Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM NEC kilichofanyika katika ukumbi wa White House jijini Dodoma leo tarehe 10 Julai 2020.


Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.John Magufuli ametumia mkutano wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho kutuma ujumbe kwa wana CCM Zanzibar kwa kuwataka kuwa wamoja na wasikubali kuyumbishwa na maneno ya wapinzani wao ambao wanataka kuivuruga Zanzibar huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dkt.Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake ulitukuka na wa mfano bora wa kuigwa.

Akimzungumzia Rais Shein mbele ya wajumbe wa mkutano huo uliofanyika leo Julai 10,2020 Mjini Dodoma, Dk.Magufuli amesema wakati Rais Shein anaingia kwenye nafasi hiyo kulikuwa na matatizo mengi lakini ameyatatua kwa kwa upole, ameingia madarakani amefanikiwa kununua meli za kwenye bahari na ameongeza ukuaji wa uchumi.

"Rais Shein umeweka mikakati ya kuanza kuchimba mafuta, umesimamia vizuri mapinduzi matukufu lakini umesimami vizuri Muungano, sikupata shida Mzee wangu kila nilipokuita ulitikia, tumetatua matatizo mengi pamoja, umekuwa mkweli na muwazi sana.Kuongoza hakuhitaji makeke, hakuhitaji matusi, wewe baba ni mnyenyekevu, Mungu akujaalie, najua huwezi kupendwa na kila mmoja.

"Wanakupenda kila mmoja kwasababu gani?Haiwezekani, inawezekana hata mama Shein wakati mwingine anakuchukia huwezi kujua lakini wewe uliyatimiza yaliyo mazuri kwa Zanzibar,najua kesho yatazungumzwa mengi kuhusu wewe kwenye Mkutano Mkuu.
 
Nachowaomba ndugu zangu wazanzibar, kajengeni umoja wenu, msisikilize maneno ya watu , msisikilize yanayozungumwa na wapinzani mkayabeba, mnajua hata baada ya uchaguzi huu labda kwa sababu ulikuwa live lakini yangezungumzwa maneno ya kila aina , watazungumza hili, watazungumza lile, haya sio maneno ya wana CCM.

"Haya maneno ni ya wapinzani wenu, kashimaneni, bila Chama Cha Mapinduzi Zanzibar hakuna Muungano, bila CCM hakuna maendeleo, Zanzibar ni nchi tajiri wanaitamani mabeberu, Baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume walikuwa ni watu wenye maono ya mbali , nataka niwaambie ndugu zangu Zanzibar bila Muungano pia hakuna Pemba wala Unguja, na baadae mtaingia vipande vingine Kaskazini na Kusini, kwa hiyo mtagawanyika, mtagawanyika,"amesema Dkt.Magufuli.

Amewaomba Zanzibar wasimame imara ma wazingatie mapinduzi matukufu yaliyofanywa na waasisi wetu, wakajenge umoja huku akifafanua kuwa hapawezi kukawa na marais wote na saa zingine hata kuchaguliwa huku wamtangulize Mungu."Mungu alishapanga siku moja Dkt.Mwinyi atashinda, hata mimi sikujua kama siku moja nitakuwa Rais, lakini kwa mapenzi ya Mungu akasema Magufuli utakuwa Rais na wala siwezi kuwa na kiburi kwasababu ya nafasi hii, hii kazi ni ya utumishi na utumishi una gharama kubwa.

"Nachotaka kuwaambia ndugu zangu wajumbe wa Halmashauri Kuu tusimame imara na umoja nawapongeza sana, ninyi mlioshiriki kwenye mchakato wa uchaguzi kule Zanzibar kashirikianeni na Mwinyi, yatazungumzwa mengi lakini ninyi kachapeni kazi , kila mmoja na zamu yake,"amesema Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa mbele ya wajumbe wa mkutano huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...