Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Vuta ni kuvute ya Sakata la mkataba wa Winga wa Kimataifa wa Ghana, Bernard Morrison na Klabu ya Yanga limechukua sura mpya baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutotoa hukumu ya kesi hiyo ya mkataba haswa kwa Waandishi wa Habari kwa sababu ambazo hazikutajwa na Mamlaka husika inayosikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo leo August 10, 2020 imefika kusikilizwa TFF ambapo ilitakiwa kutolewa hukumu, mapema asubuhi majira ya Saa nne, Viongozi mbalimbali wa Yanga na Morrison mwenyewe walionekana wakiingia katika Ofisi za TFF kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Waandishi wa Habari, Mashabiki, Wadau wa Soka walikuwa nje ya Ofisi hizo zilizopo Karume jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujua hatma ya kesi hiyo ambayo imechukua sura mpya baada ya Nyota, Morrison kumwaga wino kwa Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ambao ni Watani wa Yanga SC ijapokuwa Yanga kudai kuwa na mkataba na Winga huyo.

Tangu Saa nne asubuhi, Saa Tano, Saa Sita, Saa Saba, Saa Nane, Saa Tisa, hadi Saa 12 jioni, katika kesi hiyo ndani ya Ofisi za TFF mambo yalikuwa magumu, nje kulikosekana taarifa yeyote za humo ndani, kilichobaki ni tetesi tu zilizokuwa zinaendelea kuletwa hapo nje, hususan zile za Mitandaoni na Radioni.

Kwa hakika siku ya leo ilikuwa ngumu, siku ya kufurahisha sana kwa Mashabiki wa Soka haswa Mashabiki wa Simba na Yanga. Kiu yao kubwa ilikuwa kutaka kujua 'Mbivu na Mbichi' kuhusu usajili wa Bernard Morrison ambapo Yanga wanadai bado wana mkataba na Winga huyo, lakini kwa Simba SC wamemsajili kwa kudai hana mkataba na timu yeyote ile hapa nchini.

Suala hili lipo chini ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Mamlaka hiyo inayosimamia Soka nchini, basi hadi inafika Saa 2 Usiku, wale Viongozi wa Yanga na Viongozi wengine sambamba na Morrison walitoka nje kwa maana ya kuondoka kabisa katika eneo hilo la Ofisi za TFF. Kila mtu aliyekuwa eneo hilo alijiuliza kuna nini? nini kimeamuliwa humo? Je Morrison ni wa Yanga au wa Simba?.

Ni swali kila aliyekuwa nje alijiuliza, lakini cha kushangaza Mashabiki wa Soka haswaa wale wa Simba walisikika wakiimba, "Morrison!, Morrison!, Morrion!, Morrison!" kwa sauti kubwa bila hata ya kutolewa hukumu kwa kesi iliyokuwa inasikilizwa humo ndani.

Lakini kwa Mashabiki wa Yanga na wao hawakuwa na unyonge licha ya kuwa na sauti za chini tofauti na Mashabiki wa Simba, sina maana ya kuwa Morrison ni rasmi Mchezaji wa Simba, naeleza hali halisi iliyokuwa nje ya Ofisi hizo za TFF jioni ya leo, Yanga walisikika mara chache wakimtaja Senzo Mbatha kama Kiongozi wao mpya.

Hao Mashabiki wa Simba walikuwa wanashangilia tu kwa vile walioneka kuwa wengi nje ya ofisi hizo, Mashabiki wa Yanga wao walipaza sauti kwa Aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha japo ni kidogo kwa sauti za chini lakini walisikika wakijivunia kuwa na Kiongozi huyo shupavu katika Soka.

Hali ilikuwa shwari nje ya viunga vya TFF, licha ya Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi kuhakikisha kuna amani na utulivu kwa waliofika kujua hatma ya kesi hiyo. Ndio zilionekana 'Defenders' za Polisi tunaamini hazikuwa na kazi nyingine bali kuhakikisha amani na utulivu vinatawala. Magari ya Viongozi wa Soka yalikuwa yanapishana tu, "Huyu kaingia, huyu katoka".

Yote kwa yote tusubiri tu, sisi Waandishi wa Habari za Michezo, Wadau wa Soka sio waamuzi wa suala hili maamuzi yapo TFF kupitia Kamati yake  ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, tusubiri tujue Bernard Morrison ni wa Yanga SC au wa Simba SC...???

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...