Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Katavi jana. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na wa tatu kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipeana mkono na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoa wa Katavi Michael Nzyungu ikiwa ni ishara ya kupongezana baada ya Waziri wa Ardhi kumkabidhi gari lenye thamani ya shilingi milioni 150 na vifaa vingine vya upimaji kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi katika sekta ya ardhi nchini.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi na Naibu wake Dkt Angeline Mabuka wakiongozwa kuelekea kutoa gari na vifaa vya upimaji kwa ajili ya urahisaji utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Katavi jana baada ya kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Katavi jana, Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Msajili Msaidizi wa Hati Liz Kibada wakati akikagua majalada ya ardhi katika ofisi ya Msajili wa hati jana katika uzinduzi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Katavi. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi mbalimbali waliokwenda kushuhudia uzinduzi wa ofisi za ardhi mkoa wa Katavi jana.

(PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

***********************************

Na Munir Shemweta, WANMM KATAVI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekerwa na tabia ya baadhi ya viongozi kuhusika kupora ardhi ya wananchi na kueleza kuwa muarobaini wa viongozi hao umefika kufuatia watendaji wa sekta ya ardhi kuhamishiwa Wizarani sambamba na kuanzishwa ofisi za ardhi katika mikao.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema hayo wakati wa kuzindua ofisi ya ardhi mkoa Katavi wilayani Mpanda jana ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Alisema, wapo baadhi ya viongozi wa wilaya na mkoa ambao ni sehemu ya migogoro ya ardhi na wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kwa kupora na kuuza ardhi za wananchi tabia aliyoieleza kuwa inamkera rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli.

Kwa mujibu wa Lukuvi, uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa pamoja na uhamishaji watendaji wa sekta ya ardhi kutoka TAMISEMI kuja Wizarani unatoa nguvu kwa watumishi wa sekta ya ardhi kutumia na kusimamia sheria na kuonya viongozi kutojihusisha na kupora ardhi za wananchi na kubainisha kuwa ardhi itapangwa na kusimajiwa kwa mujibu wa sheria.

‘’ Kuna viongozi wa kuchaguliwa na wa kuteuliwa wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kupora ardhi za wananchi, safari hii hakuna fursa maana watendaji wote wa sekta ya ardhi wako chini ya Wizara ya ardhi, madiwani hawawezi tena kuwaazimia kuwafukuza.’’ alisema Lukuvi

Akizungumzia suala la upimaji ardhi katika mkoa wa Katavi, Lukuvi aliagiza hadi kufikia mwisho wa mwaka huu 2020 vijiji vyote katika mkoa huo viwe vimepimwa na kupatiwa hati za kijiji sambamba na wamiliki 15,000 waliokwama kupewa hati kutokana na urasimu kupatiwa hati zao na kuweka wazi kuwa, hivi sasa hakuna visingizio kwa kuwa vifaa kwa ajili ya upimaji vipo.

Agizo la Lukuvi linafuatia kuelezwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Katavi Siyabumi Mwaipopo kuwa kati ya vijiji 172 vilivyopo kwenye mkoa wa Katavi ni vijiji vitatu tu ndivyo vilivyopimwa na kupatiwa hati za vijiji.

‘’Mwaka huu uwe wa mwisho kwa migogoro ya ardhi nchini kwani nyenzo zote zipo ikiwemo wataalamu pamoja na vifaa vifaa vya upimaji na nawataka viongozi wa wilaya na mkoa wasiwe sehemu ya migogoro’’ alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisisitizia suala la ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi ambapo alisema ni muhimu wamiliki wa ardhi wakaepuka kuwa na malimbikizo ya kodi ya ardhi kwa kutii sheria ya kulipa kodi mujibu wa sheria.

Naye Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera mbali na kushukuru uamuzi wa kuanzisha ofisi ya ardhi katika mkoa wake, aliwataka wananchi wa Katavi kuitumia fursa ya kuwa na ofisi ya ardhi ya mkoa kupima ardhi na kumilikishwa na kusisitiza kuwa mkoa wake utaandaa opresheni maalum ya kupima ardhi katika mkoa mzima.

Uzinduzi ofisi ya ardhi mkoa wa Katavi uliambatana na makabidhiano ya vifaa mbalimbali ambapo Waziri Lukuvi alikabidhi gari lenye thamani ya shilingi milioni 150 pamoja na vifaa vya upimaji kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...