Na Mwandishi wetu, Simanjiro 
MWENYEKITI wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Development Foundation Peter Toima ambaye hivi karibuni aligombea ubunge kwenye kura za maoni jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, kwa tiketi ya CCM amewataka watia nia wote waliogombea ubunge kumuunga mkono mgombea ubunge Christopher Ole Sendeka ili aweze kuwa mbunge.

Toima akizungumza wakati akikabidhi madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo vya shule ya msingi Loorng'swani Kata ya Terrat ya thamani ya shilingi milioni 62 amesema wagombea wote wa CCM ambao kura zao hazikutosha na hawakuteuliwa wanapaswa kumuunga mkono Ole Sendeka mgombea ubunge aliyepitishwa na CCM. 

Amesema hivi sasa wagombea wanapaswa kuvunja makundi ya awali na kumuunga mkono Ole Sendeka mgombea anayepeperusha bendera ya CCM. 

"Tunatambua mchakato wa CCM ulivyokuwa, kila mtu alikuwa na kundi lake la ushindi, lakini hivi sasa tunapaswa kuwa na kundi moja la CCM pekee na siyo vinginevyo," amesema Toima. 

Amesema endapo waliogombea ubunge kwenye kura za maoni na kura hazikutosha hawatavunja makundi, itakuwa ni makosa kwani watakuwa wanawapa faida wapinzani wa CCM. 

Hata hivyo, Ole Sendeka amesema wana Simanjiro wanapaswa kuachana na siasa za maji taka kwa kudhani kuwa kila anayeleta maendeleo Simanjiro ana lengo la kugombea ubunge. 

Amesema atamuunga mkono Toima kwani ni mtu mwenye kupenda maendeleo ya wananchi wa eneo la Simanjiro na siyo yake binafsi. 

"Nitakuunga mkono hadharani na pindi saini ya mbunge ikitakiwa ili mambo yaende mbali nitafanikisha hilo bila kikwazo chochote," amesema Ole Sendeka. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Mendukenya amesema shirika la ECLAT Foundation linaloongozwa na Toima limekuwa msaada mkubwa kwao. 

Mendukenya amesema wanatarajia shirika la ECLAT Foundation litawasaidia kumalizia changamoto zinazowakabili kwenye shule hiyo ya msingi Loorng'swani. 
Mwenyekiti wa shirika la ECLAT Development Foundation Peter Toima Kiroya akizungumza na wananchi wa Kata ya Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya kuwakabidhi madarasa mawili, madawati 46 na matundu 16 ya vyoo ya shule ya msingi Loorng'swani yenye thamani ya shilingi milioni 62, kushoto ni mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka na watatu kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Terrat, Kone Mendukenya na madiwani wateule wa Kata za Terrat na Komolo waliopita bila kupingwa Jackson Ole Materi na Baraka Kanunga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...