Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Morogoro

HALMASHAURI ya Wilaya ya Morogoro imesema kuwepo kwa mradi wa mkaa endelevu katika baadhi ya vijiji vilivyopo katika wilaya hiyo kumeleta faida kubwa ya maendeleo ya wananchi.

Kutokana na maendeleo ambayo Wilaya pamoja na wananchi hao imeyapata kutokana na mradi huo wa mkaa endelevu, mkakati ulioko ni kuwepo kwa mradi wa aina hiyo katika vijiji vingine hasa kwa kuzingatia Wilaya ya Morogoro imejaaliwa kuwa na eneo kubwa la misitu ya asili.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi wakati akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini pamoja na maofisa wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) ambao wapo katika ziara ya kimafunzo kuangalia mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwepo wa Mradi wa mkaa endelevu.

"Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania limejikita zaidi katika uhifadhi wa misitu ya asili, shirika hili linafanya kazi pamoja na halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro hasa katika mchakato mzima wa ushiriki wa wananchi katika mkaa endelevu.

"Kama mnavyofahamu halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro imebarikiwa kuwa na misitu mingi ya asili , na misitu hii kwa kiasi kikubwa iko chini ya uhifadhi lakini vile vile inamilikiwa na vijiji, kwa hiyo nichukue fursa hii kulishukuru shirika hili la uhifadhi wa misitu ya asili Tanzania,wameweza kushirikiana na halmashauri yetu na vijiji vyetu vitano.

"Katika kuimarisha na kuzalisha mkaa asili ,kama tunavyofahamu shirika hili uwepo wake katika halmashauri yetu umeweza kutengeneza tija kubwa kwa halmashauri na wananchi wa vijiji ambavyo vinafanya kazi na shirika hili. Mbali na uhifadhi wa asili kama shirika lenyewe dhima yake, lakini uwepo wa shughuli hiyo ya mkaa endelevu katika halmashauri yetu kumeleta maendeleo makubwa sana kwa wananchi wetu,"amesema.

Ameongeza kwanza wanaona uhifadhi wa misitu umeimarika kwani kuwepo kwa mradi wa mkaa endelevu kumewezesha uhifadhi lakini kupatikana kwa mkaa ambapo hiyo wameona imebadilisha hali ya maisha ya wananchi wao.

"Kwa kweli haijawahi kutokea kuwepo na mkaa endelevu katika halmashauri yetu, vijiji hivyo vitano vimeweza kujipatia fedha nyingi sana , kwa mfano kijiji kimoja kimepata zaidi ya shilingi milioni 100, ni kitu ambacho kwa kweli hakijawahi kutokea miaka yote ya nyuma.

"Hivyo kuwepo na shughuli ya uzalishaji mkaa endelevu kumepanua wigo mkubwa, kwanza kujikusanyia mapato ya kutosha, ambapo mapato hayo yapo chini ya vijiji ambavyo vinatekeleza mradi huo.Pia kumekuwepo na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umesaidia kutengeneza wigo wa kuandaa mipango bora ya matumizi ya ardhi.

"Kwa hiyo pia imetoa fursa kwa wananchi ya kuwawezesha kuwa na mipango mikakati ya kuona kwamba ardhi sasa inamipango bora ambayo inatumika kwa ajili ya kilimo , ufugaji na mambo mengine ya maendeleo,"amesema.

Wakati kwa wananchi amesema wamekuwa mstari wa mbele kuchagia maendeleo kutokana na fedha ambayo wanaipatikana kutokana na shughuli za mkaa endelevu."Tumeona hata ukiangalia vijiji ambavyo vinatekeleza mradi huo kumekuwepo na ujenzi wa madarasa, kuimarisha madarasa, kujenga zahanati na maabara na mambo mengine.

"Kwa hiyo tunaona uwepo wa mkaa endelevu umeweza kujenga mazingira ya wananchi kusimama wenyewe na kuweza kutumia fedha wanazopata kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe .Kwa kweli mimi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro nichukue fursa hii kubwa na ya pekee kushukuru wenzetu wa TFCG kwa jinsi wanavyoshirikiama na wananchi kutoa mradi wa mkaa endelevu ambapo sasa tuaona mafanikio yake,"amesema.

Hata hivyo amesema wao kama halmashauri kazi yao sasa ni kusimamia kwa ukaribu zaidi mradi huo ili uwe endelevu na wanachokifanya wamekuwa wakituma watalaam wa maendeleo ya jamii kukutana na wananchi kuwapa elimu zaidi.Pia wametoa mkaguzi wa ndani kwenda katika vijiji kila wakati kukagua kuona matumizi sahihi ya hizo fedha jinsi zinavyotumika.

"Tunalo jukumu kubwa la kusimamia huu mradi, ili uwe endelevu, lakini mradi huo baada ya kukabidhiwa kwetu 2019, halmashauri imejipanga kuanzisha vijiji vingine ili kuendeleza kile ambacho tumekipata , hivyo kwa kushirikiana na ofisa wa Mali asili tumeandaa mpango mkakati wa kuona ni namna gani tunaweza kutenga vijiji vitano vingine ili viwe katika mradi.
"Kwa hiyo ni imani yangu mpango huo utakapokamilika utakuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na hatimaye tutakuja kueleza mafanikio ambayo wananchi wameyapata kwa kuwepo kwa mradi huo,"amesema.

Kwa upande wa wananchi wa vijiji ambavyo wamenufaika na mradi huo pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali wameeleza namna ambavyo uwepo wa mradi huo wa mkaa endelevu ambavyo umebadilisha maisha yao kwani wamefanya maendeleo makubwa ya vijiji vyao na wao wenyewe kwa ujumla


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehama Bwasi (kulia) akipokea majarida yanayohusu shughuli mbalimbali za mradi zinazofanywa na Shirika la Usimamizi wa Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) kutoka kwa Ofisa Uhusiano wa shirika hilo Bettie Luwuge(kushoto) baada ya kufika ofisini kwa Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehama Bwasi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akielezea mafaniko ambayo yamepatikana kutokana na uwepo wa mradi wa mkaa endelevu katika vijiji vitano vilivyopo kwenye halmashauri hiyo.
 Ofisa Uhusiano wa shirika la TFCG Bettie Luwuge(kushoto) na Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA Elida Fundi(kulia) wakichukua kumbukumbu ya picha ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Ofisa Uhusiano wa shirika la TFCG Bettie Luwuge akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi.
 Waida Salim ambaye ni Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro akitoa maelekezo kwa maofisa wa TFCG na MJUMITA baada ya kutoka katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo.
 Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro Waida Salim akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mradi wa mkaa endelevu ambao umetekelezwa kwenye vijiji vitano vya halmashauri hiyo.
 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Matuli wakiwa kwenye kikao cha kujadili mafanikio na changamoto za mradi wa mkaa endelevu kwenye kijiji chao.
 Mmoja ya watendaji wa Kata ya Matuli akizungumza jambo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...