Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Tabora

MGOMBEA urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli amesema kuna wagombea wengine wamekuwa wakisema kwamba wakipewa nchi wataanzisha mfumo wa kuigawa nchini katika Serikali za majimbo, jambo ambalo ni hatari na dhambi kubwa.

Dk.Magufuli amesema siasa za kuwagawa Watanzania ni hatari na watu wa aina hiyo wasipewe nafasi kwani tangu kuanzishwa kwa Taifa la Tanzania waasisi wake wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wamekuwa wakihimiza umoja na mshikamano na asitokee mtu wa kutugawa.

Akizungumza leo mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Tabora, Dk.John Magufuli akiwa kwenye mkutano wake wa kampeni pamoja na mambo mengine amesema amesikia wagombea wengine wanataka kuanzisha Serikali za majimbo, hiyo ni dhambi kubwa kwani baba wa Taifa alipoanzisha taifa hili hakutaka kuwagawa watanzania, aliwaunganisha.

"Hapa Tabora kuna mradi mkubwa wa maji ambao umegharimu zaidi ya Sh.bilioni 600 ambapo maji yametoka Ziwa Victoria kuja hapa Tabora, fedha hizi hazikutolewa na Mkoa wa Tabora peke yake bali ni fedha za maeneo yote ndio yamefanikisha mradi huu ambao umekamilika kwa asilimia 92.

"Ninawaomba tusije kujaribu kupewa matumaini ya utawala ambayo baba wa Taifa alikataa, fedha ambazo zimeletwa kwa ajili ya maji ni nyingi hapa Tabora, kuna barabara nyingi za lami zilizojengwa Tabora, hata watu wa maeneo mengine wamechangia, ulizeni mataifa yaliyo na majimbo.

"Watanzania tusikubali kuwa na wanasiasa ambao nia yao ni kutaka kuligawa Taifa letu, huu ni wakati wa kuungana na kuwa wamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,"amesema Dk.Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi hao wa Tabora ambapo amewataka kuwa makini na kauli za wanasiasa kwani kipndi hiki cha kampeni yatasikika mengi.

Kwa upande mwingine Dk.Magufuli amezungumzia suala la vitambulisho vya wafanyabishara wadogowadogo wa Mkoa wa Tabora baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi ya wanaohusika na vitambulisho hivyo wamekuwa wakiwasumbua wafanyabiashara ambapo amesema vitambulisho hivyo havitolewi kwa kuzalimishwa.

"Ni lazima itolewe elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa mfanyabishara kuwa na kitambulisho hicho ambacho kwa mwaka analipia Sh.20,000 ili anayekuwa nacho aweze kufanyabiashara mahali kokote.Tunatoa vitambulisho ili wafanyabiashara wasisumbuliwe , vitambulisho haviwezi kutafutwa kwa bunduki.

"Vitambulisho mtu anakata mwenyewe, akishakata usilazimishe na anayemkorogea uji naye awe na kitambulisho.Mkuu wa Wilaya ya hapa akashughulikie, ukishakuwa na kitambulisho utafanya mwaka mzima, kama hutaki utakutana na mgambo, watamwaga uji wako, watakufuza usifanye biashara.

"Wapinzani wanasema kuhusu hivi vitambulisho.Hakuna mahali hawalipi kodi, tulianzisha vitambulisho hivi, ndio maana tukasema katika kulinda vijana , wajasiriamali wadogo watakuwa wanalipa Sh.20,000,"amesema Dk.Magufuli.

Amefafanua wapinzani wao wamekuwa wakisema kuwa wakichaguliwa watafuta kodi, wakati kodi ndio inayoleta maendeleo maana kile ambacho kinakusanywa ndicho kinakwenda kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali.Serikali haina shamba, hivi fedha vidogo vidogo, tunavyokusanya kwenye madini, utalii na maeneo mengine ndizo ambazo tunapeleka katika maendeleo."

 Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni nwenyekiti wa Chama hicho Tawala na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John. Pombe Magufuli akiwasili katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi

mjini  Tabora kuhutubia mkutano wa hadhara wa kampeni leo Jumatatu Septemba 21, 2020

 

  Umati uliojitokeza kumsikiliza mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni nwenyekiti wa Chama hicho Tawala na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John. Pombe Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi leo Jumatatu Septemba 21, 2020

Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni nwenyekiti wa Chama hicho Tawala na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John. Pombe Magufuli akihutubia maelfu kwa maelfu ya Wananchi
waliofurika kumsikiliza akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini  Tabora leo Jumatatu Septemba 21, 2020

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...