Katibu Mkuu wa Chama hicho, Rashid Mtima akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania(TALGWU), kimesema kuwa kinaendelea na juhudi za kutetea haki na maslahi ya wanachama wao na kwamba taarifa kuwa kuna ubadhirifu ndani ya Chama hazina ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi juu ya utendaji kazi wa Chama hicho, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Rashid Mtima amesema kuwa taarifa hizo zimeleta mkanganyiko mkubwa kwa viongozi na wanachama hadi baadhi yao kukosa imani na Chama chao.

Amesema chama chao kilianzisha Taasisi ya fedha kwa lengo la kuwasaidia wanachama wake kupata mikopo kwa riba nafuu.

"Chama hiki kilianzishwa na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya wafanyakazi, hivyo TALGWU na  TALGWU Microfinance PLC ni taasisi mbili tofauti kwa mujukumu na uongozi ni tofauti kiutendaji. Oktoba 2018 uongozi wa Chama uligundua kuna changamoto kwa upande wa uendeshaji wa taasisi na uongozi uliotoa maelekezo kwa Bodi ya TALGWU Microfinance plc kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa uchunguzi maalum." amesema. 

Ameongeza kuwa, baada ya kufanyika kwa uchuguzi huo ambao ulipelekea watendaji wakuu wa taasisi kusimamishwa kazi na hatimaye kuachishwa kazi.

Akizungumzia suala la Ujenzi la Kitega Uchumi cha Chama, Mtima amesema tangu uongozi wao uingie madarakani Septemba 2016, ulikuta ujenzi huo wa kitega uchumi umesimamishwa na baada ya kushughulikia mnamo mwezi Agosti 2017 mamlaka husika ziliruhusu ujenzi kuendelea baada ya kujiridhisha unakidhi viwango vya kisheria.

“Tangu tulipoingia madarakani TALGWU haina madeni ya makato ya kisheria kama taarifa zinavyoeleza, bali madeni yaliyopo ni ya kawaida ya kitaasisi ambayo hayajasababishwa na ujenzi wa jengo la kitega uchumi kama taarifa zilivyodai,”alisema Mtima na kuongeza;

“Nashangaa katika taarifa hizo imesema TALGWU ilinunua samani za sh. bilioni 2, hilo si kweli bali samani zilizonunuliwa zilikuwa na thamani ya sh,. milioni 883, huku lifti ikinunuliwa kwa kiasi cha sh.milioni 980 ambayo ilijumuisha ununuzi, ufungaji pamoja na matengenezo kipindi cha matazamio,” amesema.

Amefafanua kuwa, majukumu ya TALGWU yanatekelezwa na Chama hicho kwa mujibu wa ibara ya 1.4 ya katiba ya Chama toleo la  mwaka 2016. Kwa mujibu wa Mtima Chama hicho kipo mstari wa mbele katika utetezi wa kesi mbalimbali zinazowakabili wanachama wake kwa kutumia mawakili wa Chama, makatibu wa mikoa na mawakili wa nje.

“Akitolea mfano wa Chama kusimamia kesi za wanachama wake, alisema kimesimamia kesi takribani 130 na kesi zilizoisha zilikuwa 52.

"Chama kimefanikiwa kushinda kesi 47 huku kesi 31 zikiwa bado zinaendelea kufuatiliwa katika Mahakama mbalimbali nchini,” amesema na kuongeza;

“Mwaka 2018 Chama kilisimamia suala la watumishi waliosimamishwa kazi kwa kuwa na elimu ya darasa la saba na wote walirudishwa kazini, huku mwaka 2019 Chama kilishirikiana na TUCTA kupigania kurudishwa kwa kikokotoo cha awali na hatimaye wanachama wetu wanaostaafu wanalipwa kwa kanuni za awali."

Amesema wanachama wao wamekuwa wakinufaika na mambo mengi kama utoaji wa flana na kofia wakati wa  sikukuu za Mei Mosi na pia Chama kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wanachama wake kwa viongozi wa ngazi za mikoa na matawi nchi nzima.

Amesema kila mwezi Chama kimekuwa kikipeleka fedha za uendeshaji wa Ofisi za Mikoa na ruzuku za matawi. "Chama hakina ufujaji wowote wa fedha uliofanyika kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, kwani hadi kufikia Machi 2020 chama kina wanachama 71,948," alisema. 

Akizungumzia suala la vikao vya ndani, nje na vikao vya Posho, Mtima amesema kwa mujibu wa sura ya tano ya katiba ya Chama toleo la mwaka 2016 imeainisha vikao vyote vya Chama vya kikatiba ambapo kamati ya Utendaji taifa hukutana mara nne kwa mwaka na Mkutano Mkuu wa Taifa ufanyika mara mbili ndani ya miaka mitano.

Amebainisha kuwa, vikao vya posho vinavyoitishwa ni kwa mujibu wa Katiba ya chama na hata siku moja katibu Mkuu hajawahi kuitisa vikao visivyo rasmi au nje ya katiba, kikanuni,utaratibu na bajeti ya Chama.

Mtima amesema tangu uongozi wao uliopo madarakani uingie kazini Septemba 2016, Ofisi ya Katibu Mkuu imekuwa ikitimiza takwa la kikatiba na kuitisha vikao hivyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...