RAIA wawili wa Kenya na Watanzania, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya 11 yakiwemo ya kula njama kusimika mitambo ya mawasiliano bila kibali na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya Sh milioni 16.6.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Agosti 7, 2020 na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi imewataja washtakiwa hao kuwa ni Beth Ngunyi (43) mfanyabiashara na Mkazi wa Kasaram Nairobi, Frolence Dirango (34) mfanyakazi wa Kampuni ya Betlee kama Ofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Alven Swai (26) mkazi wa Mbezi Beach na Godluck Macha (28) mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi beach.

Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa kati ya Julai Mosi na Julai 26, mwaka huu huko katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam washitakiwa kwa pamoja walikula njama ya kutumia vifaa vya mawasiliano.

Imedaiwa Julai 13, mwaka huu maeneo ya Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro washtakiwa Ngunyi na Dirangu waliingiza vifaa vya kielekroniki nchini bila ya kuwa na leseni ya TCRA. Pia washtakiwa hao wanadaiwa kuwa, Julai 20, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walisimika vifaa vya mawasiliano bila kuwa na leseni kutoka TCRA.g

Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Julai 20 na 26, mwaka huu maeneo ya Kibona lodge Mbezi beach, kinyume na sheria walifanyia marekebisho ya vifaa hivyo vya kielektroniki huku pia kinyume na sheria washitakiwa hao waliendesha mitambo ya mawasiliano bila kuwa na leseni.

Imeendelea kudaiwa kuwa, kinyume na sheria Washtakiwa hao walitumia vifaa vya mawasiliano vilivyounganishwa na vifaa vingine vya mawasiliano kwa nia ya kupokea na kusambaza mawasiliano bila kupata uthibitisho wa TCRA na kukwepa kufanya malipo ambayo yalipaswa kufanyika kwa kuruhusu mawasiliano nje ya nchi kutokana na kutumia kifaa hicho cha mawasiliano bila kuwa na leseni.

Katika Katika shtaka la tisa, inadaiwa Julai 13, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge, Mbezi beach, washitakiwa Ngunyi na Dirangu wanadaiwa kuwepo nchini bila kuwa na kibali.Mshitakiwa Macha anadaiwa Julai 15, mwaka huu kinyume na sheria aliwahifadhi Ngunyi na Dirangu kuishi kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wakijua hawana kibali.
Katika shtaka la 11, inadaiwa kati ya Julai 20 na 26, mwaka huu maeneo ya Kibona lodge Mbezi beach jijini Dar es Salaam washitakiwa hao waliisababishia TCRA hasara ya Sh 16,634,400.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali kutoka kwa DPP, Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Agosti 20 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, washitakiwa wote wamerudishwa rumande .
 Picha ya pili watanzania, Alven Swai na Godluck Macha wakitoka kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mara baada ya kumaliza kusomewa kesi yao ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 11 likiwemo la kuisababishia mamlaka ya mawasiliano TCRA hasara ya sh. Milioni 16.6
 washtakiwa Beth Ngunyi na Frolence Dirango wakitoka kizimbani mara baada ya kumaliza kusomewa kesi yao ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 11 likiwemo la kuisababishia mamlaka ya mawasiliano TCRA hasara ya sh. Milioni 16.6

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...