*Asema anahitajika kiongozi wa kuusimamia kwa maslahi ya Watanzania

*Aweka wazi mikakati ya kufufua viwanda nchini, vikiwemo vya Kilimanjaro

*Azungumzia mkakati wa Serikali wa kuwakatia bima wananchi milioni 60

 

Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kilimanjaro

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amewahakikishia Watanzania kwamba nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa,  hivyo kinachotakiwa ni kupata kiongozi ambaye atasimamia utajiri huo kwa maslahi ya wote.

Pia amesema pamoja na maendeleo makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi cha miaka mitano, mkakati uliopo katika miaka mingine mitano ijayo ni kuhakikisha viwanda vyote ambavyo vimekufa nchini vikiwemo vya mkoani Kilimanjaro vinafufuliwa na hivyo kutoa fursa ya vijana wengi kupata ajira.

Akizungumza leo Oktoba 21,2020, mbele ya maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika uliopo katika Manishaa ya Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro wa Mkoa wa kilamanjaro Dk.Magufuli amesema kutokana na utajiri uliopo nchini , wananchi wanatakiwa kupata kiongozi atakayesimamia utajiri huo na anaamini yeye anafaa kuongoza nchi kwasababu ameonesha anaweza kutokana na yale aliyoyafanya miaka mitano iliyopita.

"Kwa utajiri tulionao nchi yetu inaweza kujiendesha yenyewe...tufanya mengi zaidi, na ndio maana nataka kuwambia wana Moshi na Kilimanjaro, tumebarikiwa kuwa nchi tajiri tunachotakiwa ni kupata kiongozi ambaye atasimamia utajiri huo kwa maslahi ya watanzania wote. Naamini kazi hiyo inanifaa mimi kwani nimeonesha katika miaka mitano.

"Kilimanjaro imeamua kufanya mambo yao, nitabaki na deni kubwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro na deni hilo nitalipa kwa kuwafanyia kazi, nitajituma kwa kuibadilisha Kilimanjaro kwa manufaa ya watanzania wote. Nasema kwa dhati Kilimanjaro na Moshi mmenigusa sana kwa upendo ambao umeonesha , upendo huu ni waajabu , hapa watu wamekusanyika.

"Kabla ya kuanza hutoba yangu nipende kumshukuru Mungu mwingi wa rehema, aliyetujaalia uhai na kutuwezesha kufika hapa leo, nawashukuru viongozi wa dini kwa dua na sala zenu.Hata hivyo naomba nieleze kuanzia mwaka mwaka 2015, tulifuta ada na karo kwa watoto, katika kipindi cha miaka mitano tumetumia Sh.trilioni 1.09 kwa ajili ya elimu bure kwa shule za msingi na sekondari kwa kutumia fedha zetu.Tanzania sio masikini na kitendo cha kulipa fedha hizo ni uthibitisho tosha,"amesema.

 Dk.Magufuli amesema hata nchi za Ulaya pamoja na kuwa tajiri zimeshindwa kutoa elimu bure kwa watuwake kwani wanalipa karo huku akieleza hata katika makusanyo ya kodi katika kipindi cha miaka mitano yameongezeka kutoka Sh.bilioni 850 kwa mwezi hadi Sh. trilioni 1.5 na kuna baadhi ya miezi wanakusanya Sh.trilioni 1.9 na hiyo inadhihirisha Tanzania inaweza kujiendesha yenyewe

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015, Serikali imejenga vituo vya afya 487, zahanati 1,198 , tumepeleka umeme katika vijiji 9700 kutoka vijiji 2018 tulivyovikuta na kwa nchi nzima vimebaki vijiji 2500."Kwa miaka mitano tumeanzisha miradi mikubwa, tumejenga barabara kwa kiwango cha lami kilometa 3,500 na sasa tunaendelea kujenga barabara nyingine kilometa 2,500 kwa kiwango cha lami.

"Tumenunua ndege 11 mpya 11 na katika miaka mitano ijayo tunanunua nyingine tano ikiemo ndege moja ya mizigo ambayo itakuwa inabeba maua kutoka hapa Kilimanjaro kwenda nje ya nchi.Tumenunua rada kubwa mpya na kuzifunga katika Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, KIA, Mwanza na Songwe na ni mambo ambayo yamewezekana sasa ingawa huko nyumba tangu dunia iumbwe yalikuwa hayakuwezekana,"amesema.

Dk.Magufuli aesema katika kudhihirisha nchi ni tajiri wameamua kuanzisha ujenzi wa treni ya kisasa ya umeme ambayo ni ndefu zaidi na kiasi cha Sh.trilioni 7.028 kimetumika na ujenzi wa reli hiyo kutokea Dar es Salaam hadi Dodoma unakwenda vizuri.

Hivyo amesema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa ya viwanda, amefafanua hata Moshi ilikuwa na viwanda vya kila aina, viwanda vya magunia, viwanda va viberiti, viwanda vya ngozi, lakini hivi sasa viwanda vingi vimechaa na havipo, na vilivyopo vinasuasua."Ndio maana tumeanzisha mpango mkubwa wa kuwa na umeme wa kutosha

"Tumeanzisha mradi wa ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo linagharimu mabilioni ya fedha.Naweza kutaja miradi mingi lakini nachotoka kuwaambia tuko pazuri,  hata treni iliyosimama kwa miaka 30 ya kutoka Dar es Salaam hadi Arusha na kupita hapa Moshi leo inafanya kazi, na wananchi wanashuhudia treni.

"Tutafanya mengi zaidi na ndio maana nataka kuwambia wana Moshi na Kilimanjaro tumebarikiwa kuwa na nchi tajiri tunachotakiwa ni kupata kiongozi atakayesimamia utajiri huo kwa maslahi ya watanzania wote,"amesisitiza Dk.Magufuli ambaye amefika kwa wananchi hao kwa ajili ya kuwaomba kura zao ifikapo Oktoba 28 mwaka huu ili wamchague tena aendelee kuleta maendeleo nchini.

Akifafanua zaidi Dk.Magufuli amesema kwa Mkoa wa Kilimanjaro katika sekta ya afya wamefanya vizuri sana katika kipindi cha miaka mitano kwani mbali ya kujenga miundombinu ya sekta hiyo wamenunua vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya Sh.bilioni 4.5 wakati Sh.bilioni moja zimetumika kununua vifaa vya kutibu saratani katika Hospitali ya Kanda."Tunafanya hivyo kupunguza gharama na mateso kwa wananchi kusafiri kutoka Moshi hadi Muhimbili na Ocean Road.

"Kwenye Hospitali ya Rufaa Mawenzi tunakamilisha ujenzi wa wodi za wazazi ambapo ambapo Sh. 6.67 zimetumika pamoja na jengo la wagonjwa wa dharula ambalo linagharimu Sh.milioni 764.99.Tunafanya upanuzi katika hospitali ya rufaa ya magonjwa ambukizi kwa Sh.bilioni 14.33.Tunafanya haya kuhakikisha Watanzania wanapunguza kero na mateso.

"Zaidi ya hapo tunajenga hospitali za Wilaya Rombo na isa, tumefanya ukarabati katika hospitali ya Hai, tunafanya haya kwa ajili ya kusaidia Watanzania na hasa wenye maisha ya shida.Juzi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amezungumzia akina mama walivyokuwa wanafariki kwa shida ya kujifungua kwa mwaka walikuwa wanakufa wanawake 11,000 lakini leo hii tumepunguza sana vifo hivyo na tutaendelea kuvipunguza kwa kuboresha miundombinu.

"Na haya ndio maisha tunataka yawe kwa watanzania wote na ndio maana tulianza kwa kujenga vituo vya afya, kuongeza bajeti ya afya, lengo ni kutoa huduma kwa Watanzania wote bila kuwaacha nyuma.Tulianza na kuboresha huduma za afya badala ya kuzungumzia bima ya afya, huwezi kukata bima ya afya wakati huna hospitali, huna majengo, huna maabara, huna watalaamu.

"Ingawa kuna watu wasema hivi vituo vya afya na hospitali ambazo tunajenga havina maana lakini mimi na fahamu na Moshi wanafahamu huwezi kuzungumzia watu milioni 60 kuwa na bima ya afya wakati huna vituo vya afya.Ukurasa wa 136 wa Ilani ya uchaguzi imepanga katika miaka mitano mingine tuwakatie bima ya afya watanzania wote milioni 60 na hili linawezekana kwani tunajua fedha itatoka wapi,"amesema Dk.Magufuli.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...