Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Itigi

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amewaahidi wananchi wa Tarafa wa Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida kwamba yote aliyoahidi kwa ajili ya maendeleo yao atayatekeleza.

Akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika leo Septemba 22, 2020 Dk.Magufuli amesema miaka mitano iliyopita alifika kwa wananchi hao kuwaomba kura na kwamba katika kipindi chote hicho wamejitahidi kama Serikali, katika kutoa huduma bila kuwabagua, bila kuwagawa.

"Na hilo ndilo lilikuwa lengo letu na ndio misingi iliyoachwa na baba wa taifa hili aliyepigania taifa hadi kuweza kupata Uhuru, leo tumekuja kuomba kura, najua yako mengi na nisengependa kuyarudia yote, ninyi mnayajua.

"Ninyi hapa ni mashahidi, tumejenga vituo viwili vya afya, mmeeleza mnataka Kituo cha afya cha hapa kiwe na hadhi ya hospitali ya wilaya, nimekubali, ushahidi unatosha hawa watu wote huwezi wakawa wanasubiri waende Manyoni au Singida.Bahati nzuri Katibu Mkuu Wizara ya Afya hii ndio ahadi ambayo nimeitoa leo, hospitali hii iwekewe hadhi ya kuwa hospitali Wilaya badala ya kituo cha afya kwasababu inahudumia watu wengi,"amesema

Wakati huo huo Dk.Magufuli amesema kuwa tarafa hiyo ya Itigi inaelekea kuwa Wilaya kwani muelekeo unaonekana na ndio maana ni tarafa yenye hadhi ya halmashauri.

"Lakini kikubwa tunaangalia na kujipanga vizuri uwezo wa Serikali na ndio maana tumejenga jengo moja hapa nzuri la makao makuu ya Halmshauri yenu tuko kwenye muelekezo mzuri ambao hata ninyi mnautamani,"amesema.

Katika elimu ,Dk.Magufuli amesema wametumia takribani Sh.bilioni 4.79 kutekeleza miradi ya elimu na kiasi cha Sh.bilioni 2.27 zimetumika kutoa elimu bila malipo."Tumeleta takriban Sh.bilioni 2.84 kutekeleza miradi ya maji, iliyopo Itigi.

"Tumefikisha pia umeme kwenye vijiji mbalimbali ndani ya Itigi , lakini nafafahamu bado vijiji vingine havijapata uememe na kuna baadhi ya maeneo bado hajayapata umeme wa kutosha na bahati nzuri yote yameelekezwa kwenye Ilani ya uchaguzi,tumejipanga vizuri , wakati tunaingia madarakani vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2018 lakini miaka mitano tumepeleka umeme katika vijiji 9700 hadi takwimu za jana, vimebaki vijiji 2500, kama tumeweza kupeleka kote huko hatutashindwa Itigi,"amesema

Amesisitiza "Naomba mtuamini ndugu zangu wa Itigi , tutaweka umeme katika vijiji vyote nchini na Ilani ya uchaguzi hii inatuelekeza kila kijiji Tanzania lazima kiwe kimefikiwa na umeme na ndio maana tunao mradi mkubwa wa umeme wa bwawa la mwalimu nyerere.

"Ambapo umeme wake utakwenda kuunganishwa kwenye gridi ya taifa , Manyoni na maeneo mengine ya Tanzania na umeme utakaobaki utauzwa katika nchi nyingine."

Kuhusu miundombinu Dk.Magufuli amesema kuwa waliahidi kukamilisha ya barabara ya kutoka Itigi, Rungwa na kuunganishwa Chunya hadi Makongorosi, itengeneze kwa lami na kwamba ahadi iko pale pale."Zilitangazwa tenda hapa na zilipotangazwa zilikuwa za kifisadi gharama zilikuwa kubwa.Nataka kueleza ukweli lakini ahadi iko pale pale.

"Nawakati tukijipanga hivyo kulikuwa na kipande cha kilometa 85 kati ya Chanya na kwenda Tabora, tulimaliza hizi kilometa za mwanzo, Tabora ilikuwa bado kilometa 85 , tukasema ili Itigi iweze kuunganika vizuri na mikoa mingine tusibakize vipande tulianza na kipande kile tumetumia Sh.bilioni 117 na mkandarasi anaendelea kumalizia, zimebaki kilometa 28.

"Imeshafika ya Itigi, kule Makongorosi kilometa 50 na wale ambao wametoka Chunya tulianza Mbeya kwenda Chunya na tukatoka Chunya kwenda Makongorosi, sasa tunatoka Makongorosi kuja huku Itigi. Nataka kuahdi tutaaanzia hapa Itigi,"amesema Dk.Magufuli.

Ameongeza kuwa kwa hiyo wataweka makandarasi wengi kama walivyoweka Tabora hadi Mpanda yenye jumla ya kilometa 359."Kwa hiyo Itigi nayo tutaichafua kwa lami, msiwe na wasiwasi na ahadi yangu ya mjini ilikuwa kilometa nane na sasa itakuwa kilometa 10 pamoja na hii barabara niliyokuja nayo.Nataka niseme ukweli, ninasema si kwasababu ya kutafuta kura bali ninasema kwasababu nataka kuwambia ukweli.

"Hii ni haki yenu, huu mji umependeza sana, mmejenga nyumba nzuri, nami nataka kuwaahidi ukweli.Mkuu wa Mkoa wa Singida hili ndilo liwe la kwanza kushughughulikia, Meneja wa Taroads Mkoa na Meneja wa Tarura nataka mkae hapa, mchague baadhi ya barabara ambazo zitatosha kilometa 10 za hapa mjini mtandaze lami.

"Tangaza tenda mwezi huu, usiulize nitatoa pesa wapi? mimi bado ni Rais, kwa hiyo mjulishe na Waziri wa Ujenzi, ili kazi ianze mara moja,na hii sio hongo, tangaza tenda ya ujenzi wa barabara za mjini za kilometa 10,"amesema.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...