Na Benny Mwaipaja, Kigoma


WAZIRI wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Dkt. Philip Isdor Mpango, ameyaagiza mabaraza ya Madiwani kote nchini, kuhakikisha kuwa fedha za miradi zinazotumwa na Serikali katika maeneo yao zinasimamiwa vizuri ili kuleta tija na maendeleo ya jamii

Dkt. Mpango ametoa rai hiyo katika kata ya Mnanila mkoani Kigoma, wakati akiwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kura za kishindo, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeye binafsi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Alionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa watumishi wa umma watakaohusika kwa namna yoyote ile kujihusisha na vitendo vya ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na uzembe utakaoisababishia Serikali hasara.

“Hao mafisadi na wabadhirifu wa fedha za umma nawaonea huruma kwa sababu kisu nimepewa mwenyewe na Waziri wa Fedha hana mipaka, popote ilipo fedha na mali ya umma, akawapo mwizi, mbadhirifu, huyo ni halali yangu” alisema Dkt. Mpango.

Mishahara ya Watumishi wa Umma 

Dkt. Mpango aliahidi kuwa Wizara yake imejipanga kutekeleza ahadi iliyotolewa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kuhusu kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo nyongeza ya mishahara yao ili kuboresha na kukuza kipato chao.

“Kwahiyo lazima tufanyekazi ya kukusanya mapato na kutumia fedha vizuri ili watumishi hawa wanaohangaika kila siku na walau wapate kamshahara ambako kanasaidia zaidi” alisisitiza Dkt. Mpango.

Masuala ya Kipaumbele Jimboni Buhigwe

Dkt. Mpango aliwaahidi wakazi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kwamba atatekeleza ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni na zile zilizoko kwenye Ilani ya CCM, lakini kwa kuanza ameyapa kipaumbele masuala mawili ambayo ni Ujenzi wa Barabara yenye urefu wa kilometa 2 inayoelekea kwenye Hospitali ya Misheni ya Heri pamoja na kutatua changamoto sugu ya maji katika tarafa ya Manyovu.

“Katibu Tawala wa Wilaya ya Buhigwe, Bw. Peter Masinde, kawaambie Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini TARURA, kwamba, nataka kuona barabara ya Manyovu hadi Hospitali ya Misheni-Heri inapitika wakati wote, wakati tunatafuta lami ya kujenga kipande hicho cha barabara cha kilometa mbili!” aliongeza Dkt. Mpango.

Kuhusu Sekta ya Maji, Dkt. Mpango alieleza kuwa katika mkataba wa ujenzi wa mradi wa barabara ya Kigoma- Buhigwe hadi Kasulu kuna kipengele cha mkandarasi kutakiwa kusambaza maji katika eneo la Manyovu na kwamba hatua hiyo itapunguza kero ya maji hususan kwa akina mama na watoto. 

Awataka wana Kigoma kuchangamkia fursa mbalimbali

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, aliwataka wakazi wa Jimbo la Buhigwe na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, kuchangamkia fursa ya ujenzi wa meli mbili mpya pamoja na meli nyingine mbili za MT Sangara na MV Liemba zitakazo karabatiwa na kufanya safari zake katika Ziwa Tanganyika, ili kukuza biashara na kujipatia kipato.

“Serikali itajenga meli mpya mbili moja ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 na meli nyingine itakuwa ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 4,000 na pia tutakarabati meli ya kubeba mafuta MT Sangara na kukarabati meli nyingine ya MV Liemba, ambazo zitatumika kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani” Alifafanua Dkt. Mpango.

Awataka wananchi wajenge utamaduni wa kuweka fedha zao Benki 

Katika hatua nyingine Dkt. Mpango amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Buhigwe, kujenga tabia ya kuhifadhi fedha zao benki kwa ajili ya usalama wa fedha zao na kuwezesha uwepo wa mzunguko mzuri wa fedha.

Alisema kuwa ameanza kuzishawishi Taasisi za Fedha hususan mabenki kujenga matawi yao ya Benki katika Wilaya ya Buhigwe lakini changamoto kubwa iliyo ainishwa na taasisi hizo ni kwamba wananchi wa wilaya hiyo hawana utamaduni wa kuweka akiba zao benki.

Kukuza Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Utalii

Dkt. Mpango, aliwataka wakazi wa Wilaya ya Buhigwe kuchangamkia fursa ya kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo kahawa, michikichi, maparachichi, mkwa, mbogamboga na tangawizi ili kufaidi soko la kitaifa na kimataifa katika nchi ya Burundi.

Alisisitiza pia ufugaji wa kisasa na wenye tija pamoja na kuwashauri wananchi kuanzisha ranchi za kufuga wanyamapori pamoja na kuanzisha utalii wa kiutamaduni ili kukuza kipato chao na kuondokana na umasikini.

Serikali kuondoa kodi zenye kero kwa wajasiliamali

Dkt. Mpango aliahidi kuwa katika kukuza Sekta Binafsi, ikiwemo masuala ya uwekezaji na biashara za wajasiliamali wadogo, Serikali itachambua na kuondoa kodi mbalimbali zinazokwaza Sekta Binafsi ili kuwezesha mazingira mazuri ya ufanyaji biashara, kukuza ajira na mitaji.

“Lazima tutoe kipaumbele kukuza ujasiliamali, kuwasaidia wafanyabiashara, wenye viwanda vidogo vidogo, watoa huduma, na tutakuwa na jicho tofauti kukuza sekta hizo kwa kuondoa kodi zinazowakandamiza” Alisisitiza Dkt. Mpango.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na baadhi ya wananchi wa Kata ya Mnanila, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, alipofanya ziara katika Jimbo la Buhigwe kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kishindo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na yeye binafsi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (WA TATU KUSHOTO), akipita kwenye mitaa ya Kijiji cha Mnanila, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma, alipofanya ziara katika Jimbo la Buhigwe kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kwa kishindo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na yeye binafsi wakati wa uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni. (Picha na Josephine Majura – KIGOMA).

Baadhi ya viongozi wa Ulinzi na Usalama Wilaya ya Buhigwe, wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isodor Mpango (Mb), (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kata ya Mnanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.


Baadhi ya wakazi wa Kata ya Mnanila, wakifuatilia kwa makini Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye amewaahidi wakazi wa Jimbo hilo kwamba ahadi zote zilizoainishwa kwenye Ilani ya CCM kwenye Jimbo hilo katika sekta mbalimbali zitatimizwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Diwani wa Kata ya Mnanila Mhe. Pius Kagoma, akimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ambaye ni Mbunge wa Buhigwe, kwa kuchaguliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa mara nyingine na kuahidi kumpa ushirikiano katika kutelekeza majukumu yake kwenye Kata hiyo iliyopo wilayani Buhigwe mkoani Kigoma. 

Mkazi wa Mnanila, Bw. Moses Luhaji, akimuomba Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), kutatua kero ya gharama kubwa wanayotozwa kununua vifungashio vya kahawa, alipofanya ziara katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Buhigwe Bw. Peter Masindi, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, akifafanua jambo kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), alipotembelea Kata ya Munanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akizungumza na Wananchi wa Kata ya Mnanila, ambapo ameahidi kuanza kutekeleza miradi miwili ya kipaumbele ikiwemo ujenzi wa Barabara ya kilometa mbili kutoka Mnanila hadi Hospitali ya Misheni-Heri ma mradi wa maji katika Tarafa ya Manyovu, mkoani Kigoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akisalimiana na Mkazi wa Kijiji cha Mnanila, wilayani Buhigwe, Kigoma, Bw. Muzeye Lukanga, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata ya Mnanila, Tarafa ya Manyovu, mkoani humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...