SHULE 151 za wilaya ya Rorya mkoani Mara zikiwemo 120 za msingi na 31 za sekondari zimenufaika na mpango wa elimu bila malipo uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Shirati kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Obwere, kata ya Mkoma wilayani Rorya, mkoani Mara.

 

Alisema sh. bilioni 3.3 zilitolewa kwa ajili ya shule za msingi 120 za kufanya ukarabati, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu. “Kwa upande wa shule za sekondari, shilingi bilioni 2.5 zilitolewa kwa shule 31 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.”

 

Akielezea uboreshaji wa miundombinu ya shule ulivyofanywa kupitia Mpango wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) ulivyotekelezwa, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.2 zilitolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu kwa shule za msingi.

 

Alizitaja baadhi ya shule za msingi zilizonufaika na mpango huo kuwa ni Mori, Nyanduga, Buchuri, Kondo, Saye, Masonga, Kyaro, Kitembe, Bubombi, Oliyo B, Dagopa, Nyabi, Ratia, Kotwo, Muchirobi, Manyara, Ochuna na Nuamaguku.

 

“Kwa upande wa shule za sekondari, zimetumika shilingi milioni 777.8 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo maabara, madarasa, mabweni na vyoo kwa shule za Bukama, Mirare, Ngasaro, Nyamunga, Buturi, Goribe, Nyathorogo, Nyamtinga na Waningo,” alisema.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mara kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Rorya, Bw. Jafari Chege, mgombea udiwani wa kata ya Mkoma, Bw. Ayoi Musa Sonde na madiwani wengine wa wilaya hiyo.

 

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye sekta ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa alisema vijiji 74 kati ya vijiji 87 vya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya vimepata umeme. Alivitaja vijiji vilivyobaki visivyo na umeme kuwa ni Thabache, Nyabikondo, Nyahera, Bugendi, Burere, Wamaya, Nyabiwe, Masike, Busanga, Nyihara, Kyanyamsana, Nyamusi na Oliyo


IMETOLEWA:

JUMANNE, SEPTEMBA 22, 2020.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...