WAKALA wa Vipimo (WMA) inawakaribisha wananchi wote wa Simiyu, Shinyanga, Mara na Mikoa yote ya karibu kuhudhuria katika maonesho ya sherehe za Wakulima maarufu kama NaneNane, ambayo yanafanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi Mkoani Simiyu. Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo kushiriki katika maonesho hayo ni kuwapa elimu Wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vipimo pamoja na kuwaelezea majukumu ya Wakala wa Vipimo katika sekta mbalimbali hususani ya Kilimo.

Akizungumza na mwandishi wetu katika Viwanja vya Nyakabindi Bw. Deogratias Maneno ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Biashara wa Wakala wa Vipimo, amesema Wananchi watapata manufaa makubwa watakapotembelea banda lao katika viwanja hivyo, miongini mwa manufaa hayo ni pamoja na kujifunza namna sahihi za kufungasha bidhaa hususani za Wajasiriamali kwa kutumia vipimo sahihi na kuandika alama kwa usahihi katika kifungashio kwa lengo la kuongeza thamani za bidhaa wanazozalisha. 

Aidha, amesema kuwa, kwakuwa mikoa ya kanda ya ziwa Wakulima bado wanaendelea na zoezi la kuuza Pamba katika vituo mbalimbali vilivyothibitishwa, Wakala wa Vipimo inatoa elimu ya utambuzi wa mizani sahihi iliyohakikiwa kwa kutumia mifano ya mizani iliyoidhinishwa kununulia zao la Pamba. Mizani sahihi iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na kupitishwa kwa matumizi hufungwa lakiri (seal) ambayo huonyesha alama ya Ngao ya Taifa (Bibi na Bwana) na tarakimu mbili za mwisho za mwaka husika mfano “20” ikiwakilisha mwaka 2020. Pia mizani iliyohakikiwa huwekewa stika maalumu ya Wakala wa Vipimo.

Pamoja na maelezo hayo Bw. Maneno amesema upande wa suala la uharibu wa Mizani katika Ununuzi wa Pamba umepungua sana katika siku za hivi karibuni ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Amesema moja ya sababu zilizochangia kushuka kwa matukio hayo ni kuimarishwa kwa utendaji wa Ushirika, ambapo ununuzi hufanyikia katika Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na hupata ushirikiano mzuri toka kwa Viongozi wa Vyama hivyo. Ameishukuru Serikali kwa kuweza kurahisisha utekeleza wa majukumu yao kwa kuanzishwa kwa mfumo huo mzuri na ameshauri mfumo huo uimarishwe na kutumika katika mazao mengine. 

Pia, Bw Maneno ameshauri Uongozi wa Ushirika kuona uwezekano wa kuhakikisha kila Chama cha Msingi cha Ushirika kina kuwa na Mawe Maalum yaliyo hakikiwa na Wakala wa Vipimo ili kuhakiki mzani yao kila siku kabla ya kuanza kwa zoezi la ununuzi wa Pamba. 

Bw. Maneno ameendelea kusema kuwa, kwa sasa Wakala wa Vipimo inafanya pia uhakiki wa Dira za Maji, hivyo wananchi watembeleapo banda lao watapata fursa ya kujifunza namna ya kutambua Dira za Maji ambazo zimehakikiwa na kufungwa lakiri ya Wakala wa Vipimo. Zoezi hilo linalenga kuhakikisha kunakuwa na biashara ya haki kati ya Mteja na Mamlaka za Maji, ambapo Mamlaka za maji zitatoza fedha kwa usahihi kulingana na matumizi ya wateja wao.

Aidha, katika Maonyesho hayo amesema, Wakala wa Vipimo inaonyesha namna ya utambuzi wa mizani sahihi iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo inayotumika katika ununuzi wa Vito na Madini. Zoezi hilo linakwenda sambamba katika kufanikisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha Wananchi wake wanafaidika na Vito na Madini yanayopatikana hapa nchini.

Bw. Maneno amewataka wafanyabiashara kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa kwani adhabu zitolewazo kwa wakiukaji wa Sheria ya vipimo ni kali. Kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Vipimo Sura na. 340 na mapitio yake, endapo Mtu yeyote atabainika kutenda kosa kinyume na Sheria hiyo na akakiri kutenda kosa husika, atapaswa kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi milioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa la kwanza Na endapo mtuhumiwa atakataa kukiri kosa na kufikishwa Mahakamani kwa kosa hilo, na akabainika kutenda kosa hilo, atatozwa faini isiyopungua Shillingi laki tatu (300,000/=) na isiyozidi shilingi million hamsini (50,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja. Aidha, endapo mtuhumiwa atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na hatia, adhabu ni faini isiyopungua Shillingi laki tano (500,000/=) na isiyozidi shilingi millioni mia moja (100,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.

Kwa kumalizia Bw. Deogratius Maneno amewataka wananchi kutokuwa waoga wa kutoa taarifa zitakazo wafichua wale wote wanaojihusisha na uchezeaji / uharibifu wa Vipimo katika sekta mbalimbali kwa lengo la /kuwapunja/kuwaibia wanunuzi/wauzaji wa bidhaa mbalimbali. Taarifa hizi zitolewe kupitia ofisi zao zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara au kupitia namba yao ya simu ya bure ambayo ni 0800 11 00 97 ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara Bw. Deogratias Maneno akitoa elimu kwa mdau alietembelea banda la Wakala wa Vipimo katika maonesho ya NaneNane Bariadi Mkoani Simiyu.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo Shinyanga Bw. Hilolimus Mahundi akitoa elimu kwa Wanafunzi kuhusu uhakiki wa bidhaa zilizofungashwa.
Kaimu meneja Wakala wa Vipimo Simiyu Bw. Tuntufye Mkumbwa akitoa elimu kwa wadau kuhusu matumizi ya Vipimo sahihi katika maonesho ya NaneNane Bariadi Simiyu.
Dira ya maji iliyohakikiwa na kufungwa lakiri (seal) ya Wakala wa Vipimo.
Mizani ya digitali iliyohakikiwa na kufungwa lakiri (seal) na kubandikiwa stika maalum ya Wakala wa Vipimo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...