Na Pamela Mollel ARUSHA 


WAFANYABIARA maarufu saba wa madini ya Tanzanite mkoani Arusha wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini {TAKUKURU} kwa tuhuma za kufanya biashara ya vito ya madini hayo kwa njia ya magendo,utoroshwaji nje ya nchi na ukwepaji wa kodi bila kuzingatia sheria,kanuni,taratibu pamoja na miongozo iliyopo katika biashara ya vito na madini.

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha jana,Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU nchini,Brigedia John Mbungo aliwataja wafanyabishara hao ni pamoja na Joel Mollel maarufu kwa jina la ‘’Saitoti’’ meneja wa kampuni ya kuuuza na kununua madini ya Gem and Rock Venture ya jijini Arusha na mke wake Caren Mollel ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Asia, Rakesh Kumar Gokhroo anayemiliki kampuni ya kuuza na kununuwa madini ya Colour Clarity  ya jijini Arusha.

 

Brigedia aliwataja wengine ni pamoja na Daud Saimalie Lairumbe wakili wa kampuni ya Gem and Rock Venture kutoka kampuni ya uwakili ya Northen Law Chambers Advocates & Legal Cunsultants ya Jijini Arusha,George Poul Kivuyo maarufu kwa jina la Lekoo mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshiriki wa kibiashara wa Saitoti.

 

Aliwataja wengine ni pamoja na Naiman Emmanuel Mollel mchimbaji wa madini ya Tanzanite katika mgodi uliopo Mirerani unaomilikiwa na Kampuni ya Gems & Rock Venture ya Jijini Arusha pamoja na Ezekiel Amon Laizer mchimbaji na mfanyabiashara wa madini na mshirika wa kibiashara wa Saitoti wa jijini Arusha.

 

Mkurugenzi wa TAKUKURU alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa wafanyabiashara Saitoti na Gokhroo kwa kushirikiana na wenzao hao watano wanatuhumiwa kufanya uchimbaji,ununuzi na usafirishaji haramu wa madini ya Tanzanite kutoka katika migodi ya madini hayo yaliyopo huko Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara bila ya kufuata sheria,kanuni na taratibu.

 

Brigedia Mbungo alisema kuwa tuhuma zilizochunguzwa na zinazoendelea kuchunguzwa ni pamoja na watuhumiwa wote wamekuwa wakitumia rushwa kuwashawishi baadhi ya watendaji wa serikali ili kufanikisha azma yao ya kupunguza thamani ya madini husika hivyo kuikoshesha serikali mapato kwa madini husika kupewa thamani ndogo.

 

Alisema wafanyabiasha hao wamekuwa wakipata madini bila kufuata sheria,kanuni na taratibu wamekuwa wakiyauza nje ya nchi kinyume na taratibu na hivyo kuendelea kuikosesha serikali mapato stahiki.

 

Pia wamekuwa wakikwepa kulipa kodi halali ya serikali,wamewawezesha wafanyabiashara hao na wabia wao kutumia fedha hizo na kujijengea ukwasi mkubwa uliowawezesha kununua majengo ya kifahari na magari ya kifahari na kuanzisha biashara mbalimbali Jijini Arusha pamoja na maeneo mengine nchini.

 

Aidha  alisema kuwa ukwasi huo ambao uchunguzi unaendelea kuubaini na ambao unatuhumiwa kupatikana kwa njia zisizo halali,unakadiriwa kufikia Sh. Bilioni 7.2 .

 

Alisema TAKUKURU imebaini kuwa mali kadhaa zinazomilikiwa na watuhumiwa ambazo taasisi hiyo inaendelea kuzifanyia uchunguzi kwani Saitoti ana mali na biashara katika maeneo mbalimbali Jijini Arusha yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 4.7,mke wake anamiliki nyumba na magari yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 610.

 

Brigedia Mbungo alisema Saitoti na mke wake Caren wanamiliki kampuni ya Azo Africa ambayo inamiliki mgodi,magari na mali nyingine zenye thamani ya Sh. milioni 177.5 na kwa ujumla Saitoti anamiliki mali zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 5.5.

 

Alisema mtuhumiwa Naiman Emmanuel Mollel anamiliki nyumba na magari yenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 574,Mfanyabiashara Gohkroo anamiliki magari,fedha taslimu pamoja na madini yenye thamani ya Sh. milioni 895,Mfanyabiashara Lekoo anatuhumiwa kumiliki nyumba na magari yenye thamani ya Sh. milioni 227.

 

Alisema watuhumiwa wote wanachunguzwa na tayari uchunguzi wake unaendelea vizuri na TAKUKURU kwa kushirikiana na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa serikali na watapelekwa katika vyombo vya sheria.


Alisema endapo watatiwa hatiani,adhabu stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na utaifishwaji wa mali zao zilizotokana na ufanyaji wa biashara za madini ya vito kwa njia zilizo kinyume na sheria.

 

Brigedia Mbungo aliwataka wafanyabiashara wa madini ya vito nchini kuwa serikali iko macho sana na haitakuwa na simile au huruma kwa yeyote atayekiuka sheria na kanuni za kufanya biashara ya madini hapa nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...