MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na Rais Mstaaf wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi alipowasili katika uwanja wa Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba,
wakati wa Mkutano wa Kampeni ya Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi. (hayupo pichani) mkutano huo umefanyika leo 21/10/2020.(Picha na Ikulu)
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi Mhe.,Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi akihutubia katika viwanja
vya mpira Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba wakati wa mkutano wake wa
kampeni uliofanyika leo na kuwaomba kura Wananchi wa Pemba na kuwaombea kura Wagombea wote wa CCM.(Picha na Ikulu)

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambae pia
ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali
Mohamed Shein, akimtambulisha Mgombea Ubunge Jimbo la Kiwani Pemba
Ndg.Rashid Abdalla Rashid, wakati wa mkutano wa kampeni ya CCM
uliofanyika katika uwanja wa mpira Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba leo
21/10/2020.(Picha na Ikulu)

MWANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi akiwa na picha ya
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi
akishangiliwa wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa
Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba leo,21/10/2020.(Picha na Ikulu)

VIONGOZI wa Jukwaa Kuu wakifuatilia hutuba ya kumtambulisha
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Mhe.Dkt. Hussein Mwinyi , wakati Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein(hayupo pichani) akihutubia wakati wa mkutano wa kampeni ya CCM uliofanyika Uwanja wa mpira Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba leo
21/10/2020.(Picha na Ikulu)

****************************************

IS-HAKA OMAR, PEMBA

NGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kushika nafasi hiyo, ataimarisha huduma za afya, ili wananchi wapate uhakika wa matibabu.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo uwanjwa wa mpira Jimbo la Kiwani wilaya ya Mkoani, mkoa wa kusini Pemba, kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa chama hicho, uliokuwa na lengo la kuwanadi wagombea wa CCM.

Alisema, hayo ndio kipaumbele chake cha kwanza mara atapomaliza kuapishwa, kwani mambo hayo ni miongoni mwa mambo muhimu kwa wananchi.

Alisema moja ya dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo, ni kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati, na ndio maana anakusudia kuimrisha huduma za afya.

Alisema atakchokifanya ni kuendeleza pale alipoishia rais wa sasa wa awamu ya saba, Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, ambapo anatarajia kuimarisha miundombinu ya afya.

Dk. Mwinyi aliahidi kuwa katika kuimarisha huduma hizo, atajenga nyumba za kisasa za madaktari, ili wapate mahala pazuri na salama pakufanyia kazi zao.

‘’Kama madaktari wetu wakipata nyumba za kisasa za mkaazi inakuwa rahisi sasa kutoa huduma za afya kwa ubora na hilo nalikusudia kulifanya nikiwa rais,’’aliahidi.

Aidha mgombea huyo wa urais aliahidi kuwa, dawa zitapatikana kwa uhakika sambamba na kuajiri kwa wingi madaktari bingwa ili watoe huduma za tiba kwa ufanisi.

Jengine alilowahidi wananchi wa Zanzibar kuwa iwapo atapata ridhaa ni kuimarisha sekta ya elimu, kwa kuwepo maabara za masomo ya sayansi na vifaa vyake.

‘’Elimu ndio msingi wa kila jambo, hivyo kama nikipata ridhaa nitahakikisha hakuna usumbufu wa upatikanaji wa vifaa vya masomo kwa madarasa yote,’’alieleza.

Hata hivyo Dk. Mwinyi ameahidi ujenzi wa nyumba za waalimu sambamba na kuwaendeleza kielimu, mafunzo kwa waalimu ili wawe na ufanisi wa kazi zao.

Katika hatua nyingine Mgombea huyo wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, amesema anakusudia kuinuwa uchumi wa wazanzibari, kwa kuanzisha viwanda mbali mbali vikiwemo vya kusarifia mwani.

Alisema, pamoja na viwanda hiyo mwani huo utaongezwa thamani kwa kuyashawishi makampuni mengi zaidi, ili kununua mwani wa wakulima wa Zanzibar.

“Kilio cha wakulima wa mwani na wavuvi nimeshaskia wakati nakutana na makundi mbali mbali kwenye kampeni zangu, sasa nikichaguliwa kuwa rais, ntahakikisha naimarisha sekta hiyo,’’alihidi.

Katika eneo jingine Dk. Mwinyi alisema mafanikio ya Zanzibar yanategemea sana utendaji kazi wa kila mmoja, hivyo suala la uwajibikaji ni jambo la lazima.

Alisema kuwa, serikali atakayoiongoza hatopenda hata kidogo kuona ndani yake, mna watendaji wasiopenda kuwajibika, kwani wanakuwa kikwazo kufikia maendeleo yaliokusudiwa.

Alisema, jambo hilo ni adui mkubwa wakufikia maendeleo ya Zanzibar, na kuendelea kudumaa kwa baadhi ya sekta, jambo ambalo halikubaliki na atalisimamia kwa dhati.

“Mkinichagua kuwa rais wa Zanzibar, pamoja na mambo kadhaa ambayo ntawafanyia, lakini suala la uwajibikaji ndio kipaumbele cha kwanza, na akitokezea mtendaji kushindwa kuwajibika, ntamuwajibisha,’’alieleza.

Mapema rais wa Zanzibar wa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema CCM imewaletea kiongozi mchapakazi kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa za Dk. Mwinyi za nidhamu, uhodari wa kazi, kuwajali watu wote na ubobevu wa uongozi, hanazo mgombea mwengine yeyote kwa nafasi yoyote kutoka vyama upinzani.

Alieleza kuwa, Dk. Miwnyi amekuwa anajali sana shida za watu na kupelekea kushika nafasi mbali mbali, kuanzia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Kazi iliyofanywa na mikutano yote ya CCM na kisha kupatikana kwa mgombea huyo Dk. Hussien Miwnyi haikukosea, maana uchapakazi wake unaonekana na kila anapokabidhiwa madaraka,’’alieleza.

Hata hivyo rais huyo wa Zanzibar, alisema kutokana na kuelewa vyema majukumu ya urais kutokana na ugumu wake, na jinsi anavyomfahamu Dk. Mwinyi, basi anauweza bila ya wasi wasi.

Alieleza kuwa, Dk. Mwinyi ndio mgombea pekee ambae anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais wa Zanzibar, hasa kwa busara zake na utii wa kazi.

‘’Dk. Mwinyi anafaa kwa asilimia 100 kuwa rais, maana mimi nauwelewa sana na sijaona kiongozi mwengine anaeuweza baada ya mgombea aliyetuliwa na CCM,’’alifafanua.

Hivyo, amewataka wananchi wa Zanzibar kuhakikisha wanawapigia kura viongozi wa majimbo na wadi pamoja na mgombea huyo, ili aendelea kuwatumikia wananchi.

Alifahamisha kuwa, dhamira ya CCM kila siku ni kuona wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, hivyo ili hilo litekelezeke ni kuwapigia kura wagombea wa CCM.

“Siku ya tarehe 28, Oktoba mwaka huu, siku hiyo ya kupiga kura ikifika, muhakikishe hamfanyi makosa, na muwapigie kura rais John Pombe Magufuli, Dk. Hussein Mwinyi, wabunge, wawakilishi na madiwani wetu wote,’’alieleza.

Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, alisema, ushindi wa CCM hauna shaka, kutokana na kuitekeleza vyema ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

‘’Leo kutoka mjini Wete hadi kijiji cha Gando, unatumia dakika zisizozidi 20, maana barabara imejengwa tena kwa kiwango cha lami, hayo ndio mambo ya CCM,’’alisema.

Wakati huo huo wagombea ubunge, uwakilishi wa Jimbo la Kiwani pamoja na madiwani, wamewaomba wananchi hao kuwapigia kura ili kuimarisha maendeleo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...