*Ni barabara za lami, gati, reli, gesi, viwanja vya ndege na dampo la kisasa

ILANI YA UCHAGUZI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 imeubeba mkoa wa Lindi kwa kupata miradi mingi ndani yake.

 Hayo yamebainishwa na jumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati akiwasomea ilani hiyo wakazi wa mji wa Lindi na vitongoji vyake waliofurika kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana (Jumamosi, Oktoba 24, 2020) kwenye uwanja wa Ilulu, mjini Lindi.

 Akifafanua, alisema katika uk.86, ilani hiyo inaelezea kufanyika kwa ukarabati wa gati la Kilwa ambalo liko mkoani Lindi. “Ukurasa wa 88 katika kipengele cha miradi ya reli inayoendelea, kinataja maandalizi ya ujenzi wa reli ya Mtwara – Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga kwa ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP); uk. 90 Kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja 11 vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Masoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Singida, Musoma na Simiyu,”

 “Uk.92 (ii) inaelezea ukarabati wa vituo saba vya hali ya hewa vilivyopo Zanzibar, Mtwara, Kilwa Masoko, KIA, JNIA, Handeni na Morogoro; Uk.94 (d) inahusu ujenzi wa reli ya Mtwara - Songea - Mbamba-bay na Matawi; Liganga na Mchuchuma (km 1,000) na uk. 95 (h) inataja ujenzi kwa kiwango cha lami wa viwanja vya ndege vya Iringa, Moshi, Lake Manyara, Tanga, Musoma, Lindi, Kilwamasoko, Njombe, Singida na Simiyu.”

 Alisema uk.104 (e) unalezea utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati ambayo ipo katika hatua za mwisho za makubaliano ikiwemo mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi ambayo itaongeza ajira kwa Watanzania na mapato kwa nchi.

 “Uk.171 (n) unaelezea kuimarisha usafi wa mazingira na afya za wananchi kwa kujenga madampo saba ya kisasa katika majiji ya Dodoma, Tanga, Mbeya, Kigoma, Mtwara, Mwanza na Arusha na kukarabati madampo mawili katika halmashauri za manispaa za Moshi na Lindi,” alisema.

 Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Lindi kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Lindi, Bi. Hamida Abdallah na wagombea udiwani wa kata 20 za jimbo hilo.

 Akielezea miradi ya bandari na vivuko, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali iliboresha bandari ya Lindi kwa kufanya ukarabati wa gati kwa thamani ya sh. bilioni 3.1. “Tumefanya ukarabati na ujenzi wa maghala katika bandari za Lindi na Kilwa Masoko ambao umegharimu shilingi bilioni 3.2. Pia shilingi bilioni 1.9 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kivuko cha Kitunda ambacho sasa kinafanya kazi.

 “Serikali inapanga kununua kivuko kingine kipya kwa sababu kilichopo ni cha zamani na imeamua kutengeneza speed boat moja ya kuwalinda. Kati ya boti saba zitakazonunuliwa, moja kituo chake litakuna ni hapa Lindi,” alisema huku akishangiliwa.

 Kuhusu sekta ndogo ya gesi, Mheshimiwa Majaliwa alisema katika azma ya kuwa na mradi mkubwa wa kuchakata gesi asilia (LNG), makampuni ya Equinor na Statoil yanafanya mazungumzo na Serikali juu ya kuanza utekelezaji wa mradi huu. Mazungumzo hayo yapo katika hatua za mwisho. Kwa sasa fidia ya shilingi bilioni 5.2 imelipwa kwa walengwa na usanifu wa kimazingira umeshafanyika,” alisema.

 Akielezea miradi mingine ambayo imeshatekelezwa, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 898 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ufungaji wa taa kwenye barabara za Lindi Mjini na mji wa Ruangwa.

 Kuhusu uboreshaji wa miundombinu, Mheshimiwa Majaliwa alisema wanaLindi wamekula bingo kutoka kwa Rais Magufuli kwani hivi karibuni alitoa sh. bilioni 10 ili kukarabati barabara yenye urefu wa km.90 ya kutoka Lindi kuelekea Dar es Salaam. Pia barabra ta kutoka Mtwara hadi Masasi ya km. 210 itafumuliwa yote na kuwekwa lami ya kisasa. Kwa Lindi, barabara hii inaanzia kule Ndumbwe hadi Nanganga,” alisema.

 Akielezea kazi nyingine zilizokwishafanyika, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara za Ruangwa – Nanjilinji – Kiranjeranje (km 120), Ngongo – Mandawa – Chukuani (km 85), Liwale - Nachingwea - Ruangwa (km 185), Kilwa - Liwale (km 258), Mtwara – Mingoyo – Masasi (Km 200), na Nanganga - Ruangwa – Nachingwea (km 100).

 Alisema Serikali itaanza ujenzi mpya na ukarabati kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mtwara – Newala - Masasi (Km 160) na kwamba imepanga kuanza ujenzi wa barabara ya Nachingwea – Masasi kwa kiwango cha lami (km 45).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...