Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii
MAHAKAMA ya Rufaa imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuruhusu makosa yasiyo na dhamana yadhaminiwe na kubainisha kwamba kifungu kinachozuia dhamana hakikinzani na Katiba na kukubali rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG) 

Uamuzi wa kukubaliwa kwa rufaa hiyo ulisikilizwa na jopo la majaji watano, Stella Mugasha, Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi, na umesomwa leo Agosti 5, 2020 na msajili Mwandamizi wa mahakama ya rufaa Eva Nkya 

Katika uamuzi wao wamesema kifungu namba 148(5) A mpaka E havikinzani na Katiba na vinakidhi masharti na kwamba kifungu hicho kinachobainisha makosa ambayo hayadhaminiki kinakidhi matakwa ya Kikatiba.

"Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama inatamka kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu umebatilishwa.

Baadhi ya makosa yaliyo katika kifungu hicho ni makosa ya mauaji, unyang'anyi wa kutumia siraha, uhaini, ugaidi, utakatishaji fedha na kesi za dawa za kulevya. 

Makosa mengine ni mtu aliyewahi kufungwa miaka 30 jela hataweza kupata dhamana, mtu aliyepewa dhamana akashindwa kutekeleza masharti ya dhamana au akaruka dhamana, pale ambapo mtu anatakiwa kukaa ndani kwa ajili ya usalama wake, pale ambapo kosa linazidi milioni 10.

Mapema, DPP na AG walikata rufaa hiyo wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri lililofunguliwa na Dickson Sanga akitaka makosa hayo yawe na dhamana kwa sababu kifungu kilichokuwa kinazuia kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mei 18, mwaka huu mahakama Kuu ilitoa uamuzi dhidi ya Maombi hayo na kusema kwamba Kifungu cha 148 (5)  cha sheria ya makosa ya jinai kinakiuka Katiba.

Katika rufaa yake DPP na AG walidai kifungu hicho hakikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa Mahakama Kuu ilikosea  kisheria kutamka kuwa kifungu namba 148(5) kinakiuka Ibara ya 13(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia mahakama  hiyo ilifanya makosa ya kisheria kutamka kuwa Kifungu hicho namba 148 cha sheria ya makosa ya jinai hakithibitishwi na Ibara ya 15(1) na (2)(a ) ya Katiba wa Jamhuri ya Muungano,  kwamba kifungu hicho kilikiuka Katiba pamoja na kwamba mjibu rufaa alishindwa kuthibitisha madai yake pasi kuacha shaka.

Katika hoja nyingine ya warufani hao walidai kwamba Mahakama kuu ilikosea kupinga kifungu hicho bila kuzingatia shida zinazoweza kusababishwa katika mfumo mzima wa utawala wa haki za Jinai nchini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...