumika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma katika ngazi mbalimbali huko vyuoni,”amesema Madala.

Dk Madala ameongeza kuwa kituo hicho kitakuwa kama cha mfano na kitawasaidia kutoa muongozo wa kujenga vituo vingine katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, Nyasa na maeneo ya Pwani lengo likiwa ni kuhakikisha viwanda vyote vya samaki havikosi malighafi ili kufikia adhma ya kuwa nchi ya viwanda. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho aliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kupeleka mradi huo katika Wilaya hiyo na aliahidi kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za ujenzi wa kituo hicho hadi kitakapokamilika.

Naye, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Rubambangwe, Restituta Majura alisema kuwa mradi huo ukikamilika utawanufaisha sana wakazi wa kijiji hicho kwani  utatoa ajira kwa wananchi na kusaidia kuchachua uchumi wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...