Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa jimbo la Itilima, katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika Kata ya Ligangabilili, wilayani Itilima. 
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa jimbo la Itilima, wakati akiwasili katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika Kata ya Ligangabilili, wilayani Itilima. 

************************************* 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 3.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika wilaya ya Busega. 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Septemba 18, 2020) kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Mkula na Lamadi, wilaya ya Busega, mkoani Simiyu wakati akiwa njiani kuelekea wilayani Bunda, mkoani Mara. 

Mheshimiwa Majaliwa amesema fedha hizo zimetumika kujenga mradi wa maji bomba katika kijiji cha Lukungu ambao tayari umekamilika. “Pia fedha hizo zilitumika kufanya ukarabati wa chanzo cha maji katika mradi wa maji wa Kalemela-Mkula ambao nao tayari umekamilika.” 

Ameitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa maji bomba Kiloleli unaohudumia vijiji vitatu vya Ihale, Ijitu na Yitwimila B ambao pia umekamilika. 

Amesema fedha hizo zimetumika kufanya upanuzi wa mradi wa maji Lamadi (Kalago na Mwabayanda) ambao umefikia asilimia 50; upanuzi wa mradi wa maji Nyashimo ambao umefikia asilimia 10; ujenzi wa mradi wa maji Mkula sekondari ambao umefikia asilimia 60 na mradi wa maji Bushgwamhala ambao umefikia asilimia 100. 

Kuhusu umeme, Mheshimiwa Majaliwa amesema kati ya vijiji 59, vijiji 53 vimeshapelekewa huduma ya umeme, na vijiji sita bado havina umeme. Amesema vijiji ambavyo havina umeme, vipo kwenye mpango wa kupelekewa umeme 

Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo mpya, sh. bilioni 2.3 zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. 

Amesema fedha zilizotolewa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara zilihusisha barabara za Mwamanyili – Busami; Masanza Sec. School – Sayaka Road; Nyamikoma – Busega na Lamadi Sec.School – Suti Moja. 

Amezitaja barabara nyingine kuwa ni Masanja-Ashico Petroli Road; Malili- Mwamigongwa-Ng’wang’wenge; Nyang’haya-Kasoli na Ngong’ho-Ndono Petrol Station. 

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alitumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Busega, Bw. Simon Songe na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Busega licha ya kuwa wawili kati yao wamepita bila kupingwa akiwemo mgombea udiwani wa Mkula, Bw. Godfrey Kalango.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...