Na Muhidin Amri,
Tunduru

SERIKALI ya kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru kilichopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Msumbuji,kimetoa ardhi yenye ukubwa wa ekari 3,000 kwa ajili ya kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo cha  zao la ufuta katika msimu wa 2021.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Silaju  Said alisema, hapo awali eneo hilo lilitengwa kwa ajili ya makazi ya jeshi la wananchi Tanzania, hata hivyo  serikali ya wilaya ikiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro wameona ni vizuri eneo hilo liwe sehemu ya mradi wa kilimo cha ufuta kutokana na ardhi yake kuwa mzuri kwa kilimo.

Alisema, katika mradi huo  makundi mbalimbali  ikiwemo shule, muungano wa vyama vya wakulima(Mviwata) yatapewa  maeneo ambapo ameipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuimarisha zao la ufuta ambalo ni la pili kuwaingizia fedha nyingi wakulima wa wilaya ya Tunduru .

Alisema,  wametoa eneo hilo kwa manufaa ya jamii na pia itasaidia wakazi wa kijiji hicho na  vijiji vya jirani kwenda  kujifunza kilimo bora cha ufuta pindi mradi utakapoanza na  utafungua fursa kwa wakulima kupata  masoko na taasisi mbalimbali kwenda kuwekeza katika shamba hilo.

Baadhi ya wananchi wa Makande Adinan Kihosa na Tabia Ali wameshukuru kupelekewa mradi wa kilimo cha ufuta kwani mbali  kuwapatia kipato cha uhakika,pia utasaidia kupata elimu ya kilimo cha kisasa ambacho kitakwenda kumaliza suala la umaskini wa kipato katika familia zao.

Tabia Ali alisema,  mbali ya mradi huo kuwa sehemu ya kujifunza kama shamba darasa utakwenda kupunguza tatizo la vijana wengi kukaa vijiweni, kwa sababu baadhi yao watapata shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.

Hata hivyo,ameiomba serikali kupitia Benki ya maendeleo ya kilimo ambayo ndiyo itatoa fedha za mradi kuhakikisha  inatoa fedha hizo mapema ili wakulima na vikundi vitakavyoingizwa kenye mradi huo waweze kuwahi msimu wa kilimo kwani tayari mvua za kwanza zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya  ya Tunduru.

Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisa alisema,mradi wa kilimo cha ufuta katika wilaya hiyo umelenga sana vikundi vidogo vidogo ambavyo vitaungana pamoja na vitapata fedha kutoka kwa chama kikuu cha ushirika TAMCU ambayo imebeba dhamana ya kusimamia mradi huo.

Alisema, mradi wa kilimo cha ufuta umegawanyika katika meneo mawili ambayo ni shamba la ushirika kijiji cha Pacha nne kata ya Namiungo ambalo litachukua vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na pili ni shamba la Makande ambalo litahusisha kwa vikundi maalum vilivyoonesha nia ya kulima zao hilo.

Kwa mujibu wake, kwa kuanzia mradi huu utaanza kwa kilimo cha kutegemea mvua ambapo hunyesha kuanzia katikati ya mwezi Novemba,hivyo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba inatakiwa mashamba yote yawe yamelimwa ili mwishoni mwa mwezi Desemba kazi za kupanda zianze na kukamilika katikati ya mwezi Januari kwa kuwa maeneo hayo yamezungukwa na maji.

Alitaja mategemeo ya mradi ni kuleta tija kwa wana vikundi kujitegemea kiuchumi kutokana na faida itakayopatikana kwenye mradi na kuacha kutegemea chanzo kimoja cha mapato ambacho ni ushuru wa mazao,kuongezeka uzalishaji wa ufuta,kutoa ajira kwa baadhi ya wana vikundi ambapo zaidi ya watu  20,000 hususani vijana watapata ajira.

Alisema, kwa kuanzia chama kikuu cha Ushirika Tamcu ambacho ndiyo wasimamizi wakuu  wa mradi huo kimejipanga kuomba kwa makubaliano maalum taasisi ya Magereza na vijana wa jeshi la akiba kufanya kazi katika mashamba yote mawili.

Mwenyekiti wa kijiji cha Makande kata ya Lukumbule wilayani Tunduru Silaju Said aliyenyoosha mkono katikati akiwaonesha baadhi ya  wataalam wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Afisa kilimo anayeshughulikia mazao Gallus Makwisa wa kwanza kulia,afisa ushirika George Bisan wa pili kushoto na mjumbe wa chama kikuu cha ushirika Tamcu Ltd Zainabu Yassin.

Baadhi ya wananchi  viongozi wa Serikali ya kijiji cha Makande na wataalam wa kilimo ba ushirika kutoka halmashauri ya wilaya Tunduru wakikagua eneo la shamba lililopangwa kutumika kwa ajili ya mradi wa kilimo cha ufuta katika msimu wa 2020/2021.

Picha na Muhidin Amri

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...