Julai 27, 2020- Asasi ya Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 57,881,360 kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) katika hospitali ya St. Mary's iliyopo Kibara wilayani Bunda.

Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa asasi hiyo ambaye pia ni mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano, Rosalynn Mworia alisema kwamba jukumu la taasisi hiyo ni kurudisha tabasamu kwa jamii, hivyo kutoa vifaa tiba kwa ajili ya watoto njiti ni faraja kwa taasisi yake, “tunafuraha kuwa sehemu ya kuokoa maisha kwa watoto njiti, maana vifaa tiba hivi vitawasaidia kuendelea kuishi na hivyo kutimiza ndoto na malengo yao hapo baadaye,”.

Kati ya malengo ya taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation ni kuokoa maisha ya kina mama na watoto na ndio maana wamekuwa mstari wa mbele katika kuunga juhudi za serikali katika kutokomeza vifo vya kina mama na watoto nchini.

Katika miaka ya nyuma, taasisi hiyo imechangia vifaa tiba 4,161 katika hospitali na vituo vya afya hapa nchini kama: Pwani, Tabora, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Rufiji, Lindi, Kigoma na hivi karibuni wametoa msaada wa vifaa tiba huko mkoani Arusha katika kituo cha Afya Muriet. lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa njiti wanaishi na kukuwa ili kutimiza malengo yao, mifano hai ni hopitali ya mkoa wa Dodoma, Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu na nyinginezo nyingi, aliendelea kusema Mworia.

Alisema, “leo hii tumechangia vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 57,881,360 katika hospitali hii, lengo ni kusaidia watoto wote wanaozaliwa njiti hospitalini hapa, na kuhakikisha wanapata huduma inayostahiki kupitia vifaa hivi, kwa sababu watoto wote wana haki ya kuishi, hakuna sababu ya wao kupoteza maisha kwa vile wamekosa vifaa vya kuwasaidia kuendelea kuishi,” alisema Mworia.

Mchango wa vifaa tiba ulijumuisha vifaa muhimu vya kuokoa maisha kama vile vifaa vya oksijeni ambavyo vitasaidia watoto njiti kupumua, viongeza joto kwa ajili ya kuhifadhi watoto hao, mashine za tiba mwanga (phototherapy machine), na mashine maalum za kupimia mapigo ya moyo, lakini pia walitoa vitanda vinne, shuka 50, na mablanketi 20.

Shirika la Afya duniani linaonesha kwamba kila mwaka watoto milioni 15 huzaliwa kabla ya wakati kusini mwa jangwa la Sahara ambapo watoto milioni 1 hufariki. Lakini imethibitika kuwa Watoto njiti wana nafasi kubwa ya kukuwa na kuwa na afya nzuri endapo watapata msaada wa vifaa na usimamizi mzuri wa kiafya kuzingatiwa.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza Renatusa Nkwande aliishukuru taasisi hiyo kwa kazi wanayofanya, “kwa mara nyingine tena napenda kuwashukuru kwa kazi mnayoifanya pamoja na kujituma kwenu kuhakisha kwamba akina mama na Watoto nchini wanapata huduma, pia watoto wote wanaozaliwa kabla ya muda wanaishi na kufikia malengo yao,” alisema huku akiongeza kwamba wana imani kuwa vifaa vilivyokabidhiwa hospitalini hapo vitatumika kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma bora ya afya kwa watu wengi zaidi hususan akina mama na watoto wilayani humo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bunda Mhe. Lydia Bupilipili akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima alitoa shukurani za dhati kwa kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia Asasi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa msaada huo utakaowezesha watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kupata matibabu kupitia vifaa tiba hivyo.

“Hii itasaidia kupunguza vifo vya watoto mkoani Mara na pia ina maana kubwa kwetu kwa kuona hata Bunda kuna watoto wanazaliwa kabla ya wakati huku mama zao wanafanyiwa ukatili lakini nyinyi mmeweza kuja na kutoa msaada kwa ajili yao”, alisema Bupilipili.

Aliziomba taasisi nyingine kujitokeza na kuunga mkono juhudi za kampuni ya Vodacom Tanzania ili kurudisha tabasamu kwa jamii pale wanapoguswa.
 Mkurugenzi wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia (wa pili kushoto) akikabidhi moja ya mashine kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) katika hospitali ya St. Mary's iliyopo Kibara, wilaya ya Bunda  kwa mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Lydia Bupilipili (wa pili kulia), wanaoshuhudia ni Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza Renatus Nkwande na Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Samuel Paul. Jumla ya vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 57,881,360   vilikabidhiwa kutoka taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, vifaa hivyo vitawasaidia watoto uwezo wa kupumua, kuongeza joto na kuwapa tiba mwanga.
Mkurugenzi wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia akikabidhi sehemu ya msaada katika hospitali ya St. Mary's iliyopo Kibara, wilaya ya Bunda kwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza Renatus Nkwande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...