Na Karama Kenyunko Michuzi TV

 MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi imemuhukumu mfanyabiashara Said Malikita kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.

Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Lilian Mashaka wa mahakama hiyo Septemba 18, 2020.

 Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mashaka amesema, upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake nane waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi na vielelezo vitano vilivyowasilishwa wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa.

"Baada ya kuchambua ushahidi, upande wa Jamuhuri, wameweza kuthibitisha kesi bila kuacha shaka hivyo mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela". Amesema Jaji Mashaka

 Mapema kabla ya kusomwa adhabu hiyo, Jaji Mashaka aliuliza upande wa Jamuhuri kama walikuwa na lolote la kusema ambapo wakili wa serikali Constantine Kakula alisema hawana  kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa ila ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo kwani vitendo vya makosa ya dawa za kulevya vimekithiri katika jamii.

Aidha mshtakiwa katika utetezi wake ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ana watoto wadogo ambao bado hawajaenda shule, ana wazazi wanaomtegemea, baba yake ni mzee wa miaka 84 na mama yake licha ya kuwa ni mzee pia ni mgonjwa sana na hajamuona tangia alipoingia gerezani 2017.

Mbali na wakili Kakula wakili wa serikali  mwingine aliyeendesha kesi hiyo ni Batilda Mushi huku mshtakiwa akitetewa na wakili Abrahamu Senguji.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Agosti 29,2017 huko katika mtaa wa Ufipa eneo la  Kinondoni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na gramu 238.4 za dawa za kulevya  aina ha Heroine Hydrochloride .



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...