Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Same

MRADI wa maji wa Bwawa la Mungu ambao ulitakiwa kukamilika mwaka 2017 , umesababisha Rais Dk.John Magufuli kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wizara ya Maji yakiwemo ya kuanza kuchunguzi kuanzia leo na kisha akabidhiwe ripoti haraka huku  walioshirikiana na mkandarasi wa mradi huo kula fedha zaidi ya Sh. bilioni 200 kuanza kuzitapika fedha hizo.

Rais Magufuli ametoa maelekezo na maagizo hayo leo wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati akiomba ridhaa ya kuomba tena kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu ili aendelee kuongoza nchi na kuiletea maendeleo.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi hao msamaha kwa mradi huo kuchelewa kukamilika kwani aliahidi kuutekeleza alipokuwa akiomba kura mwaka 2015 lakini cha kusikitisha hadi sasa haujakamilika ambapo amesema mradi wa maji wa Bwawa la Mungu umeshindwa kukamilika mapema kwani ulitakiwa uwe umekamilika mwaka 2017.

"Hadi leo hii bado, sasa nasema  hapa mkandarasi anayetekeleza, Waziri wa Maji najua anasikia , ndani ya mwezi mmoja  nataka abadilike aongeze kasi ya kumaliza mradi huu nisipoona mabadiliko namfukuza huyo mkandarasi.Haiwezekani wananchi wa Hedaru wazame kisa changamoto za maji wanasubiri mradi huu kwa muda mrefu.

"Hivyo nasema  kwa dhati nawaomba radhi, huyo kandarasi huyu kama wapo marafiki zake, watu wa Wizara ya Maji walikula naye waanze kuzitapika hizo fedha kuanzia leo hii.Ndio maana siwezi kuzungumza uongom ninafahamu kuzungumza uongo ni dhambi. 

"Hivyo iwe Waziri au Naibu ama Katibu na Mkurugenzi kwa sababu bado ni Rais mpaka sasa,kesho waje wakague mradi na mkandarasi wake halafu nikifika Moshi waniletee ripoti yake.Nawaombaradhi nimekosa sana, nisamehe,"amesema Dk.Magufuli.

Hata hivyo amesema anafahamu tatizo la mradi huo ni mkandarsi na kwamba atalala nae mbele kwani haiwezekani Sh.bilioni 262 zilizotolea halafu yeye acheze nazo wakati kazi hadi sasa kazi imefanyika kwa asilimia 64 tu na kama yupo eneo hilo la mkutano hata akimnyima kura hajali.

Wakati akitoa maelekezo hayo Naibu Waziri wa Maji alikuwepo hapo na hivyo amemtaka  pamoja na watalaamu wake wa maji Same, Mkurugenzi wa Mkoa na Wilaya wakae kutafuta ufumbuzi na maagizo yake yapo pale pale.

"Nasema ukweli nitawafukuza wezi na ikiwezekana nitatoa amri awekwe ndani mkandarasi kwani haiwezakani wapo watu waliokufa kwa kukosa maji. Kama mlipata mkandarasi wa kughushi  mwende mkatatue,haiwezekani nikawa Rais halafu maji hayapo na kama ni fedha nilitoa tayari kakaeni mtafute suluhu."


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...