Na Said Mwishehe, Michuzi Tv-Kaliua

MAELFU ya wananchi wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wamejitokeza katika mkutano wa kampeni za Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Dk.John Magufuli ambaye ameingia katika mkoa huo       leo akitokea Mkoa wa Kigoma.

Baada ya kufika Mkoa wa Tabora, Dk.Magufuli amepata fursa ya kuzungumza na wananchi wa Wilaya ya Kaliua ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuwaomba kura ili aweze kushinda tena kiti cha urais aendelee kuwatumika katika kuwaletea maendeleo.

Akizungumza zaidi na wananchi hao wa Kaliua leo Septemba 20, mwaka 2020, Dk.Magufuli amewaomba pia wachague wabunge na madiwani kutoka CCM ili kuwa na sauti ya pamoja katika kuleta maendeleo huku akiwakumbusha mwaka 2015 walimchagua yeye kwa kura nyingi lakini kwa nafasi ya mbunge walichagua upinzani,hivyo kusababisha kukwamisha maendeleo.

"Uchaguzi mkuu mwaka huu nawaomba wananchi msifanye tena makosa, nichagueni mimi kwa nafasi ya urais kwa kura nyingi, chagueni mbunge na madiwani wa CCM. Mkinichagua mimi tu halafu mkanichangia mbunge kutoka kwingine mtanitia unyonge hata wa kufanya yale niliyopanga kuyafanya kwa ajili ya wananchi wa Kaliua.,"amesema Dk.Magufuli.

Akizungumza zaidi na wananchi hao, Dk.Magufuli ambaye ameendelea kuchanja mbuga kwa kuendelea kusaka kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, amesema tangu ametoka Kigoma njiani watu wamejaa, lakini pamoja na kuchelewa kwake bado wananchi wa Kaliua waliendelea kumsubiri tena kwa wingi.

Wakati huo huo Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa mwaka 2015 wakati amekwenda kwa wananchi hao kuomba ridhaa ya kuwa Rais, kuna mambo aliyokuwa ameahidi yakiwemo ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami Kaliua Mjini yenye urefu wa kilometa tano.

"Hapa Kaliua kwenye wakati wa kampeni mwaka 2015 niliahidi kujenga kilometa tano za barabara za lami , na tayari tumejenga kilometa mbili, zile nyingine ambazo zimebaki nitajenga.Nafahamu tulipanga kuboresha barabara inayotoka Mpanda ,Ugala , Kaliua mpaka Kahama yenye urefu wa kilometa 428.

"Barabara hiyo imetajwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, mimi nataka kuwaambia tutaendelea kushughulikia yale yote ambayo yameahidiwa kwenye Ilani ya uchaguzi kwani ndio mkataba kati yetu sisi na wananchi.Ilani ya Uchaguzi Mkuu ina mambo mengi,inakurasa  303, mambo ni mengi lakini tutashughulikia ,"amesema.

Dk.Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano wamejitahidi kuboresha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kaliua na hasa katika hasa kwenye maeneo ya vijiji.Pa wamekarabati visima vingine katika vijiji vinne vipatavyo 60.

"Hapa Kaliua Mjini bado kuna shida ya maji kwani hayatoshi, nataka kuwaahidi hapa leo tumefikisha maji Tabora, tutayavuta kutoka Tabora, Urambo mkapa Kaliua kwani uwezo huo tunao, hivyo tunaomba msituangushe, maana ninyi wakazi wa Kaliua mnabadilika.

"Nataka kuweleza ukweli hata hii lami asingekuwa Profesa Juma Kapuya isingekuwepo, nataka kuwaeleza ukweli, hii barabara aliiomba Kapuya ambaye alikuwa Waziri mwenzangu , chini ya utawala wa Mkapa , akiwa Waziri wa Elimu, mimi nilikuwa Waziri wa Ujenzi.

"Kapuya ni kaka yangu, namfahamu sana, akaniomba anataka barabara ya lami, nataka kueleza historia maana itabaki hivyo hivyo, na ndio maana nikaianzisha Kaliua,"amesema Dk.Magufuli mbele ya wananchi wa Kaliua .

Pia amesema ili kuendelea kujenga barabara za lami ameomba wananchi kumchagua mbunge wa CCM kwani mwaka 2015 aliwaomba wamchague mbunge wa CCM, lakini wananchi wakachagua upinzani."Sikulalamika ndio demokrasia lakini demokrasia yenye machungu haileti raha.Mwaka huu tumekuja tena , Mji wa Kaliua umebadilika, umekuwa na maendeleo, umejengeka na ni kwasababu ya uwepo wa barabara ya lami.Umeme umefika lakini kuna maeneo bado hatujaanza kuusambaza. Katika suala la maji tumeanza ingawa halijaenda kila mahali".

Katika hatua nyinine Dk.Magufuli amewaambia wananchi hao katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM walijitokeza wana CCM wengi na miongoni mwao alikuwepo Profesa Kapuya na aliongoza katika kura za maoni lakini jina lake halikupitishwa.

"Kapuya ndio aliyeongoza kwenye kura, na Kapuya ni rafiki yangu, ni kaka yangu.Katika mchakato huo alikuwepo pia Aloyce Kwezi  ambaye katika miaka mitano iliyopita nilimteua kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya kilolo. Aliyoyafanya Kilolo ni maajabu, amejenga hospitali ya Wilaya ambayo ni nzuri kuliko hospitali zote za wilaya, ni hospitali ya ghorofa

"Nikamuona huyu kijana ana akili, nataka niwaeleze wana Kaliua, alifufua miradi mpaka akaomba na fedha za kuunganisha barabara ya Kilolo hadi Iringa kwa lami , nilienda kilolo kuifungua.Nikamuuliza kwanini haya usifanye Kaliua kwenye Wilaya ambayo ni yazamani lakini imedorola, akanijibu akienda kuomba kura atanyimwa.

"Nikamwambia nenda ukaombe, ndio maana Kapuya alikuwa wa kwanza na Kwezi alikuwa wa pili walipishana kwa kura  nane, tukaa kwenye vikao vya Chama tukapitisha jina la Kwezi.Kapuya ni kaka yangu , lakini umri nao umeenda.Nikaangalia Kaliua inahitaji mabadiliko , Kaliua inahitaji spidi mpya, ndio maana kwenye Kamati Kuu tukamleta huyu Kwezi , hakujileta kwa makosa, tumemleta kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza ndio maana sasa hata moyo wake umeanza kurudi kiasi cha kutangaza zabuni ya barabara ya Kazilambwa  kwenda Maragalasi nayo itandikwe kwa lami na mkandarasi yupo , hivyo mwaka huu wasimuangushe. "Kaliua mwaka huu msituangushe, unanichagua mimi halafu mbunge na madiwani ni wa chama kingine mtakuwa mmeninyima nguvu mimi,

"Kaliua mnachangamoto nyingi, kuna mambo bado hayajaenda, nikajata hapa changamoto zenu ni nyingi sana, mlihitaji vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya, mlihitaji barabara ya Kaliua Mjini, niliahidi lakini nilikosa wa kunikumbusha, nileteeni mbunge na madiwani wa kunikumbusha, ombi la Mahakama ya wilaya hapa halipo

"Watu wanasafirishwa kwenda kule haki zao wanachelewa kuzipata, sasa niweze kujenga mabarabara yote haya nishindwe kujenga Mahakama ya Wilaya , mlihitaji ofisi ya wilaya ya TRA , hii ni wilaya ya  zamani haina jengo la TRA, Gereza la Wilaya Kaliua halipo, hata wakosaji lazima wapelekwe kwenye wilaya nyingine.Changamoto  ziko nyingi , uhaba wa watumishi wa afya wa wilaya zima, amekosekana mtu wa kwenda kumkumbusha Waziri wa Afya, juzi tumeajiri watumishi wa afya 1,000 lakini amekosekana wa kumkumbusha, hakuna aliyekwenda kuomba.

"Barabara nyingi  za vijijini nyingi hazipitiki, wakati tunazo fedha za mfuko wa barabara ambazo zinatakiwa kutengeneza zile barabara, kuna ombi la ujenzi wa barabara inayounganisha Wilaya ya Kaliua na Mkoa wa Katavi kilometa 423 , mnahitaji mtu wa kupiga hodi kweli na tunayeweza kuzungumza la lugha moja, akisema CCM hoyee na mimi nasema CCM hoyee,"amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza Kaliua kuna uhaba wa masoko  ya pamba na tumbaku, ndio maana leo amemleta Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe lakini lazima apate kiunganishi.

"Mnachangamoto ya barabara ya Ugasa Shuleni hadi Kituo cha Afya Usinge, ucheleweshaji pembejeo za kilimo na mengine mengi. Kaliua ndio maana nisimama kuomba kura, tugange yajayo, tunataka kufanya ukarabati wa barabara ya lami kutoka Kaliua hadi Mpanda, watu wafanye biashara, na hata hii reli ya hapa iko katika mpango wa kuijenga kwa kiwango cha reli ya kisasa ili iende mwendo kasi,"amesema Dk.Magufuli.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...