Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi Injini ya Boti kwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi, Zilagula, Agness Mbasha katika hafla fupi ya kugawa Injini za Boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika katika Wilaya ya  Muleba, Mkoani Kagera Oktoba 23, 2020.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wawakilishi wa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria muda mfupi baada ya kukabidhi Injini za Boti kwa Vyama (4) vya Ushirika wa Wavuvi Oktoba 23, 2020. Kutoka kulia waliokaa ni Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Huduma za Ugani za Uvuvi, Anthony Dadu na wapili kutoka kulia ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utafiti na Mafunzo ya Uvuvi, Dkt. Erastus Mosha. Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Omary Mchengule na wapili kutoka kushoto ni Kaimu Mwenyekiti, Chama cha Ushirika cha Wavuvi, Zilagula, Agness Mbasha.

Injini za Boti (4) aina ya Yamaha ambazo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imezikabidhi kwa Vyama vinne vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria katika hafla fupi iliyofanyika Wilayani Muleba, Mkoani Kagera Oktoba 23, 2020.

**********************************************

Na Mbaraka Kambona, Kagera

Katika kuhakikisha shughuli za Wavuvi zinaboreshwa ili kukuza kipato chao, Serikali imegawa Injini za Boti nne (4) aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi milioni 35 kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi vinne vinavyofanya shughuli zao katika Ukanda wa Ziwa Victoria.

Wakati akikabidhi Injini hizo kwa Wavuvi Wilayani Muleba Mkoani Kagera jana, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid  Tamatamah alisema kuwa ugawaji wa Injini hizo  ni katika kutekeleza moja ya majukumu ya Wizara ya kuhakikisha wanawezesha upatikanaji wa utaalamu, rasilimali fedha na vitendea kazi ili kuwasaidia Wavuvi kuboresha kazi zao na kuendeleza sekta ya uvuvi kwa ujumla.

Dkt. Tamatamah alisema kuwa katika kuhakikisha Vyama vya Wavuvi vinawezeshwa,  mwaka wa fedha 2020/ 2021 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga shilingi milioni mia mbili (200,000,000) kwa ajili ya kuviwezesha vyama vya Ushirika vya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji.

“Rai yangu kwa Vyama hivi vya Ushirika  wazitumie injini hizi kwa kufanya uvuvi endelevu na kuachana na uvuvi haramu”, alisema Dkt. Tamatamah

“Nawahamasisha pia wavuvi wajiunge katika vikundi vya ushirika ili iwe rahisi kuwezeshwa kwa mikopo na vitendea kazi ili waweze kujikwamua kiuchumi”,aliongeza Dkt. Tamatamah

Kuhusu muitikio wa Wavuvi kujiunga na Vyama vya ushirika, Dkt. Tamatamah alisema kuwa muitikio ni mzuri na Wilaya ya Muleba imekuwa kinara wa kuanzisha vyama hivyo.

Akiongea baada ya kupokea Injini ya Boti, Mwakilishi wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi, Izigo, Wilayani Muleba, Naziru Kassanga alisema kuwa  Injini hiyo ya Boti waliyopatiwa itawasaidia sana wao kama wavuvi wadogo wadogo kufanya uvuvi wa kisasa utakaowasaidia kuboresha maisha yao.

“Injini hii itatusaidia sisi wavuvi wadogo kwenda kuvua katika kina kirefu kwa urahisi na kuondokana na uvuvi wa kienyeji ambao tija yake ni ndogo”, alisema Kassanga

Naye, kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi cha Zilagula,Wilayani Buchosa,  Agnes Mbasha aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwakabidhi boti ambayo anasema itawasaidia kufanya doria ya kulinda nyavu zao dhidi ya wezi.

“Nitumie nafasi hii pia kuwahamasisha wanawake wenzangu kujiunga na Vyama hivi vya Ushirika kwani vinasaidia sana kujikwamua kimaisha”,alisema Mbasha

Kuhusu  Vyama vya Ushirika kuunganishwa na taasisi za fedha, Dkt. Tamatamah alisema mikopo iliyoombwa na kupitishwa kwa ajili ya vyama vya ushirika ni shilingi bilioni 2.6 na ambayo tayari imeshatolewa ni shilingi milioni 873.8 na vyama 14 viko katika hatua za mwisho kupatiwa mikopo.

“Wizara imeihamasisha Benki ya Posta Tanzania (TPB) kuzindua akaunti ya Wavuvi (Wavuvi account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa Wavuvi hususani wavuvi wadogo”,alifafanua Dkt. Tamatamah

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...