WATUMISHI wa Tume ya Madini nchini wametakiwa kuwa waadilifu kwenye utendaji wa shughuli zao za kila siku na  kuendelea kujenga taswira chanya kwenye Sekta ya Madini.

Wito huo umetolewa leo tarehe 22 Oktoba, 2020 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli za Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Manya ameambatana na Meneja Utawala na Rasilimali watu, Gift Kilimwomeshi na kupokelewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Godson Kamihanda.

Akizungumza na watumishi hao Profesa Manya amesema kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye Sekta hiyo  na kusisitiza kuwa uadilifu kwenye utendaji kazi unahitajika ili kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye Sekta ya Madini.

Katika hatua nyingine, Profesa Manya amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi ili kujenga jina zuri la Tume ya Madini.

Ziara hiyo ni sehemu ya ziara ya Profesa Manya katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini yenye lengo la kukagua utendaji wa Ofisi za Madini, kusikiliza changamoto za watumishi na kuzitatua huku elimu kuhusu utumishi wa umma na maelekezo mbalimbali yakitolewa.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa ofisi hiyo katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Godson Kamihanda amesema kuwa wamefarijika na ujio wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kwenye ofisi hiyo na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa.

"Tunashukuru na kumpongeza sana Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na Meneja Utawala na Rasilimali watu, Gift Kilimwomeshi kwa kututembelea na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatukabili pamoja na kutupa ufafanuzi wa miongozo mbalimbali kwenye utendaji wa shughuli za Serikali, ninaamini elimu kubwa waliyotupa itatusaidia kutatua changamoto ndogo zilizokuwa zinatukabili," amesema Kamihanda.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...