Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti akizungumza na viongozi wa chama cha wachimbaji madini wa mkoa huo (MAREMA) walipotembelea ofisini kwake kujitambulisha kwenye ziara yao ya kutembelea machimbo na kutatua changamoto mbalimbali za wachimbaji madini, kulia ni Mwenyekiti wa MAREMA Justin Nyari na Katibu wa MAREMA Tariq James.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara, (MAREMA) Justin Nyari (wapili kulia) akizungumza na Ofisa madini mkazi wa mkoa huo Godfrey Nyanda, baada ya viongozi wa Marema kutembelea ofisini kwake kwenye ziara yao ya kutembelea machimbo na kutatua changamoto mbalimbali za wachimbaji madini, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa MAREMA, Money Yusuf na kulia ni Katibu Msaidizi wa MAREMA,  Joseph Manga.
******************************
Na Mwandishi wetu, Babati
VIONGOZI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) wameanza ziara ya wiki mbili kutembelea wachimbaji mbalimbali wa madini kwenye Wilaya za Babati, Mbulu, Kiteto, Hanang’ na Simanjiro. 

Mwenyekiti wa MAREMA Justin Nyari akizungumza jana mjini Babati alisema lengo la ziara hiyo ni kutembelea machimbo mbalimbali kwa lengo la kukagua usalama migodini, afya na mazingira. 

Nyari alisema pia wataangalia suala zima la tozo na kodi za serikali, matumizi ya baruti, uhai wa leseni, mikataba na vitambulisho wachimbaji wasio rasmi na wanachama wapya.

Makamu Mwenyekiti wa MAREMA, Money Yusuf alisema watakutana na wanachama mbalimbali wa chama hicho wa eneo hilo kwa lengo la kutambua changamoto zao na kuzitatua zile zilizopo ndani ya uwezo wao. 

“Wanachama wetu huwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo tunawafuata kwenye matawi yao kwa ajili ya kuwasikiliza na kuzungumza nao,” alisema Yusuf. 

Katibu wa MAREMA, Tariq James alisema pia watafika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Joseph Joseph Mkirikiti kwa ajili ya kufahamiana naye ili kushirikiana katika kuhudumia wachimbaji. 

James alisema pia watakutana na ofisa madini mkazi wa mkoa huo Godfrey Nyanda ambaye ndiye mlezi wa MAREMA katika eneo hilo. 

Mweka hazina wa MAREMA, Neney Lyimo alisema katika ziara yao watatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo ile yenye migogoro ya wachimbaji na hifadhi za Taifa. 

“Tutafuatilia migogoro ya wachimbaji wa madini ya Green Aventurine wa kijiji cha Sangaiwe na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na wachimbaji wa madini ya Alexander light wa kijiji cha Mayoka na hifadhi ya Ziwa Manyara,” alisema. 

Katibu msaidizi wa MAREMA, Joseph Manga alisema wao kama viongozi wameonelea wasikae ofisini pekee ila wawafuate wanachama kwenye matawi yao mbalimbali. 

“Tukiwa viongozi wa MAREMA ni muhimu kuwafikia wanachama wetu na kusikiliza kero, changamoto na ushauri wao kwenye sekta hii ya madini,” alisema Manga. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...