Mkurugenzi wa Ofisi ya Tume Zanzibar, Hamidu Mwanga akizungumza na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano maalumu ulioandaliwa na Tume hiyo katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, Mwanga amesema kuwa Tume imejipanga katika kuhakikisha uchaguzi mkuu unazingatia katiba ya nchi, sheria na miongozo, leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi msaidizi wa Elimu ya mpiga kura Monica Mnanka akizungumza na wadau wa uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam, na kueleza kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 utakuwa wa huru, haki na kila mwananchi atapata nafasi ya kupiga kura katika mazingira rafiki, leo jijini Dar es Salaam. 


Baadhi ya makundi mbalimbali ya wadau wa uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC,) mara baada ya mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 utakuwa wa huru, haki na wenye kufuata katiba na hiyo ni pamoja na kuruhusu watazamaji wa ndani na nje ya nchi ambapo hadi sasa Tume imetoa vibali kwa Asasi za kiraia na Taasisi 97 za ndani ya nchi na makundi 16 ya watazamaji kutoka nje ya nchi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano maalumu uliowakutanisha na wadau wa uchaguzi kutoka makundi mbalimbali ndani ya Mkoa huo zikiwemo Asasi za kiraia, viongozi wa dini, wawakilishi wa wanawake, vijana, waandishi wa habari na wazee wa kimila Mkurugenzi wa Ofisi ya Tume Zanzibar, Hamidu Mwanga amesema kuwa Tume imejipanga katika kusimamia uchaguzi wa mwaka huu kwa kufuata katiba ya nchi, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali na inaamini kuwa kila mdau akitimiza wajibu wake kwa kufuata taratibu watanzania watapiga kura kwa amani siku hiyo ya uchaguzi mkuu.

"Tume inatumia nafasi hii pia kuwatoa hofu wapiga kura wote wenye mahitaji maalumu kwa kuwa maelekezo yote yametolewa kwa watendaji wa uchaguzi... maelekezo yamewataka kutoa vipaumbele kwa watu, wenye ulemavu, wajawazito, wanaonyonyesha, watakaokwenda na watoto vituoni, Wazee na wagonjwa" ameeleza.

Aidha amesema kuwa Tume imeweka mazingira bora kwa wenye ulemavu wakiwemo wa viungo ambao watatumia vituturi, wasioona watatumia kifaa cha maandishi cha nukta nundu na wasiojua kutumia kifaa hicho na wale wasiojua kusoma na kuandika wanaoruhusiwa kwenda na watu wanaowaamini kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Amesema kuwa katika kipindi hiki cha kampeni Tume imekuwa ikisisitiza vyama vya siasa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeni zao ikiwemo kuepuka lugha za kashfa, maneno ya uchochezi yanayotishia usalama na amani ya nchi pamoja na kufanya kampeni zinazoashiria ubaguzi katika misingi ya jinsi, ulemavu, ukabila, udini, maumbile au rangi.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Elimu ya mpiga kura Monica Mnanka amesema kuwa daftari lina wapiga kura 29,188,347 ambapo wapiga kura 29,059,507 wapo Tanzania bara na 128, 840 wapo Tanzania, Zanzibar na tayari Tume imeshatoa orodha ya wapiga kura kwa wasimamizi wa uchaguzi na vyama vya siasa kwa uhakiki na rejea wakati wa uchaguzi.

Vilevile amesema kuwa Tume inawahikikishia usalama wananchi wote na wajitokeze kwa wingi siku ya Oktoba 28 na kuchagua wawakilishi wao na kurejea majumbani na kusubiri matokeo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...