MFANYABIASHARA, Tariq Machibya (29) maarufu kwa jina la Mr Kuku, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka saba likiwemo la kufanya biashara ya upatu na utakatishaji fedha wa Sh bilioni 17.

Machibya ambaye ni Mkazi wa Oysterbay jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani hapo leo Agosti 10, 2020 mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Katika hati ya mashtaka hayo, iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon imedai katika tarehe tofauti kati ya Januari 2018 na Mei 2020, maeneo ya jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alifanya na kusimamia biashara ya upatu kwa kukusanya fedha toka kwa umma kwa ahadi kwamba zimewekwa kwenye biashara ya kuku na watu wangepata asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 kwa mtaji wa awali uliowekezwa kwa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mtaji uliokusanywa.

Inadaiwa, kati ya Januari 2018 na Mei 2020, katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Machibya alikubali kupokea fedha kutoka kwa umma ambazo ni Sh bilioni 17 bila kuwa na leseni.

Imeendelea kudaiwa kuwa kati ya Aprili 26, 2019 na Januari 26,2020 mshitakiwa Machibya alijihusisha na miamala ya Sh 6,477,297,614.83 kwa kutoa kutoka kwenye akaunti ya CRDB ya Mr Kuku Farmers Ltd huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kusimamia biashara ya upatu.

Pia inadaiwa kati ya Januari 17,2020 na Machi 30,2020  Machibya alijihusisha na miamala ya Sh 629,249,576.36 kwa kutoa fedha hizo katika akaunti ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la biashara ya upatu.

Aidha kati ya Machi 5,2020 na Aprili 17, 2020 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijihusisha na miamala ya 1,366,718,048.46 huku pia akidaiwa kuwa kati ya Januari 17,2020 na Januari 30,2020 huko CRDB Viva tower iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam Machibya alijihusisha na miamala ya USD 107,893.73 na kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya CRDB.

Pia kati ya Machi 3 na 30, mwaka huu huko CRDB Waterfront mshtakiwa alijihusisha na muamala.wa fedha kwa kuingiza USD 146,300 kwenye akaunti ya Mr Kuku Farmers Ltd.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na mashtaka ya utakatishaji hayana dhamana.  

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...