WAZAZI/WALEZI WAASWA KUWA KUWAPELEKA WATOTO KATIKA VITUO VYA AFYA ILI KUPATA CHANJO KWA WAKATI

Na Avila Kakingo, Globu ya Jamii
IMETHIBITIKA kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo vya watoto, hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia na Taifa kwa ujumla ingetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Hayo ameyasema Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Ayoub Kibao wakati akizungumza na waandishi wa habari katika semina fupi iliyofanyika katika Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam Septemba 25,2020. Amesema kuwa Magonjwa yanayolengwa na Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa sasa ni Kifua Kikuu, Dondakoo, Kifaduro, Polio, Surua, Rubella, Pepopunda, homa ya ini, homa ya uti mgongo, kichomi, kuhara na Saratani ya mlango wa kizazi.

Dkt. Kibao amesema kuwa rejea za kitaaluma zimethibitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo million 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani. 

"Hapa nchini mafanikio ya chanjo ni dhahiri, kwa mfano tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Ndui, magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Polio na Pepopunda yamedhibitiwa na wodi za surua zimefungwa." Amesema Dkt. Kibao

Hata hivyo Dkt. Kibao amesema kuwa Mafanikio haya makubwa yametokana na kufanikiwa kuwapatia chanjo zaidi ya asimilia 80 ya watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja hapa nchini.

"Serikali kwa kushirikiana wa wadau wetu imewezesha upatikana wa Chanjo zote za kuzuia magonjwa niliyoyataja hapo juu, na kwa takwimu za mwaka 2018/2019, Tanzania imefikia kiwango cha uchanjaji kwa asimilia 99. Hii ni hatua kubwa sana iliyofikiwa na Serikali ya awamu ya Tano katika kupambana na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo." Amesema Dkt. Kibao

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya 5 chini ya Mhe. Raisi Dkt. John Pombe Magufuri kwa kushirikiana na shirika la Gavi, na wadau wengine wa Maendeleo, imefanikiwa kununua jumla ya magari 74, fork lift 3 na jenerata 1 vyote vikiwa na thamani ya shilingi Bilioni 7,759,302,831 kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo hapa nchini. Kati ya magari 74 yaliyonunuliwa, magari 61 ni aina ya Toyota Pick Up (kila gari moja likiwa na thamani ya shilingi milioni 56.6), ni kwa ajili ya kuimarisha usambazaji wa chanjo katika halmashauri 61 hapa nchini, na magari mengine yakiwemo malori ya ubaridi 3, malori 2 na magari mengine 8 ni kwa ajili ya Mpango wa Taifa wa chanjo kuanza shughuli za usambazaji wa Chanjo kutoka stoo ya Taifa hadi stoo za chanjo za Mikoa.Vile vile Wizara imeanza kukusanya na kutunza takwimu kwa njiaya mfumo kutumia Vishikwambi (tablets).

Kununuliwa magari haya ni juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali katika kuhahakisha kuwa chanjo zinasambazwa kwa wakati na kuwafikia walengwa wote hapa nchini.

Wizara imetoa huduma za chanjo kuwa kipaumbele cha kwanza katika Afya. Hivyo, Serikali inafanya kila iwezalo kuhakikisha Chanjo zinapatikana kwa wakati katika vituo vyote vinavyotoa huduma za chanjo hapa nchini.

"Serikali ya awamu ya 5 imedhamiria kuwa kila Halmashauri hapa nchini inakuwa na gari la kusambaza chanjo. Kwa kipindi cha 2012 hadi 2015 jumla ya halmashauri 78 zilipatiwa magari ya kusambazia chanjo, na mwaka 2019 Serikali ilitoa magari 61 katika halmashauri nyingine. Na mpaka kufikia mwaka 2021/2022, halmashauri zote zilizobaki nchini zitakuwa zimepatiwa magari ya chanjo."Amesema Dkt. Kibao.

Hata hivyo Dkt. Kibao amewahimiza wazazi, walezi na familia kuwapeleka watoto wanaostahili kupata chanjo vituoni ili wapate chanjo stahiki kwa ratiba iliyopangwa ili kila mmoja wetu ahakikishe mtoto wake, mtoto wa jirani au mtoto yeyote yule anapewa haki ya kupata chanjo ili asiwe hatari kwa wengine kwa kusababisha milipuko ya magojwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...