Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Liwale

HALMASHAURI ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi imesema kuna faida nyingi wanazopata kutokana na uwepo wa rasimali ya misitu katika maeneo yao huku akitumia nafasi hiyo kueleza jitihada zinafanyika kuhakikisha misitu inalindwa na kuhifadhiwa vizuri wakati wote.

Pia imepongeza mashirika na wadau mbalimbali wakiwemo wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) pamoja na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania(TFCG).MJUMITA na TFCG kwa sasa wanasimamia utekelezaji wa mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu(CoFoREST)chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi(SDC).

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari , Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi James Milanzi amesema wilaya yao imebahatika kuwa na misitu mingi ingawa baadhi ya wananchi hawajui faida zake au wanaitumia vibaya, hivyo mpango huo wa MJUMITA na TFCG umekuja wakati muafaka kwani utachochea kutoa elimu ya wananchi kushiriki katika uhifadhi wa misitu.

Amefafanua kiasili wananchi wao wengi wanajihusisha na kilimo na hasa kilimo cha kuhamahama."Leo wanalima hapa, kesho wanalima kwingine na kila wanapohama wanakwenda kufyeka msitu.Kwa hiyo hii ni changamoto iliyopo ndani ya Wilaya yetu, miradi kama hii ya CoFoREST) inapokuja inasaidia kuelimisha wananchi wetu.

"Mipango hii mizuri ya wadau hao na wengine wengi kwetu  halmashauri inatusaidia, moja kukuza kipato cha wananchi wetu , vijiji ambavyo vimeanza na huu mpango wa matumizi bora ya ardhi sasa wameanza kupata manufaa , kupitia uvunaji wa mazao ya misitu, kwa mwaka wa fedha uliopita tumepata sio chini ya milioni Sh.150.

"Na hiyo ni kutokana na asilimia tano ya kipato chote ambacho kijiji kimepata kutokana na uvunaji misitu, kwa mujibu wa watalaam wanatuambia sasa asilimia inakwenda kuongeza kutoka tano hadi asilimia 10, hivyo mapato yataongezeka.Kwa hiyo halmashauri inanufaika,"amesema.

Ameogeza manufaa mengine kwa halmashauri ni maeneo ambayo yanahudumiwa na halmashauri kwa hiyo mipango yao ni kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya maeneo hayo katika ujenzi wa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii.

"Unapozungumzia ujenzi wa madarasa, vyoo, zahanati, ofisi na huduma nyingine halmashauri inatakiwa kutenga fedha lakini kama kuna chanzo kingine basi chanzo hicho kinaisaidia halmashauri kuekeleza majukumu yake ya kuhudumia wananchi ,

"Kwa hiyo ni manufaa makubwa kwetu sisi halmashauri.Kwa hiyo wananchi wanaweza kutekeleza majukumu yao kupitia fedha ambazo wanazipata kutokana na uwepo wa rasilimali ya misitu,"amesema Milanzi.

Aidha amesema kutokana na faida ambazo zinaonekana kupitia miradi ya uhifadhi misitu ,ameweka wazi  wanayo mipango ya kuhakikisha miradi hiyo inakwenda katika vijiji vingine ili navyo viweze kunufaika.

Akizungumzia uharibifu wa mazingira, amesema kuna mipango mingine inaendelea ikiwemo ya kutoa elimu kwa wananchi kuwa wanayo nafasi ya kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na baadae, tunawahimiza wananchi kushiriki kutunza mazingira ikiwemo misitu iliyopo kwenye maeneo yao.

"Na wananchi kupitia miradi hii na faida ambazo zinaonekana zinasaidia kuwafanya waelewe na kuona umuhimu wake.Kuhusu ushirikiano kati ya serikali na taasisi kama MJUMITA NA TFCG kwa kweli tunafurahi sana, miradi wanayofanya mbali ya kunufaisha wananchi, pia inafanya halmashauri kuongeza kipato.

"Inatusaidia  kutekeleza majukumu ambayo tunayo, kwani unapopata chanzo kingine cha fedha maana yake unakwenda kujazia pale ambapo hapajaaa , kwa maana ya kwamba tunaongeza nguvu zaidi na  sisi halmashauri inapokuja miradi ya aina hii tunaiunga mkono na kuna mashirika mengine ya aina hii ambayo wanafanya kazi zinazofanana na MJUMITA.

Kwa upande wake Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA, Elida Fundi amesema "tumekuja na mradi wa kuhifadhi misitu kupitia biashara endelevu ya mazao ya misitu inayofahamika(CoFoREST). Mradi kama huu umekuwa ukitekelezwa katika Mkoa wa Morogoro katika wilaya tatu za Kilosa, Morogoro na Mvomero , tumekuwa tukiutekeleza kwa awamu na sasa tumepata awamu ya tatu itakayokwenda mpaka mwaka 2023.

 ."Kwa hiyo mradi huu wenyewe sasa tulikuwa tunatekeleza na muundo ambao umelenga katika kuanzisha usimamizi shirikishi katika vijiji pamoja na kuanzisha dhana ya uzalishaji wa mazao ya misitu kwenye usimamizi wa misitu na hii yote inalenga kuhamasisha uhifadhi wa misitu.

"Na kutoa motisha kwa jamii zinazohifadhi misitu waweze kunufaika na ile misitu na kuisimamia kwa nguvu zote na hii imeweza kufanikiwa katika Mkoa wa Morogoro, tukaona tusiishie Morogoro bali twende na wilaya zingine nne.

"Hivyo tunategemea kwenda katika wilaya nyingine nne katika kipindi hiki cha miaka mitatu ikiwemo Wilaya ya Liwale ambako tutakuwa tunatoa mafunzo na kuwa na kijiji cha mfano kimoja.Pia tupo na Wilaya ya Kilolo katika kijiji cha Mahenge,"amesema.

Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Liwale Mosses Mkoveke amesema ushiriki wa jinsia katika masuala ya uhifadhi wa misitu umekuwa wa kuridhisha kwani wanaume na wanawake wanashirikiana  vizuri.

"Katika masuala ya misitu kwa sasa wanawake wako sawa na wanaume katika kupata taarifa kuhusu misitu, uongozi na usimamizi wake , katika Kamati za misitu zilizopo vijiji, robo tatu ya wajumbe wote wawe wanawake, na vile vile katika nafasi tatu za uongozi ambazo ni Mwenyekiti , Katibu na Mtunza hazina, mmojawapo asikosekane mwanamke.

"Tumefanya hivyo kwasababu wanawake ni watumiaji wakubwa wa rasilimali zinazotokana na misitu, ndio wanafuata kuni, maji, mbogamboga na matunda yanayopatikana kule porini , kwa hiyo tunatenga muda wa kutosha kuwajenga uwezo kwa wanawake kuweza kutambua na kuthamini na kutenga muda wa kutosha kushiriki, kusimamia na kupanga pamoja maendeleo ya misitu katika vijiji wanavyoishi,"amesema Mkoveke.

 Moja ya jengo la darasa la shule ya msingi ambalo limegharimu Sh.milioni 18 ambalo limejengwa kutokana na fedha ambazo zinatokana na rasilimali ya misitu iliyopo kijiji cha Mtawatawa.

Ofisa Misitu Wilaya ya Liwale mkoani LindiNassoro Mzui (watatu kulia), Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA Elida Fundi(wa nne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wasimamizi wa misitu wa Mbila baada ya kutembelea msitu huo ambao umekuwa na faida lukuki kwa wananchi.

Kaimu Mtendaji  wa Serikali ya Kijiji cha Mtawatawa kilichopo wilayali Liwale mkoani Benadetha Kitang'ita akitoa taarifa ya maendeleo yaliyopatikana kupitia miradi ya usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii.

Baadhi ya wanakijiji wa Mtawatawa walioko katika Kamati ya Usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii wakiwa katika mkutano baada ya maofisa kutoka Mtanadao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania(MJUMITA) pamoja na waandishi wa habari walipofanya ziara ya kutembelea kujiji hicho kuona mafanikio ambayo yamepatikana kutokana na usimamizi shirikishi wa misitu.


Kaimu Mtendaji  wa Serikali ya Kijiji cha Mtawatawa kilichopo wilayali Liwale mkoani Lindika (kushoto)Benadetha Kitang'ita akipiga hesabu ya fedha za kijiji hicho zilizotumika katika shughuli za maendeleo.Fedha hizo zinatokana na usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii (USMJ) unaoratibiwa na na mashirika mbalimbali na Serikali.Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtawatawa Omary Shamte

 

Kulia ni Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA Elida Fundi akiwa makini kuandika maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi James Milanzi.Kaimu huyo Mkurugenzi alikuwa akilezea faida ambazo wilaya hiyo inapata kutokana na uwepo wa misitu ya asili katika wilaya hiyo.

 

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi James Milanzi akielezea mikakati ya Wilaya hiyo katika kuhakikisha misitu ya asili iliyopo ndani ya wilaya hiyo inaendelea kutunzwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wa MJUMITA pamoja na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) kupitia mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara ya mazao ya misitu tanzania(CoFoREST).

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi James Milanzi(kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari baada ya kutembelea miradi ya usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii katika Kijiji cha Mtawatawa.Kulia ni Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA Elida Fundi aliyekuwa akiongoza msafara waandishi hao(hawapo pichani).

Ofisa Maendeleo Wilaya ya Liwale mkoani Lindi ...Kulia na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtawatawa(watatu kulia) wakiwa pamoja na Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mtawatawa Benadetha Kitang'ita(wa pili kulia) wakati wa mkutano wa kujadili masual mbalimbali yanayohusu usimamizi shirikishi wa misitu ya jamii.

Moja ya wasimamizi wa misitu wa Mbila akiwa makini kumsikiliza Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA Elida Fundi(hayupo pichani) wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho kuhusu umuhimu wa kuendelea kutunza misitu ya asili ukiwemo msitu wa Mbila uliopo kwenye kijiji hicho.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...